‘If you can’t fight them, join them’

Huu ni usemi wa wahenga Waingereza hapo kale. Asili yake sijaifahamu sawa sawa, lakini ni usemi unaotumika sana.

Nia au shabaha ya usemi huu ni ushauri kwa makundi hasimu, kupata suluhisho la kudumu maana kupambana daima ni ishara ya mvurugano na kutoweka kwa amani. Ni nani asiyependa kuishi kwa amani na mstarehe ajipatie maendeleo yake mwenyewe?

Usemi kuwa “iwapo huwezi kupigana nao, basi ungana nao” una funzo muhimu sana kwa wanasiasa. Hapa inamaanisha kuna mapambano ya kisiasa kati ya itikadi tofauti – ni mapigano kwa maana ya vita kati ya makundi na hasa baina ya mataifa hasimu. Kwa vyovyote vile, usemi unashauri kuwa ukiona umezidiwa kimbinu au kinguvu (physical confrontation) njia nzuri na ya suluhisho ni wewe unayezidiwa kukubali yaishe.

Kivita bwana, ukishakubali yaishe, hapo unajingiza katika hali ngumu sana. Hapo utapewa masharti ambayo itakubidi uyakubali na huo ni unyonge (humiliation) mkubwa. Lakini kisiasa, hakuna haja ya masharti, bali ni mgeuko tu wa hali. Ndipo pale mtu anabadili msimamo wake wa itikadi na kujiunga na msimamo au itikadi hiyo nyingine.

Waingereza wanaita hali ya namna hiyo kuwa “crossing the floor” na hali namna hiyo imeshazoeleka kule kwa wenzetu.

Niliwahi kuandika katika makala ile ya “ASILI YA VYAMA VYA SIASA” pale nilipogusia kihistoria namna “The Whings” walivyobadilika kuwa “Liberals” na hata kuwa “Laborities”. Aidha, nilisema kule Marekani “The Federalist” waliweza kubadilika na kuwa au “Republican” au “Democratic”. Suala la kuhama kutoka chama fulani na kuingia chama kingine si suala geni katika ulimwengu wetu.

Huku Bongo, tuna mtazamo tofauti. Huku mtu akibadili msimamo akahama kutoka chama “A” na kwenda chama “B” kunatokea maneno mengi. Kwanza kabisa kunazuka dhana ya biashara ya binadamu. Hapo kunasikika maneno kama “kununuliwa” au “kurubuniwa” au hata neno lile lisilopendeza kutamkwa “kibaraka”.

Lakini wahenga walituasa kuwa mkuki kwa nguruwe mtamu, lakini kwa binadamu huwa mchungu”. Usemi huu una funzo kuwa, tendo likielekezwa kwa mwingine linakuwa jema au zuri. Kumbe tendo lile lile likikufika wewe, hapo linakuwa chungu na kulaaniwa. Hivyo ndivyo hali yetu binadamu sote.

Usemi mwingine unaongelea hivi “mwosha naye huja akaoshwa” hapo sasa kunasikika makelele wakati yeye anaosha mtu mwingine anajisikia uhodari na anaona fahari kweli. Lakini ikitokea sasa zamu yake yeye huyo aliyekiosha kuoshwa, mama wee si malalamiko hayo!

Yote haya yanalenga kwenye siasa katika nchi yetu. Pale wana-CCM wanapohamia vyama vingine, vyama vile vinafurahia na kuwasifia wahamaji wale na kuwaita mashujaa na wana demokrasia kweli. Wameona ukweli na ndiyo maana wamefuata na hivyo wamejikomboa toka minyororo ya dhuluma.

Hayo yalionekana mwaka 2015 wakati mawimbi ya makada na viongozi wa CCM walipohamia vyama vya upinzani. Hakuna ilipotajwa neno “kununuliwa”. Ukaja wakati mbunge wa Singida na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii “ku-cross the floor”. Kukasikika vifijo vya furaha tu.

Mwaka 2017 na 2018 hii kumetokea wimbi la viongozi kuanzia madiwani mpaka wabunge kuhama kutoka Upinzani na kuingia CCM. Mwee! Jamani, si maneno hayo! Watu wamenunuliwa, watu wamelaghaiwa na kadhalika na kadhalika. Sasa ukiulizia kwa bei gani kwa kila aliyenunuliwa, au ni kiasi gani kila mmoja amehongwa na akahongeka (thamani) – hakuna anayeweza kutoa jibu.

Hali hii ndiyo ninaita “mwosha naye huoshwa” hapo kuna ubaya gani? Nini kinamtoa mtu kutoka chama kimoja kwenda na kuingia chama kingine? Hapa nafikiri ndugu yangu Shibuda yule Msukuma wa misamiati angesema “siri ya mtungi aijuaye ni kata”. Ina maana kila anayehama chama fulani na kuingia chama kingine ana sababu yake maalumu anaijua mwenyewe.

Sheria za uchaguzi zilitungwa na Bunge. Katiba imetoa vipengele kadhaa kuelekeza namna ya kuendesha uchaguzi. Baadhi ya walalamikaji wa leo ni wale waliopata kuwa wabunge enzi hizo na walishiriki kutunga sheria zile. Sasa haieleweki wanapolaumu leo utaratibu huu kwani pale walipokuwa bungeni hawakufikiria kuwa matokeo ya uamuzi wao ule siku zile ungekuja kuwaathiri na wao watungaji wenyewe?

Toka baada ya ule uchaguzi Mkuu wa 2015 mpaka sasa kumetokea uchaguzi mdogo kadhaa. Kwa kadri ya maneno ya Mheshimiwa Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, aliyasema haya: “…Zimefanyika mara tano katika majimbo na kata mbalimbali ambazo CCM imeshinda mara zote isipokuwa         Kata ya Ibigi – Mbeya iliyochukuliwa na CHADEMA.”

Sasa kuanzia ule uchaguzi mdogo wa Kinondoni, ukafuata ule wa Buyungu, ukafuata huu wa Monduli na Ukonga, matokeo yake yote yamelalamikiwa huku CCM wamechekelea wakati vyama pinzani vyote wamelia “foul”.

 Nakumbuka Kampeni za Monduli na Ukonga zilivyoendeshwa. Kulikuwa na tambo mbalimbali kutoka viongozi wa kila chama. Kuna wakati makundi ya wasikilizaji yalionekana kwenye runinga na pia katika magazeti.

Watu wengi wamesheheni wakisikiliza waomba kura. Haikuweza kutabirika chama kipi kitaibuka mshindi kwa mwonekano ule wa usikilizaji kwenye kampeni zile. Basi, iliaminika kulikuwa na uhuru wa kujieleza na michuano ilikuwa mikali kwelikweli.

Kule Monduli ilisikika viongozi wakiapa, “Hatoki mtu hapa hata CCM wakileta wabunge wangapi – watagalagazwa tu”. Hizo zilikuwa ni tambo za CHADEMA. CCM nao wakijibu mapigo walisema – “Hapa Monduli hali ya hewa ilishachafuliwa, tumekuja kuisafisha hali ile na kubadili upepo!”

Mwisho wa tambo zile za vyama ulikuwa wapigakura Jumapili, Septemba 16, 2018 pale walipotoa uamuzi wao.

Kwa Monduli matokeo tuliyopewa ni kuwa CCM wamevuna kura 65,714 wakali CHADEMA wameambulia kura 3,167 tu! Kwa Ukonga nako matokeo tuliyopewa ni kuwa CCM wamezoa kura 77,795 wakati CHADEMA wamepata kura 8,676! Mimi hapo nabaki kujiuliza matokeo haya maana yake nini? Hapa kuna usemi kuwa “mwenye macho haambiwi tazama au ona”

Kwa mtazamo wa kawaida, ningeweza kusema wale viongozi waliohamia CCM kutoka upinzani walisukumwa na ule usemi wa Waingereza, kuwa “If you can’t fight them, then join them” na ndiyo maana wamejiunga huko. Hii inamaanisha nini? Inamaanisha, wanataka kujenga taifa moja lenye mshikamano ili kuharakisha maendeleo yetu.

Kuna usemi wa wahenga kuwa “mvunja nchi ni mwananchi huyo huyo”, basi kinyume cha usemi ule ni kwamba mjenga nchi ni huyo huyo mwananchi mwenyewe. Labda inafaa hapa tukumbushane yale maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambvarae Nyerere katika ile hadithi yake. Alisema, kama bado nakumbuka vizuri (If my memory in still sharp) kuwa kijana aliekwenda kutafuta posa kule milimani. Njiani alimkuta bibi kizee aliyempa masharti ya kumfikia yule kimwana. Mwalimu alimalizia hadithi ile kwa maneno haya, “Mimi sitaki nigeuke jiwe hata kidogo, watasema huyo muoga, watazomea huyo, huyo…, lakini potelea mbali. Mimi bado ninaamini kwa dhati kabisa juu ya Ujamaa.

Wanaozomea ndio hao mafisadi, warongo na wapinga Ujamaa na maendeleo…, ama tulikuwa tuna wadanganya watu juu ya huo Ujamaa na mimi nasema sikuwahi kudanganya…” hao waliohamia hawakutaka kugeuka mawe nadhani.

753 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons