Mkuu wa Mkoa (RC) wa Simiyu, Anthony Mtaka, ametoa msimamo wa namna alivyodhamiria kuubadilisha mkoa huo ili uendane na ‘Tanzania ya Viwanda.’

Kabla na baada ya kusifiwa na Rais John Magufuli, aliyemtaja kama RC bora nchini, Mtaka ameendelea kuonyesha maono makubwa ya uongozi. Amezidi kuibua miongozo mbalimbali ya kiuongozi ambayo kwa kweli imekuwa nadra kuipata kutoka kwa viongozi wengi nchini.

Amekuwa mbunifu wa mambo mbalimbali ya kimaendeleo kiasi cha kuuweka Mkoa wa Simiyu kwenye orodha ya mikoa yenye uongozi bora unaolenga kubadilisha maisha ya watu na vitu kwa vitendo.

Kwa namna ya pekee tunapenda kumpongeza kwa uamuzi wake wa kuhakikisha Jeshi la Polisi haliwi kikwazo cha biashara na ukuzaji wa uchumi mkoani Simiyu, bali linakuwa kichocheo cha mambo hayo.

Amefafanua kwa ufasaha na kwa lugha nyepesi namna biashara zinavyopaswa kuendeshwa, akipinga utaratibu wa polisi kuamuru baa na sehemu nyingine za huduma za kijamii kufungwa mapema.

Ameelekeza namna shule za sekondari na vyuo vinavyopaswa kutumia fursa ya kuwa na umeme katika maeneo yao kwa kuwaruhusu wanafunzi wajisomee kwa muda mrefu usiku badala ya kuwalazimisha kulala mapema.

RC Mtaka ameeleza pia faida za kuwa na taa za mitaani mjini Bariadi, na hivi punde Ramadi, akisema hazipaswi kuwa mapambano, bali zitumike kuangaza ili wafanyabiashara waendelee na kazi zao nyakati zote za usiku kadiri wanavyoweza.

Tunachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati RC Mtaka, tukiamini kuwa maono na miongozo anayoitoa mkoani mwake ni chachu kubwa ya maendeleo.

Wakati tukiwa kwenye harakati za kuhakikisha tunakuwa na ‘Tanzania ya Viwanda’, hakutakuwa na maana kama watu watapangiwa muda wa kulala au kufanya biashara. Nchi jirani ambako hakuna amani kama kwetu, biashara zinafanywa muda wote – saa 24, siku zote saba za wiki. Kama wao wameweza, kwanini ishindikane kwetu?

Tunampongeza RC Mtaka kwa sababu ni kiongozi anayeamini kila jambo jema linawezekana, muhimu ni kuwashirikisha viongozi wengine na wadau wakuu ambao ni wananchi.

Jeshi la Polisi, kama alivyosema, wajibu wake ni kulinda biashara zisifungwe badala ya kuwa lenyewe ndilo linalolazimisha watu kufunga biashara kwa kigezo cha usalama.

Tunampongeza RC Mtaka tukiamini wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa mingine wataiga mfano wake ili kuhakikisha Tanzania yote inakuwa ‘macho’ kibiashara muda wote wa saa 24. Pia tunawahimiza wananchi na viongozi wote wa Simiyu kumuunga mkono ili kuufanya mkoa huo kuwa wa kupigiwa mfano. Hatua hii ni muhimu sana katika kuelekea Tanzania mpya. Hongera sana RC Mtaka.

1164 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!