Haya ndiyo malipo kwa wazalendo?

Januari 28, 2016: Wafanyakazi wa TanzaniteOne waliuandikia notisi uongozi wa mgodi huo kupitia Chama cha Wafanyakazi Mgodini (TAMICO) baada ya haki na masilahi yao kukiukwa na mgomo huo ulipaswa kuanza Februari 1, 2016.

Hata hivyo mgomo huo haukufanikiwa baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mikoa mitatu ya Arusha, Kilimajaro na Manyara kupitia kwa Mwenyekiti wake, Amos Makalla, kufika sehemu ya kazi na kufanya vikao na wafanyakazi na uongozi wa TanzaniteOne na kufikia suluhu. Wafanyakazi waliendelea na kazi.

Februari 8, 2016: Baada ya uongozi wa TanzaniteOne kutotii maagizo ya serikali, hasa ya muda mfupi yaliyoafikiwa kwenye vikao vya Februari 1, 2016 na kutolipa mishahara ya wafanyakazi wengi kama ilivyoagizwa mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mikoa mitatu, uongozi uliwaandikia wafanyakazi 201 notisi ya kuwaachisha kazi baada ya wao kuulizia mishahara yao ya Januari 2016 na mshahara wa 13 wa Desemba, 2015.

 Februari 9, 2016: Baada ya wafanyakazi 201 kufukuzwa, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mahmoud Kambona, alifika TanzaniteOne akitaka kufahamu kwanini wafanyakazi 201 walifukuzwa.  Alifanya vikao viwili na uongozi wa kampuni na wafanyakazi 201. Alisema wafanyakazi hao walifukuzwa pasipo kufuata taratibu, hivyo TanzaniteOne wawarejeshe na wasiajiri wafanyakazi wengine hadi suala la wafanyakazi hao 201 lipatiwe ufumbuzi.

TanzaniteOne walikaidi agizo hilo na Februari 9, 2016 walibandika tangazo la ajira kinyume cha maagizo ya mkuu wa wilaya; jambo lililomuudhi kiongozi huyo na kuagiza Meneja Rasilimali Watu wa TanzaniteOne akamatwe kwa kudharau maagizo yake. Akaagiza awe amepata majibu ndani ya siku tatu.

Februari 10, 2016: Kutokana na notisi, wafanyakazi hao walifika TanzaniteOne kuchukua barua za kuachishwa kazi, lakini barua hizo zilibainika zina makosa. Hazikuwa na mhuri wa kampuni kwa hiyo waliambiwa waziache, badala yake wazichukue Februari 19, 2016.

Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi mgodini hapo ambao ndio asilimia kubwa waliofukuzwa walikutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) aliyekuwa akiitwa Zena na timu yake aliyotoka nayo Dar es Salaam ili kujua sababu za kufukuzwa wafanyakazi hao.

Alisema kisheria uongozi wa TanzaniteOne ulifanya makosa kuwafukuza wafanyakazi. Akashauri viongozi wa wafanyakazi wakafanye kikao cha nidhamu. Viongozi hao waliwauliza kati ya kufukuzwa kazi na kikao cha nidhamu kipi kinatangulia?

Wafanyakazi waliofukuzwa walikwenda TanzaniteOne kufuatilia maagizo yaliyotolewa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro. Walitaka kutekeleza maagizo ya siku tatu walizopewa TanzaniteOne za kuwarudisha kazini. Walipofika walikuta tangazo kwenye ubao wa matangazo langoni linalowataka waende kwenye kikao cha nidhamu tu.

Februari 22, 2016: Wafanyakazi 201 waliofukuzwa walionana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mikoa mitatu – mkoani Kilimanjaro kumweleza kuwa wamefukuzwa kazi ilhali maagizo waliyoafikiana yakiwa hayajatekelezwa.

Mwenyekiti aliwasomea maagizo rasmi ya serikali yaliyotoka Wizara ya Madini kuhusu malalamiko 14 ya wafanyakazi hao.

Aliwaeleza kuwa Naibu Waziri mwenye dhamana ya Kazi na Ajira, Anthony Mavunde, amempigia simu muda huo kuwa yuko njiani anakwenda TanzaniteOne, hivyo wafanyakazi hawana budi kuonana naye.

Wafanyakazi walitii maelekezo. Naibu Waziri akawaambia: “Serikali haina kauli mbili”; kwa maana  kwamba maagizo 14 yaliyotoka Wizara ya Madini kuhusu malalamiko 14 ni lazima uongozi wa TanzaniteOne uyatekeleze. Akasema kuwafukuza wafanyakazi bila kutekeleza  maagizo hayo ni dharau kwa serikali, na haitakuwa tayari kukubali.

Mavunde  alipomaliza kikao na wafanyakazi 201; aliwakutanisha viongozi wa chama cha wafanyakazi na uongozi na wataalamu aliotoka nao wizarani, na mkuu wa wilaya.

Naibu waziri aliwaambia TanzaniteOne kuwa aina ya ufukuzaji waliofanya hauwezi kumaliza mgogoro.

Fabruari 24, 2016: TAMICO walipata barua kutoka uongozi wa mgodi wakitakiwa wahudhurie kikao cha usuluhishi kama ilivyoagizwa na Mavunde chini ya usimamizi wa aliyekuwa mkuu wa wilaya.

Februari 26, 2016: Viongozi wa TAMICO walifika eneo lililoelekezwa kwenye barua ya kuwataka wahudhurie kikao ambacho kilifanyika, lakini uongozi wa TanzaniteOne ulisema msimamo wao ni ule ule – kutowarejesha wafanyakazi hao kazini. Msuluhishi aliyeachiwa kazi hiyo, Mavunde, uongozi wa mgodi haukumtaarifu kuwa kutakuwa na kikao hicho.

Februari 26, 2016: Mmoja wa viongozi wa TAMICO alimpigia simu mkuu wa wilaya na kumuuliza kwanini hakuonekana kwenye kikao cha usuluhishi. Alisema hakupewa taarifa na uongozi wa kampuni. Akasema amekwisha kumaliza kazi yake, kwa hiyo kazi iliyobaki ilikuwa ya Mavunde kumaliza mgogoro huo, kama ameshindwa yeye mkuu wa wilaya atauweza?

Baada ya hapo waliwasiliana na Mavunde na alisema serikali inaendelea kufuatilia suala la wafanyakazi kufukuzwa kazi, na kwamba walikuwa wakisubiri Wizara ya Madini na Wizara ya Ajira wajadiliane.

Hitimisho

Tumekwenda sehemu mbalimbali kufuatilia suala letu, lakini inavyoonekana ni kama kuna mikono ya hawa wawekezaji kutukwamisha. Nikiwa katibu nilishampigia simu waziri mwenye dhamana na ajira na akaniambia nimpigie baada ya siku mbili. Baada ya hapo amekuwa hapokei tena simu yangu.

Angela Kairuki alipokuwa Waziri wa Madini nilimpigia simu akaniahidi akifika mjini Arusha anatanipigia, lakini hakufanya hivyo.

Hadi anaondolewa katika wizara hiyo hakutusaidia lolote.

Sisi kama wazawa tumeshindwa kuelewa hii Kampuni ya TanzaniteOne ina mkubwa gani anayeogopwa kiasi hiki?

Baada ya kampuni hii kuingia kama wabia wazawa mwaka 2015 walianza kufanya hujuma za wazi wazi. Walikuwa wakivuna madini na kutoa taarifa zikionyesha kuwa hawavuni kitu. TAMICO tukaanza kupiga kelele, hapo ndipo tatizo lilipoanza.

Kwa ufupi, sisi kwa kuwa tumekuwa watetezi wa masilahi ya nchi, ndiyo tumekuwa waathirika kwa kufukuzwa kazi. Kumbe mtu akiwa mzalendo kwa nchi yake haya ndiyo malipo yake?

Ilitumwa tume maalumu ya CAG kufanya uchunguzi. Wakifanya kazi zao na kwa bahati nzuri kamati ile ilipata habari kuwa kuna wafanyakazi wamefukuzwa. Walipouuliza uongozi ukakataa kuwa hakuna watu waliofukuzwa kazi. Wao kwa ujanja wao walinipigia mimi kama katibu na wakaniomba kama tuna vielelezo vinavyoweza kuwasaidia.

Nikawaita wenzangu tukajipanga tukaenda na vielelezo vya kutosha. Tukawaambia wachunguze. Baada ya kufanya vile walinipigia tena wakaniambia kila tulichowapa ni cha kweli.

Miongoni mwa waliyobaini ni wizi wa madini uliokuwa unafanyika kwenye idara ya kuchambua mawe (sort house). Walikuwa wanabadilisha madini mazuri na kuacha yasiyofaa au yenye thamani ndogo sana. Walifuatilia CCTV na kujionea hali ya mambo.

Mwenyekiti wa kamati ile ya CAG tulimwambia kuna barua kutoka serikalini inautaka uongozi wa mgodi ifikapo Machi 6, 2016 wawe wameturudisha kazini, lakini wanaficha. Wakakiri kuyaona maagizo hayo. Hatujarudishwa kazini, nani anayewapa kiburi?

Tunamshukuru Mwenyekiti wa kamati ile, Kilondera. Alifanya kazi yake kwa weledi. Ripoti hiyo ina mengi yanayohusu wizi wa madini mgodini.

Bado tuna mengi ya kuelezea kuhusu wizi wa tanzanite unaoendelea hata wakati huu ambao kuna ukuta. Tutafutwe tueleze wizi unavyofanywa na nini kifanyike ili kukomesha uhujumu uchumi huo.

Mwandishi wa taarifa hii, Richard Nyanginywa, alikuwa Katibu wa TAMICO na ni miongoni mwa wafanyakazi 201 waliofukuzwa. Anapatikana kwa simu namba 0767 465452 au 0684 096361.