Hotuba tata ya Nape kutoka Mtama

Ndugu Rais, Mbunge wa Mtama, Ndugu Nape Moses Nnauye amepata mapokezi makubwa jimboni mwake. Alienda kwa wapiga kura wake baada ya kuenguliwa kwenye uwaziri. Tunaambiwa mapokezi yale hutolewa kwa shujaa aliyerudi na ushindi. Ni ushindi gani Nape alirudi nao Mtama haujulikani! Kama uwaziri alikuwa amekwisha upoteza.

 Nape alijisahau akafikia hata kuwapanda migongoni mama zake walewale waliombeba kwa miezi tisa tumboni na kisha kwa miaka kadhaa akakulia migongoni mwao wakimvumilia kwa kila jambo! Hakika hii kama ilikuwa ni heshima, ilikuwa ni heshima kubwa mno mahsusi kwa aliyefanya jambo kubwa mno! Ni jambo lipi kubwa mno alilowafanyia wana Mtama kwa ubunge ambao haujafikia hata miaka miwili?

Wakati wa Uchaguzi Mkuu, Edward Lowassa kila alikokuwa akienda, mapokezi yake yalikuwa ni mafuriko! Nape alisema mafuriko yale alikuwa anayatengeneza Lowassa mwenyewe kwa kuwanunua watu. Leo nao wakisema mapokezi ya Nape kule Mtama aliyatengeneza Nape mwenyewe kwa kuwanunua watu watakuwa wamekosea wapi? Nilivyomjua marehemu mama yangu asingekubali kudhalilishwa kiasi kile! Mtu wa hivi hivi tu ampande mgongoni eti anapita! Wanaume wa Mtama hawana migongo?

Ndugu Rais, tunaambiwa alilia mbele ya wale wanawake. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu wote walionisaidia kuiona nchi ya ahadi, Israel, iwe ni kwa sala zao au kwa mali zao! Wabarikiwe na wadumu katika amani Yake!

Tulipokuwa Jerusalem tulifanya ibada ya njia ya Msalaba tukiifuata njia ile ile aliyopita Bwana Yesu akiwa amebeba msalaba wake, kituo kwa kituo mpaka Golgota alipotundikwa msalabani! Tulifika katika kituo ambako Bwana Yesu aliwakuta akina mama waliokuwa wanamlilia!

Aliwaambia, “Msinililie mimi! Jililieni nyinyi na watoto wenu!” Katika kutafakari nikajiuliza, kule Mtama Nape alikuwa analilia nini? Uwaziri wake!

Ndugu Rais asiye bahati, habahatishi! Alitakiwa ndiye awatoe machozi wale mama kwa kuwajulisha jinsi maisha ya watoto wao na waume zao yalivyo shakani! Wananchi wanatekwa nyara na kuumizwa vibaya huku wakiwa wameshikiwa silaha za moto mahali ambako hakuna dalili zozote za uhalifu? Angewauliza, kwa kuwa Serikali haichukui hatua zozote, imekuwa kimya kama vile imeridhia ni mtoto wa nani au mume wa nani angebaki salama kesho yake? Kwa kihoro cha mama zetu wangetokwa na machozi! Ndipo Nape angewaambia, “Msinililie mimi, mlilieni Rais wenu ili awaepushie nchi yenu na nyinyi wenyewe, msije mkajikuta sawa na wale wanaoongozwa na wana wa kizazi cha nyoka!”

Badala yake, ilishangaza kumwona Nape akishikwa na uchungu wa ghafla kwa kutekwa nyara Ben Saanane kama vile habari zile alizisikia kwa mara ya kwanza alipofika Mtama. Mtenda husahau haraka. Anatafuta huruma hata kwa wale aliowaumiza sana!

Aliposema matendo ya utekaji nyara wananchi yasipotatuliwa yatakipa shida sana Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alikuwa haongelei amani ya nchi! Alikuwa haongelei hali duni ya maisha ya wananchi wa Mtama na Watanzania kwa ujumla, bali ushindi wa CCM utakaomwezesha kuendelea kuifaidi nchi! Na kwa kuwa kutekwa nyara akina Ben Saanane, Roma Mkatoliki na wengine kunamjengea chuki Rais Dk. John Magufuli dhidi ya wananchi, hivyo ni muhimu kwa maoni yake akasimama mtu mwingine mbadala mwaka 2020. Kama Nape alienda msituni, alienda kwa njaa zake mwenyewe! Anaposema, “Kifua changu kina mengi sana, siwezi kuyasema, lakini lazima mkumbuke kuwa Rais Magufuli nimemtafutia kura mimi mwenyewe!” Huko ndiyo kutapatapa, maneno ya mkosaji.

Ndugu Rais ni kweli hali ya usalama nchini inasikitisha! Majuzi nilipokuwa natoka nilimwomba binti yangu aniombee. Badala ya kuniombea akaniambia, “Baba nenda tu, lakini kuwa mwangalifu. Usisimame karibu na gari aina ya Noah nyeusi!” Nyerere alituachia nchi ya upendo na amani tukiishi kama watoto wa baba mmoja; hawa viongozi wetu wanataka kuwaachia watoto wetu nchi ya visasi! Wabunge badala ya kuungana kuiwajibisha Serikali, wameng’ang’ania upuuzi wa u-vyama vyao! Matokeo yake wananchi wanalalamika na wenyewe wanaishia kulalamika! Bila aibu mbunge anasema, “Nai-miss sana Dar es Salaam, lakini mkuu wa mkoa huo amesema nikienda tu ataniteka nyara!” Huyu ni mbunge masikini!

Ndugu Rais ikasikika sauti kutoka ndani ya Bunge kuwa, “Habari za kutekwa Ben Saanane hazina ukweli kwa sababu hakuna ushahidi wowote!”

Huyu ndugu angekuwa hakusoma shule kabisa angeonekana ni mhuni tu wa kawaida kama walivyo wahuni wenzake. Angesoma japo kidogo angeonekana ni  mjinga watu wakamdharau. Bahati hana uelewa wa sheria!

Angeonekana ni mpumbavu kwa sababu anatafuta ushahidi wa kumwezesha kujua kuwa mama aliyemzaa, alikuwa mwanamke!

Ndugu Rais, Nape kukutajia Lowassa katika hotuba yake ya Mtama, alikuwa anakutishia nyau! Anakwambia, “Kama mimi na Lowassa tunakunywa chai pamoja sasa, nyie mnanuniana nini? Sisi sasa ni kitu kimoja” Nape ana moyo mpana kama ule aliousema Baba wa Taifa! Ni udhalilishaji upi ambao Nape hakumfanyia Lowassa? Edward alinyamaza muda wote! Makuzi ya vijana wa kizazi cha ‘dot.com’ hawajui kumwangukia mzee waliyemkosea kumwomba msamaha!

Akidhani ni sifa, akataka ujue kuwa ni yeye ndiye aliweka ‘mguu’(kumzuia) Edward Lowassa asipate ridhaa ya CCM kuwania urais.

 

Anasema Lowassa alikuwa na nguvu sana ndani ya chama. Yaani kama alimweza Lowassa atamshindwa nani? Baba ujumbe huo unatumwa, unafika?

Nape soma kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa msiba wa kujitakia hauna kilio! Ulikuwa unashika mapindi ya nyoka kwa hiari yako wenyewe hivyo kuumwa na nyoka si muhali! Unachotakiwa sasa ni kukiri kuwa ulifanya kosa kuufunga mlango ambao sasa hauwezi kuufungua!

Ndugu Rais, Nape anaposema Tanzania itakuwa salama kama vijana watasimama kuusemea ukweli ni kauli hatarishi! Nape, aliulizwa Bwana Yesu, ukweli ni kitu gani? Vijana wasimame wampiganie nani? Baba na Nape wote mrudieni Muumba wenu kwa ajili ya amani ya nchi hii na kwa ajili ya ustawi wa waja wake. Adhabu zake Mungu za sasa ni hapa hapa duniani! Henche anasema Maandiko Matakatifu katika Methali 12:15 yanasema, “Mtu mpumbavu njia yake imenyooka machoni kwake mwenyewe tu, bali mwenye hekima husikiliza ushauri” Tusiukubali upumbavu!

573 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons