Hongera Magufuli, ila sukari, matrafiki…

Wiki iliyopita nilipata fursa ya kuzungumza na mtu mmoja mzito. Mazungumzo yetu yalikuwa ni kwa maslahi ya Taifa. Tulizungumzia ustawi wa Taifa letu na mwelekeo wa nchi chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.

Mazungumzo yetu yalijaa nia njema, ila kwa sababu tu hakunituma nimtaje gazetini, bora nifikishe ujumbe bila kutaja anwani ya posta alikotokea. Joto la kisiasa linaloendelea nchini, hasa Lugumi, ndilo lililoibua mazungumzo hayo.

 Sitanii, nguzo ya mazungumzo yetu ilijikita katika mambo makuu mawili ya msingi – Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (aliyetumbuliwa), Charles Kitwanga, na mkataba wa Lugumi huku la pili likihusu uhuru wa watu kutoa mawazo – kuzungumza bila kuingiliwa na mamlaka.

Mambo haya tuliyazungumza kwa kina. Utadhani tulijua kuwa jipu la Kitwanga lilikuwa limeiva tayari kukamuliwa. Tulisemezana kuwa bila Rais Magufuli kumtumbua Kitwanga, basi sura ya Serikali yake inaingia shakani.

Ukiacha huyo kigogo, ndani ya wiki iliyopita nilipata simu kadhaa kutoka maeneo mbalimbali na moja ninayoikumbuka mno ni kutoka Kamachumu, Muleba. Huyu alizungumza lugha sawa na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

 Mwananchi huyu alihoji Kitwanga anapata wapi nguvu ya kuendelea kukalia kiti cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa wimbi hili la kashifa ya Lugumi, mtu anayedaiwa kupewa zabuni ya kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole na hakufanya hivyo ila malipo alipokea.

 “Tunasikia taarifa kuwa Kitwanga ni mume mwenza wa Rais Magufuli. Tulimpenda sana Rais Magufuli, ila yapo mambo yameanza kututia shaka juu yake. Yeye amejinadi kuwa ni muwazi na hafumbii macho uozo, sasa tunataka tuone akimtumbua huyu anayejinasibu kuwa ni rafiki yake.

 “Hatutaki kuona Rais Magufuli anakuwa double standard. Kwamba awatumbue wengine marafiki zake wapete tu, hili halikubaliki. Tunataka amtumbue Kitwanga ndipo tutaamini kuwa yuko serious.

 “Nakugambila ndamubona ali mushaji ekyoma kalabinga Kitwanga obuwaziri (nakwambia, nitamuona ni mwanaume chuma akimfukuza Kitwanga uwaziri,” maneno haya aliyasema kabla ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Kitwanga, bila shaka sasa anamuona Rais Magufuli ni chuma.

 Wakati huyu Mtanzania mkulima wa kawaida, kijana mwenye umri wa miaka 30 akitilia shaka utendaji wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kitwanga, kama saa 6 mchana hivi, siku ya Ijumaa nikapata taarifa kuwa Kitwanga ameingia katika Ukumbi wa Bunge Dodoma akiwa amelewa chakari. Moyo wangu ukapiga paaaah!

 Joto lililokuwapo, nikajua kuwa yametimia. Baada ya muda si mrefu, nikaona ujumbe huu kupitia katika mitandao ya kijamii: “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Charles Kitwanga, kuanzia (leo) 20 Mei, 2016.

“Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kufuatia kitendo cha Mheshimiwa Charles Kitwanga kuingia bungeni na kujibu swali linalohusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa amelewa. Gerson Msigwa, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Dar es Salaam, 20 Mei, 2016.”

Nakiri kuwa Rais Magufuli ilikuwa kama vile anatusikia mazungumzo yangu na huyo kigogo. Hakika hakuna mwenye chuki na Kitwanga, ila yaliyomkuta yanapasa kuwa fundisho. Sitaki kuamini kuwa ulevi ndiyo uliomwondoa Kitwanga kwenye nafasi hiyo.

 Upepo ulivyokuwa ukivuma ndani na nje ya ukumbi wa Bunge, nilijua kuwa Kitwanga anasubiri wakati. Hata Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia wapo wanaodhani ilizuka baada ya mauaji ya Kaizari Mkuu wa Austria, Franz Ferdinand Carl Ludwig Joseph Maria, na mkewe Juni 28, 1914, lakini kumbe maandalizi ya vita yalianza mwaka 1750 baada ya mapinduzi ya viwanda. Hiyo ni mada pana naiachia hapo.

Vivyo hivyo, kwa Kitwanga, kupoteza kwake uwaziri kulianza pale kampuni yake ya Infosys ilipopata mkataba wa kufunga hivyo vifaa vya utambuzi wa alama za vidole katika ofisi za polisi kutokana na uhusiano wake wa kibiashara na Kampuni ya Lugumi.

Kwa Kiingereza cha kwetu ungeniuliza ningesema; “Rais Magufuli asindikile atandamile (Rais Magufuli alimsukuma aliyechuchumaa).” Hivi, kwa hali aliyokuwa nayo, Kitwanga alikuwa mtu wa kuongeza kosa jingine kweli? Na hasa ulevi bungeni? Hapa ndipo ninapopata shaka vyombo vya dola kama vinachunguza na kutoa taarifa sahihi za wateule kabla ya kuteuliwa au ‘fitna’ tu ndiyo itawalayo mchujo?

Sitanii, katika hili nampongeza Rais Magufuli. Hakuangalia makunyanzi. Kitwanga kama ametenda dhambi zake, amemtumbua mara moja. Tena Rais Magufuli usiishie kuwarekodi tu hao wanaolalamika kama ulivyotwambia karibuni, watumbue tu.

 Rais Magufuli, naamini kwenye Baraza la Mawaziri unaendesha vikao kwa uwazi. Sitarajii Waziri ashindwe kusema linalomkera kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri halafu aanze kulalamika mitaani. Kama una waziri wa hivyo, huyo ni mnafiki hakufai. Muungwana yeyote husema bayana asilolipenda bila kupepesa macho.

 Nasikia mawaziri na watendaji wengi wanakuogopa, hilo nasema si sahihi. Wakuheshimu, wasikuogope. Mawaziri wako lazima wajifunze kusema NO, katika jambo lisilowezekana. kama Rais atawaambia kila jambo mkaishia kusema NDIYO MHESHIMIWA, tena wengine mtakwenda mbali na kusema NDIYO MTUKUFU, mtaishia kumpotosha Rais.

 Sitanii, mawaziri na watendaji serikalini jengeni moyo wa kujiamini. Jengeni utamaduni wa kumwambia Rais Magufuli hata mnayoamini hataki kuyasikia. Jengeni utamaduni wa kwenda mbele ya Rais kujenga hoja, kueleza malengo na mipango inayotekelezeka ndani ya muda maalumu, na si kuomba kupokea maelekezo.

 Hoja hii inanileta kwenye suala la pili tulilozungumza na kigogo. Uhuru wa watu kutoa mawazo (freedom of expression). Mazungumzo yetu yalikwenda mbali zaidi na kuangalia nchi za Scandinavia zilivyoendelea kwa kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari, na hatimaye huru wa kutoa mawazo.

 Suala kama matangazo ya Bunge kurushwa ‘live’ au la, wala haikupaswa kuwa ajenda. Mawaziri, Mwansheria Mkuu na wengine wenye fursa wangesimama wakamwambia Rais (kama ndiye aliyezuia), kuwa Mheshimiwa Rais dhana ya kuzuia matangazo ya Bunge ‘live’, inapingana na utendaji wako.

 Kwamba wewe unapenda kutumbua majipu hadharani, hivyo kuficha yanayoendelea katika ukumbi wa Bunge si fursa ya kulisaidia Taifa hili. Kwamba kinachotokea bungeni ni kukiri kuwa kiti cha Spika kimeyumba kwa kiwango ambacho hakiwezi kuwasimamia wabunge.

 Ikiwa Bunge lina kanuni na kanuni zinafanya kazi, kinachopaswa kuwapo hapa ni kuweka wazi kanuni za uendeshaji wa Bunge. Kama mbunge anatukana, basi bila kusubiri anatumbuliwa. Si kazi ya mbunge kuingia bungeni kuvurumisha matusi. Anayetukana inabidi aadhibiwe mara moja.

 Mheshimiwa Rais, hili nimeliandika mara nyingi kiasi na usinichoke, nitaendelea kuliandika, kwamba kuzuia matangazo ya Bunge ‘live’ kama ni mkakati wa wasaidizi wako, basi hili ni shimo unalochimbiwa.

Ni bora ushauriane na Spika mrekebishe kanuni za Bunge ziwabane wavurumisha matusi, lakini bila kufanya hivyo unawapa wapinzani wako ajenda za kusema. Na wala usidhani Lema aliyesema ameanza kum-miss Rais Jakaya Kikwete yuko peke yake, hata wabunge wengi wa CCM nikizungumza nao lugha yao ni hiyo hiyo.

 Sasa Rais Magufuli naomba kukuongezea jambo. Mimi nilishajitolea kusema ukweli na naamini kwa kusema ukweli ndiyo maana umetupongeza hadharani sisi wa gazeti la JAMHURI. Nakuomba uwachunguze hata wazalishaji wa sukari. Inawezekana takwimu walizokupatia si za kweli. Sukari ni janga katika nchi hii kwa sasa.

 Sitanii, tena si sukari tu, bali hata mafuta ya kula wakati ulipoingia madarakani ndoo ikiuzwa Sh 24,000 kwa sasa inauzwa 35,000. Bidhaa pekee ambayo nayo uishukuru Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ni mafuta.

 Shule binafsi wameongeza ada, TBL wameongeza bei ya hiyo bidhaa iliyokufanya utengue uteuzi wa Kitwanga, kitimoto imepanda bei kutoka 10,000 hadi 12,000 kwa kilo iliyokaangwa safi (niwie radhi wale wa imani nyingine), nyama kwenye bucha ni Sh 8,000 kutoka wastani wa Sh 5,000 kwa Dar es Salaam na mengine mengi. Maisha yanazidi kuwa magumu.

Sitanii, ni kwa unyenyekevu na upendo mkubwa nayafikisha haya kwako. Kasi uliyoanza nayo kazi, nakusihi uiongezee nguvu kwa kugatua (devolve) madaraka. Rais, jenga mfumo kwa kurekebisha Sheria Na 8 ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake urejeshe angalau unyapara katika sehemu za kazi.

Haiwezekani leo wewe ukitoka ziara ya kushtukiza Muhimbili, Airport, Bandari, Wizara ya Fedha na kwingine kila kitu kisimame hadi utakaposhtukiza tena. Sasa uingie mikataba na mawaziri, nao waingie na makatibu wakuu, nao waingie na makamishna, wakurugenzi na kuendelea kudai matokeo ya kazi.

Mwisho, si kwa umuhimu, bali nikudokeze tu kuwa kikosi cha usalama barabarani kinafanya kazi ya kukuhujumu. Matrafiki sasa wanabambikia watu kesi usipime. Wanajificha vichakani na kamera na kusingizia watu mwendo kasi waweze kupata fedha.

Tangu umeagiza huyo trafiki apandishwe cheo aliyeambiwa na mke wa Waziri mwenye dhamana na Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, kuwa anaweza kutoa onyo yeye akasema ametukanwa, kwa sasa wanasema hatuna pa kwenda. Wanazo mashine za kukusanya mapato, ikikupendeza TRA uwapeleke likizo kazi hii waifanye matrafiki.

Sitanii, Mheshimiwa Rais, hili linakujengea chuki usipime. Tuma watu wako unaowaamini wakueleze uonevu na manyanyaso wanayofanyiwa madereva kutokana na kauli yako. Nasema, madereva wasivunje sheria wala kutukana matrafiki, lakini pia ni dhambi kubwa mbele ya Mungu matrafiki kubambikia madereva kesi.

Kasi ya matrafiki kubambikia madereva kesi ikiendelea hivi, muda si mrefu tarajia maandamano ya wanyonge. Kamanda Mohamed Mpinga namsihi atume watu wake aone vioja. Wanachofanya sasa matrafiki ni kutimiza hesabu, bila kujali una kosa au la. Hii haina afya kwa ustawi wa jamii. Rais Magufuli litupie macho hili, bila kusahau sukari na mafuta ya kula. Mungu ibariki Tanzania.