Ihsani (hisani) ni neno muhimu sana kwa binadamu akitambua maana na matumizi yake.  Ihsani ni moyo wa kumtendea mtu mema. Hii ni pamoja na kumhifadhi, kumkarimu na kumfanyia mtu jamala.
Unapomtendea mtu hisani, si vyema kumtangaza au kumsimanga mbele ya watu. Unapoitumia hubaki ndani ya moyo wako na huwa ni mapokeo ndani ya moyo wa mtendewa. Ni juu ya mtendewa kuelezea kwa watu au asifanye hivyo na ikabaki kuwa siri yake.
Ni tendo jamala wala halina mizizi kwa mtu mstaarabu asifanye kazi awe mvivu au tegemezi. Hisani anayopewa si mtaji wa kuiba mali, kuhujumu uchumi, kuwa na kiburi wala kujinadi. Hisani hujikita katika uhusiano mwema.
Wenye kutenda hisani kwa watu zama hizi ni wachache mno. Hali hii inatokana na visa mbalimbali vikiwamo vya kutothamini utu, kupuuza masuala ya dini na kupenda kufanya ubazazi na ukatili kwa watu.
Zama zile watu walipendana kama chanda na pete na walichukuana kama mama na mwana kwa sababu walitambua thamani ya utu wa mtu, walimwabudu na mkutii Mwenyezi Mungu kweli kweli na waliona fahari mtu kufarijiwa.
Mioyo ya hisani ilistawi katika mazingira hayo na kuneemesha mayatima, wanyonge, mafukara na wajane katika maisha yao. Ihsani ilipata kete ya kutanda kuanzia kwa watoto, vijana, watu wazima hadi kwa wazee na vikongwe. Jamii ya watu ilishikamana kama viungo vya mwili.
Ubazazi na ukatili ulikuwa ni uvundo kwa watu na kichefuchefu kwa viongozi na watawala wema. Kilio cha ukatili kiliposikika katika kaya, koo, kabila au jamii, haraka ilifanywa kuzima mawimbi ya sauti ya ukatili kusikika.
Sifa mojawapo ya kuwa kiongozi ilikuwa ni ukarimu na kujali watu bila kuangalia nasaba zao, elimu yao, uzuri wao au rangi zao.  Mambo hayo yalikuwa ni mapambo ya mtu mwenyewe.
Ukweli, zama zetu hizi hisani imepotea. Mtu anapojaribu kuirejesha hupata kichapo cha zomeazomea, dharau, kejeli na heshima yake kuvunjwa. Nyimbo za mdhaifu, mpuuzi na hana maana husikika kila mahali.
Katika mazingira kama hayo, mtu mwadilifu na mwenye moyo wa ihsani hubeza kauli na nyimbo zipambazo siasa, utawala na maisha ya watu. Hupiga moyo konde na kujibu, “Natenda mema singoji shukurani” kwa sababu binadamu hawana wema.
Wiki iliyopita huko bungeni, Dodoma, Watanzania tulishangazwa kusikia mayowe na nderemo kutoka kwa wabunge wote wa Bunge la Muungano wakiwa furahani na kutawaliwa na vigelegele na sauti isemayo ‘tumeku-miss’.
Mirindimo hiyo ilimwangukia aliyekuwa Rais wa Serikali ya awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, alipokuwa bungeni kumsindikiza na kushuhudia mke wake, Mama Salima Rashidi KIkwete, akila kiapo cha kuwa mbunge na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuteuliwa kuwa mbunge na Rais John Pombe Magufuli.
Bunge la Muungano kusimamisha shughuli zake za kawaida kwa muda wa takribani dakika tano kupisha chereko, furaha na kumkaribisha Kikwete bungeni, si jambo la masihara hata kidogo. Ni kitendo cha heshima na kujali hisani yake kwao.
Mbegu ya hisani aliyoipanda katika uongozi wake kwa muhimili wa Bunge ilikuwa na thamani kubwa na uhusiano mwema na muhimili wa dola (Serikali) umetuamsha na kutujuza  kwamba ihsani ni jambo jema.
Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, aliwahi kupuuzwa, kukejeliwa, kudharauliwa na kuvunjiwa heshima na vijana ambao hata ubwabwa wa shingo haujawatoka. Lakini yeye aliendelea kutimiza hisani kwa kila kiongozi. Leo wanamkumbuka.
Tumeshuhudia viongozi mbali mbali wanavyomkumbuka, hata waliokuwa mahasimu wake kisiasa wamefurahi. Wamekumbuka kauli yake isemayo “Mtanikumbuka. “ Ni kweli wamemkumbuka, tunamkumbuka. Kumbe hisani ni jambo muhimu.

By Jamhuri