Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imetimiza miaka mitatu tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015.

Rais Magufuli alishika uongozi nchi ikiwa inakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi, kijamii na kimaadili. Hatuna kipimo sahihi cha kubainisha kazi zilizokwisha kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa miaka hii mitatu, lakini itoshe tu kusema yapo mambo mengi; makubwa, mazuri na ya kupigiwa mfano yaliyofanywa.

Kwa namna ya pekee tunampongeza Rais Magufuli na safu nzima ya uongozi wa taifa letu kwa kutufikisha hapa tulipo. Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake na hata yeye mwenyewe, taifa letu limeendelea kukabiliwa na changamoto nyingi.

Maadui Ujinga, Maradhi na Umaskini waliotangazwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, karibu miaka 60 iliyopita bado wapo; na kwa kweli unatakiwa umoja na mshikamano wa hali ya juu miongoni mwa Watanzania ili kuendelea kuwakabili na hatimaye kuwashinda.

Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusimama imara katika vita dhidi ya rushwa, ufisadi; na kurejesha imani ya wananchi, hasa wanyonge kwa serikali yao. Miaka kadhaa iliyopita nchi hii ilishikwa na wenye ukwasi na madaraka makubwa. Wanyonge walitaabika. Dhuluma bado ipo, lakini dalili za kuikabili zinaonekana.

Uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma yalikuwa mambo ya kufikirika, lakini leo walau tunaona nidhamu na uwajibikaji.

Tunampongeza Rais Magufuli kwa kusimama kidete kuhakikisha tunakuwa na miradi mikubwa kama ya umeme, reli, barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini, hospitali, shule, vyuo na kadhalika. Hii ni dalili nzuri ya huko tuendako.

Ni ukweli ulio wazi kuwa Rais Magufuli na safu yake ya uongozi – wao pekee hawawezi kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Ni kwa kulitambua hilo, tunatoa mwito kwa wananchi, kila mmoja kwenye nafasi yake kuwajibika ipasavyo. Malalamiko pekee hayawezi kuyabadili maisha yetu na ya kizazi kijacho.

Tunapaswa kufanya kazi kwa kulenga kukikomboa kizazi kijacho badala ya kujitafutia faraja sisi tunaoishi sasa.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli, tunamuomba asikilize baadhi ya matamanio ya Watanzania, likiwamo suala la Katiba. Haya mazuri anayofanya sasa yanaweza yasidumu kama hayatalindwa kikatiba. Katiba nzuri inayotakiwa na watu wengi ni uzio imara wa kuyaenzi mema yote yanayofanywa na viongozi wetu wakuu.

Pia ahakikishe heshima ya Tanzania mbele ya mataifa mengine haiteteleki. Tuhakikishe Tanzania inakuwa mahali salama kwa wenyeji na wageni, tuhakikishe watu wanakuwa na uhuru wa kukosoa na kushauri kwa staha, pia tuhakikishe tunaondoa aina zote za dhuluma na uonevu katika nchi yetu. Matukio ya kutekwa na kuuawa kwa Watanzania hayana budi kufikia mwisho sasa.

Kwa dhati kabisa tunampongeza Rais Magufuli na wasaidizi wake wote. Tunawaahidi ushirikiano katika kuhakikisha tunaijenga Tanzania njema ya sasa na ijayo.

Mungu Ibariki Tanzania.

By Jamhuri