Hofu kutawala nchi ni hatari

Watanzania tumepata kusikia na baadhi yetu wamekumbwa na vitendo vya kubakwa, kutekwa, kujeruhiwa na wengine kuuawa. Tunadhani vitendo hivi viovu vina asili ya uendeshaji maisha au ukinzani wa kisiasa ndani ya nchi yetu.

Ukweli tumeingiwa na hofu, hata kudhania kwamba hatuwezi kupambana na hali hiyo. Hofu ni kushindwa na kuwa na woga. Ni vitisho na hali ya kutokuwa na ushujaa wa kukomesha vitendo vya ukatili. Hofu ni woga, hali ambayo Watanzania hatupaswi kuwa nayo.

Kisiasa hofu ni adui wa maendeleo. Hutia shaka watu kufanya shughuli zao za kujipatia elimu, riziki na kutoa maoni himilivu katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kitamaduni. Nchi inapokuwa katika hali kama hiyo ni hatari kwa wananchi wake.

Masuala ya kubaka, kuteka, kujeruhi na kuua yamekuwa yakifanywa na waovu na kuwaacha Watanzania vinywa wazi na wasijue la kufanya kwa sababu hawaelewi chanzo chake ni nini. Katika mazingira hayo, watu wanajenga hisia, jambo ambalo si jema.

Kuruhusu hisia au udhanifu kubembea ni kudhihirishia ulimwengu kwamba Watanzania si mashujaa! Binafsi, siamini hivyo. Watanzani ni wapevu na mahodari katika masuala ya hekima na busara, ulinzi na usalama wa Taifa lao.

Serikali na vyombo vyake vinaweza kupambana na maovu hayo. Hii ni imani na ukweli uliomo ndani ya mioyo ya Watanzania. Vipi tumudu kumkabili na kumchakaza adui wa Taifa letu kutoka nje ya nchi yetu, tushindwe kujikabili na kujidhibiti wenyewe? Ni mshangao mzito!

Methali ya mganga hajigangi au msemo kinyozi hajinyoi, hapa hauna nafasi kwa sababu waganga na vinyozi (Watanzania) hao ndiyo wanaotaka kuondolewa maovu hayo. Ni vyema tukajipanga kuondoa hali hii kwa vitendo chini ya Serikali yetu sikivu.

Sitaki kuamini eti waganga na vinyozi hao wamo ndani ya vyombo vya Serikali kama baadhi ya waliotekwa na viongozi wanavyoamini na kutuaminisha. Kama hivyo si kweli, basi raha na neema iliyoje Serikali na vyombo vya haki na usalama vikazinduka na kujitetea mbele ya Watanzania?

Ni kweli Serikali huwa na subira. Na mwenye kusubiri yupo na Mwenyezi Mungu na mwenye haraka yupo na shetani. Hata kama Serikali haina dini, wanaounda na kuiendesha Serikali wana dini zao ndani ya Serikali hiyo. Ni busara tukawa na hadhari katika kulikabiri jambo hili.

Subira imekuwako si chini ya miaka kumi tangu vitendo viovu vilipoanza kutekelezwa. Je, kipindi hiki hakitoshi kuwa subira njema? Hali si shwari. Minong’ono, vilio na simanzi zinazidi kuwatia hofu Watanzania na kujihisi kama wanapuuzwa ilhali Serikali ni yao. Vipi wakwazwe? 

Tunapochelea kupambana na maovu haya, tuelewe tunajenga au tunapanda siasa chafu ndani ya siasa safi ya nchi yetu. Tunaweka wazi milango ya maovu na mmomonyoko wa maadili, uadilifu na uwajibikaji wa wananchi, na hasa vijana wajenzi wa Taifa hili. Uzalendo una dalili ya kutoweka.

Nasikitika kusema baadhi ya milango inawekwa wazi na wale wasioitakia mema Tanzania. Angalia lugha za baadhi ya viongozi wetu kwenye vyombo vya uamuzi; Bunge na mikutano. Angalia mambo na maelezo machafu kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii!

Heshima inaondoka na dharau inaingia. Utu unafungiwa na unyama unafunguliwa. Utulivu unadidimizwa na fujo inaibuliwa na kadhalika. Dharau, unyama, fujo ni baadhi ya mambo ndani ya siasa chafu. Watanzania tusiamini mambo machafu ni maendeleo, hapana. Ni laana.

Nakiomba chama tawala (CCM) na Serikali yake kuchukua uamuzi wa makusudi na maarifa waliyonayo kukabiliana na matukio haya machafu. Aidha, nafikiri Serikali itakuwa katika mchakato wa kukabiliana na watenda maovu na kufumbua kitendawili cha wananchi. Amani ni mwavuli wetu.

396 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons