Hukumu ya kesi ya rufani namba 285/2012 iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa Mkoa wa Mwanza, imemliza Bibi Kizee, Moshi Juma  Nzungu (67), kwa hofu ya kunyang’anywa nyumba anayoishi tangu miaka ya 1957 katika eneo la Pasiansi, jijini Mwanza.

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 25, mwaka huu na jopo la majaji watatu ambao ni E.M.K. Rutakangwa, K.K. Oriyo na S.S. Kaijage na kuthibitishwa na Kaimu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufaa, P.W. Bampikya.

Kesi hiyo ilikuwa inatetewa na Jamhuri (Serikali) ikiongozwa na shahidi namba moja, Moshi Juma Nzungu dhidi ya mlalamikiwa, Shida Manyama anayefahamika pia kwa jina la Seleman Mabuba katika kesi hiyo.

Mei 24, 2012 Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza chini ya Hakimu Mkazi, Mwambapa, ilimtia hatiani Seleman Mabuba katika kesi ya jinai namba 81/2012 kwa kughushi nyaraka za kujipatia  kiwanja  kwa njia  ya udanganyifu na ikamhukumu kutumikia kifungo cha miaka sita kwa kila kosa gerezani.

Katika kesi hiyo Seleman Mabuba anadai ndiye mmliki halali wa kiwanja namba 410 Block L yalipo makazi ya mlalamikaji, Moshi Juma Nzungu kwa miaka 56.

Hata hivyo, hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufaa Mkoa wa Mwanza imemwachia huru mlalamikiwa huyo ambaye inaelezwa tayari amemwandikia bibi kizee huyo barua ya kumdai fidia ya Sh milioni 200.

Hukumu hiyo imekuja miezi tisa baada ya baadhi ya watumishi 11 wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuvamia na kuvunja bafu katika makazi ya bibi kizee huyo. Bibi kizee huyo alitoa taarifa za tukio hilo katika kituo cha polisi, ingawa hadi sasa watuhumiwa hawajafikishwa mahakamani.

Gazeti hili lilishuhudia sehemu ya chumba cha bafu ikiwa imebomolewa hali inayomlazimu bibi kizee huyo na familia yake kuonekana wasumbufu wa kuomba sehemu ya kuogea kwa majirani.

Julai 15, 2010 mlalamikiwa huyo katika kesi hiyo alikubali kwa maandishi mbele ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Pasiansi Mashariki ‘B’, Idd Halfani, kurudisha ofa ya kiwanja anapoishi bibi kizee huyo akikiri kuwa ilitolewa kimakosa.

Kwa upande mwingine, mlalamikiwa huyo amesema kwamba nakala halisi ya maelezo ya ofa hiyo ilipotea, huku akiwa ameambatanisha vielelezo vya ripoti na nakala hiyo.

Julai 16, 2010 mwenyekiti huyo wa mtaa alimwandikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza barua kupitia kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Pasiansi, Simon A.M. kumjulisha maelezo hayo ya mlalamikiwa huyo.

 

Mbali ya Idd Halfani, mashahidi wengine wa maelezo hayo ya mlalamikiwa huyo walioweka saini zao katika nakala husika ni Justin Timotheo, Haji Omari, Athumani Faraji na Kahama Edward.

 

Akizungumza na JAMHURI nyumbani kwake wiki iliyopita, bibi kizee huyo amesema hukumu ya mahakama ya rufaa imemweka katika hatari ya kunyang’anywa kiwanja na nyumba yake aliyopangisha watu kwa ajili ya kujipatia fedha za kujikimu na familia yake.


“Sasa mimi nitakuwa mgeni wa nani na uzee huu jamani… serikali nisaidieni jamani, nitakuwa mgeni wa nani?,” amesema bibi kizee huyo huku akitokwa machozi.

Bibi kizee huyo alisema kwamba hana uwezo wa kulipa kiasi cha Sh milioni 200 anazodaiwa na mlaalamikiwa wake huyo, wala hana uwezo wa kununua kiwanja na kujenga makazi mapya.

2539 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!