DAR ES SALAAM

Na Christopher Msekena

Bara la Afrika halijawahi kukaukiwa na vijana wenye vipaji wanaofanya shughuli za usanii na sanaa ndani na nje ya bara hili, huku wakifikia hatua mbalimbali za mafanikio.

Miongoni mwa vijana hao ni Michael Baiye, ambaye akiwa stejini hufahamika zaidi kama Jbwai, msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Cameroon anayeishi nchini Canada kwa sasa.

Mwishoni mwa wiki hii, Jbwai anatarajia kuingiza sokoni albamu fupi (EP) inayoitwa ‘Certified’.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Jbwai na mwandishi wa makala hii kwa njia ya mtandao:

Swali: Kwa ufupi Jbwai ni nani na aliingia vipi kwenye ulimwengu wa sanaa?

Jbwai: Mimi ni mwanamuziki kutoka barani Afrika; raia wa Cameroon. Ni mwimbaji, mtunzi wa nyimbo na mtayarishaji wa muziki. Nilizaliwa Septemba 28, 1993. Nilianza au kuingia rasmi katika anga za muziki nilipohamia Toronto nchini Canada, ingawa kwa kusema ukweli historia yangu katika muziki ilianza nikiwa bado mdogo sana.

Swali: Je, unakabiliwa na changamoto gani katika muziki wako ndani na nje ya Canada? 

Jbwai: Changamoto kubwa kama msanii wa Kiafrika aliyeko Canada, ni kwamba bado sijaunganishwa moja kwa moja na mashabiki damudamu wa muziki huu ambao ni watu kutoka Afrika. Hawa nikiwapata au kuunganishwa nao kwa hakika watahusika kwa urahisi katika kuupaisha muziki wangu kimataifa. 

Swali: Ungependa kufanya kazi na wanamuziki gani kutoka Tanzania au Afrika Mashariki? 

Jbwai: Msanii kutoka Tanzania ninayetamani sana kufanya naye kazi ni yule nyota anayependwa zaidi na mashabiki, Diamond Platnumz. Lakini wapo wasanii wengine wa Tanzania kama Harmonize na Rayvanny ambao nina mipango ya kufanya nao kazi siku za baadaye.

Swali: Hadi sasa mafanikio gani umepata kupitia muziki wako?

Jbwai: Katika kazi yangu yote ya muziki, nimekuwa na mafanikio mazuri kisanii kwa kuwa nimekuwa na maonyesho mazuri. Pia nina uhusiano mzuri na watu wengi, uhusiano ambao umenipa faida kubwa katika maisha ya kisanii na maisha ya kawaida.

Swali: Kwa nini ulifikiria kukuza muziki wako Afrika? 

Jbwai: Afrika ndipo mahali ambapo watu wanaupenda zaidi muziki wangu. Pia ni nyumbani hata kama tunaishi huku ughaibuni. Namshukuru Meneja wangu, Rim Life Immortal, kwa kazi kubwa anayofanya.

Swali: Una mipango gani kwa mwaka huu hasa nchini Tanzania?

Jbwai: Katika miezi ijayo mpango wangu ni kutembelea Tanzania, kuwa na maonyesho kadhaa na kujiunganisha na mashabiki wangu na kujifunza tamaduni za huko ambazo naamini nitazifurahia.

Pia Mei 13, mwaka huu, yaani Ijumaa ya wiki hii, nitaachia EP yangu inayoitwa ‘Certified’ na kabla ya hapo nitaachia wimbo wa kwanza kutoka kwenye EP hiyo unaoitwa ‘Gbas Gbos’ ambao naamini utafanya vizuri kwenye kumbi za starehe huko Afrika hivyo ma-DJ wajiandae kuwarusha mashabiki kwa muziki mzuri kutoka kwangu.

By Jamhuri