Hotuba hii ya Rais John Magufuli, aliitoa Aprili 6, 2018 wakati wa uzinduzi wa ukuta wa machimbo ya tanzanite Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara. Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli, alimzawadia mgunduzi wa madini hayo, Mzee Jumanne Ngoma, Sh milioni 100. ENDELEA…

 

Kwanza kabisa ndugu zangu wananchi na Watanzania mlioko hapa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kama walivyotangulia viongozi wetu wa dini kumshukuru kwa kutuwezesha sisi wote kwa pamoja tuione siku hii ya leo ambayo ni siku muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu.

Napenda kwa namna ya pekee kuwashukuru sana mawaziri wa ulinzi na mawaziri wa wizara ya madini kwa kunikaribisha mimi nije nishiriki nanyi katika hafla hii muhimu sana ya kuufungua ukuta huu wenye urefu wa kilometa 24.5 ambao ulitakiwa ukamilike kwa miezi sita -umekamilika kwa miezi mitatu kwa sababu ya juhudi za Jeshi letu la Wananchi.

Napenda nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee nilipongeze sana Jeshi la Wananchi. Jenerali Mabeyo nakupongeza nataka nikueleze hiki kilikuwa kipimo chako. Na umekishinda. Nasema kwa dhati umekishinda. Kwa sababu hakuna mtu aliyetegemea kwamba ukuta wa kilometa 24.5 unaweza ukajengwa kwa kipindi cha miezi mitatu.

Tungeweka kandarasi hapa angekaa miaka 15 na angeomba variation. Na tungeweka kandarasi nondo zingeibiwa, misumari ingeibiwa, simenti ingeibiwa, hata mchanga wangeiba. Na ndiyo maana nasema kwa dhati kutoka moyoni na Mungu alilinde sana Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na JKT.

Na ndiyo maana maombi yaliyokuwa yanapeperushwa hapa, kwa mtu wa kawaida unayemheshimu Mungu unashindwa kukataa. Na ndio maana nimeanza na kushukuru sana, tunaambiwa tushukuru kwa kila jambo.

Mmeonyesha uwezo wa majeshi yetu, Jeshi letu hilo hilo ndilo lililomtoa nduli Amin, Jeshi ndilo lililoshiriki kwenye ukombozi wa nchi nyingine ambazo zilikuwa bado zinatawaliwa na wimbi la kibeberu. Jeshi hilo hilo lililokuwepo… ninaweza kuliona kwamba lipo katika mwaka 2018. Hongereni sana Jeshi. Mimi kama kamanda wenu ninajisikia raha sana. Ninajisikia raha kuwa Tanzania, ninajisikia raha kuwa Tanzania kwa sababu hata haya maneno mliyoyazungumza kwamba mtaendelea kuilinda Katiba na amani ya Watanzania ni maneno ambayo yana busara ya pekee, hongereni sana majeshi yetu.

Lakini pia napenda nizishukuru wizara, Wizara ya Madini- Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Kamishina na watendaji wote. Na nashukuru wizara yote kwa ujumla ya Ulinzi ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mwinyi, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Majemedari wote, Ma-Meja Jenerali, ma-Breigedia Jenerali mpaka huku chini, kwa jinsi mlivyolisimamia hili na kuweza kulifikisha hapa. Ninawapongeza wote kwa ujumla.

Mmenieleza kwamba palikuwa na maofisa 34 na maaskari wengine 287, na ma-servicemen and women- au ni girl -zaidi ya 2000 na kitu. Nataka nikuahidi Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na CDF, nitatoa barua yangu ya kuwapongeza hawa maofisa wa Jeshi la Wananchi 34 pamoja na 287 walioshiriki katika ujenzi huu na ninaposema kupongeza tutaangalia utaratibu wa kupongezana wa aina tofauti tofauti (makofi).

Nilikuwa namsikiliza aliyekuwa akitoa maelezo Kanali Charles sijui nani, alikuwa anaeleza unajua kabisa kuwa huyu field hii anaifahamu na alikuwa anazungumza with confidence. Na nilipokuwa nawaona hata wale wengine waliokuwa wamekaa pembeni nao wako hivyo hivyo. Kwa hiyo ninawapongeza sana.

Lakini kwa hawa vijana wangu, Operesheni Jakaya Mrisho Kikwete na Operesheni John Pombe Magufuli… CDF alipokuwa akizungumza hapa nilikuwa ninawaona kweli wakuu wa vyombo wakitabasamu. Hii inadhihirisha wazi kwamba ninyi mmejiuza wenyewe (makofi).

Nitahakikisha wale watakaofiti vizuri, na ninavyoona wote mnafiti vizuri, basi CDF, IGP, na maeneo mengine ambayo tutaweza kuwachukua muweze kuchukuliwa kwa wale watakaotaka kutumikia katika majeshi yetu, kuanzia Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi na kadhalika (makofi). Kwa sababu sina cha kuwalipa. Kuwalipa kwangu mimi ni ninyi kupata ajira (makofi).

Napenda pia kwa namna ya pekee niwashukuru sana wananchi wa Simanjiro. Wananchi wa Simanjiro wameshirikiana vizuri. Walikuja pale wakanieleza shida zao na mimi nikawaeleza kwa kweli hapa hapakutakiwa pawe hivi. Mahali ambapo tunachimba madini pekee katika dunia wananchi wa Simajiro hawana maji, wananchi wa Simajiro hawana hospitali nzuri, wananchi wa Simanjiro hawana hata gari la wagonjwa – siku ile niliambiwa.

Nataka niwaambie wananchi wa Simanjiro, gari la wagonjwa nimekuja nalo leo hapa nitawakabidhi. Nitamuita mkurugenzi wenu ili kusudi lisiwe linakosa mafuta, nitamkabidhi leo hapa libaki hapa hapa kwa ajili ya huduma za hapa. Simanjiro oyeee.

Lakini ndugu zangu ni ukweli usiopingika kwamba madini yetu yameibiwa sana. Yameibiwa na tumeibiwa kweli kweli. Ninaambiwa tangu madini haya yavumbuliwe na Mzee Jumanne Ngoma kwenye mwaka 67, mzee yule pamoja na kutambuliwa na Mheshimiwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye barua niliyoiona imesainiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ya tarehe 3/8/1980. Na document yake ya kwamba amevumbua madini ya aina ya pekee ambayo hata yeye alikuwa hayajui na akayapeleka kwa jiolojia mkuu wa nchi mwaka 67, barua ya m-jiolojia hiyo nimeiona.

Na bahati nzuri ninayo, hebu leta document zangu hapa. Hii inadhihirisha kwamba tanzanite haikuvumbuliwa na mtu kutoka nje. Imevumbuliwa na Mtanzania.

Barua ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliisani tarehe 8/10/80 akitambua kazi nzuri za mzee huyu ambaye ninaambiwa kwa sasa hivi ame- paralyze kidogo. Lakini barua ya Inspector of Mines, Officer Incharge aliisaini tarehe 23, Septemba 1967. Lakini alishapewa hati ya kupewa tuzo ya sayansi ya ufundi mwaka 84 na kadhalika. Huyu mzee amekuwa akihangaika siku nyingi. Tangu 67 anahangaika, na ndiyo tatizo la Tanzania. Ukifanya chochote hata kama ni kizuri namna gani, hata ungevumbua nini. Mimi nawafahamu wavumbuzi wengi tu chuo kikuu waliofanya makubwa tu, lakini hata kutambuliwa hawakutambuliwa. Hata mimi nilivumbua kitu fulani cha Anacardic Acid nilipoomba hata kutambuliwa tu mpaka leo wala hata kuandikiwa tu barua. Wamebaki na kitabu changu kwenye library ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa hiyo nilipomuona huyu mzee anahangaika ninajua matatizo ya Watanzania. Na ndiyo maana wavumbuzi wengi wa Tanzania saa zingine huwa wanaishia, yale waliyoyavumbua anakwenda anapewa pick-up na mzungu yanaisha huko huko naye anatakuwa anatembelea hata kubebea mchicha.

Huyu mzee sifahamu kama yuko hapa, niliagiza aje hapa. Aje tu hapa nimtambulishe huyo mzee. Kama ataweza, angalau wakuone Watanzania historia ibaki kuwa Tanzania kwamba wewe ndiyo mgunduzi wa tanzanite. Kama anaweza kuja mumsogeze, kama ikishindikana basi muache. Angalau mumlete akae hapa mbele. Leo ni siku ya tanzanite angalau mumlete huyu mzee akae hapa mbele.

Bila yeye tusingekuwa tunasherekea. Mumlete kabisa hapa. Mlete hapa Mzee Jumanne sogea hapa uje ukae hapa. Tunafanya haya kwa heshima yako na upendo wako mkubwa. Mlete hapa huyu baba aje akae hapa.

Nimeona nimlete huyu mzee ili Watanzania wamtambue, kwamba leo tusingekuwa tunazungumza tanzanite bila huyu baba, anaitwa Jumanne Ngoma. Sasa mnamuona mzee wa watu leo anaumwa mguu wake ameshapalalaizi. Ili kusudi aende akatibiwe vizuri, Serikali yangu tutampa shilingi milioni 100 (makofi) ili akazitumie katika matibabu yake na kuweza kujisitiri sitiri, yale mengine tumuachie Mungu tutajua namna ya kufanya.

Hiyo hela hatumpi sasa hivi hapa, tutaiweka kwenye akaunti yake atazungumza, wasaidizi wangu watazungumza atoe akaunti ikiwezekana kuanzia kesho, keshokutwa ziingie shilingi milioni 100 zimsaidie huyu shujaa wa Watanzania. Mzee Ngoma oyeee…

Leo sisi wote hapa tusingekuwepo asingekuwa huyu mzee. Aliamua kuyaokota hayo akayapata, akaamua kwenda kuyashughulikia. Na katika ripoti ya mjiolojia alipeleka sample tatu – wala hawakujua kama yanaitwa ni tanzanite. Kwa sababu hapa wanasema; almost unusually veniality it is softer than most gemstones. Hardness ni 6 hadi 6.5, but their outstanding quality suggest that the market could be found.

Na akaambiwa pia katika sample nyingine ya pili; similar to K4A but poorly quality nyingine akasema is also probability the all side but the identification not yet felted. They are unusually stones especially the sample K6 and it is likely that the market could be found. Mwaka 67, tarehe 23 Septemba.

Wito wangu kwa Watanzania, tuwathamini watu wanaofanya mazuri kwa ajili ya nchi. Kwa hiyo mzee hakutakiwa kuwa hivi, wapo watu wanaotajirika kwa sababu ya Mungu alimuonyesha kwenda kuvumbua haya.

Wapo watu wamekuwa mabilionea, tena wengine siyo Watanzania kwa sababu tanzanite imekuwa ikisombwa kwenda nje ya nchi. Huyu ambaye alipewa tunu hii kwa kudra za Mwenyezi Mungu amebaki hivyo hivyo. Mungu atusaidie zile mionyo za fitna ziwe zinaondoka ili tutambue wazee kama Mzee Ngoma. Kwa hiyo niliona nilizungumze hili kwa sababu leo tuko kwenye issue ya tanzanite lakini na yeye awepo.

Mimi nimezipata habari kwa kuandikiwa meseji. Baadaye nikamsikia sijui ndugu yake, mtoto wake Hassan Ngoma naye alikuwa anazungumza hivyo. Nikaona huyu ana maneno mengi mengi itakuwa nanii hivi, lakini kumbe baada ya kuchunguza tumekuta ni kweli.

Kwa hiyo niwashukuru sana aliyeniandikia meseji na waliokuwa wakiandika meseji nyingi kuhusu huyu mzee. Nafikiri huu ni mwanzo mzuri wa kuwakumbuka mashujaa wetu waliotengeneza jina la Tanzania kupitia tanzanite kwa kazi nzuri wanazozifanya.

1277 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!