Wiki iliyopita nilisitisha safu hii kwa toleo moja kwa nia ya kuandika juu ya kifo cha mmiliki wa vyombo vya habari, Dk. Reginald Mengi. Hadi leo bado naendelea kusikitika na Watanzania wanasikitika. Hata hivyo, ni lazima maisha yaendelee. Tumwombee huko aliko apumzike kwa amani, ilhali sisi tuliobaki tukiendelea kumuenzi kwa kazi ya mfano aliyoifanya maishani mwake.

Sitanii, safu hii inasema: “Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania.” Leo naandika sehemu ya 13 niliyoiahidi muda mrefu. Safu hii kwa kiasi kikubwa inatokana na Sheria ya Kampuni Na. 12 ya Mwaka 2002. Katika sehemu ya kuanzisha na kusajili Jina la Biashara nilitumia muda mrefu mno kuelezea, ila katika eneo hili la kampuni nitaeleza mambo ya msingi.

Kwanza, niseme bayana hapa kuwa usajili wa kampuni kuukamilisha ni lazima umshirikishe mwanasheria aweze kukuandikia Katiba ya Kampuni yako (Memorandum of Understanding and Articles of Association). Andiko hili lina misingi na matakwa mengi ya kisheria yenye madhara au faida mbele ya safari, hivyo ni vema ukamtumia mwanasheria kuliandaa.

Siku hizi mambo yamerahisishwa. Ukijisajili kupitia kwenye mtandao wa Brela, una uwezo wa kusajili kampuni ndani ya siku 7 hadi 14 kwa Tanzania, na kama nyaraka zako ziko sawa unasajili ndani ya siku za kazi 5. Katika maandishi yangu ya awali nilizungumzia kufungua akaunti Brela. Kwa popote ulipo duniani, unaweza kupata maelezo ya kina juu ya usajili wa kampuni ukiingia katika mtandao wa www.brela.go.tz.

Sitanii, zipo hatua za kufuata wakati wa kusajili kampuni. Hatua ya kwanza unapaswa kuchunguza iwapo jina unalotaka kutumia kwa kampuni yako limewahi kutumiwa na kampuni nyingine au la. Pili, ukibaini kuwa jina unalotaka kutumia halina kikwazo, unaanza mchakato wa kusajili kampuni kwa kujaza fomu Na. 14a na 14b. Kama kampuni inaanzishwa hapa nchini, baada ya kujaza fomu hizi unaambatanisha Katiba ya Kampuni unawasilisha Brela. Siku hizi uwasilishaji unafanyika mtandaoni.

Ikiwa kampuni unayotaka kuanzisha hapa nchini ilikwisha kusajiliwa katika nchi nyingine, basi unawasilisha nakala ya Memorandum and Articles of Association za kampuni hiyo, kisha taarifa za iliposajiliwa katika nchi husika, orodha ya wakurugenzi na majina ya wawakilishi wa kampuni hiyo hapa nchini.

Zipo kampuni za aina nne na ngazi mbalimbali. Kampuni inaweza kuwa (1) Binafsi. (2) Umma. (3) Tawi la Kigeni. (4) Inayomilikiwa na serikali. Kampuni hizi pia zinaweza kuwa za mmiliki pekee (sole proprietor), umiliki wa ushirika (joint venture), umiliki wa kuunganisha nguvu (incorporation) na aina nyingine kadhaa.

Kampuni inapaswa kuwa na hisa, ikiwa itafanya biashara na kupata faida (company by shares) au kutokuwa na hisa (company by guarantee), ikiwa itakuwa inatoa huduma kwa jamii au inaunganisha wanataaluma wanaojadili masuala ya kitaaluma bila kupata au kugawana faida inayotokana na shughuli zinazofanywa na kampuni.

Sitanii, kampuni hizi zinapaswa kuwa na ukomo katika uwajibikaji (limited liability) au kuachia wazi kwamba ikitokea mtu anafilisika, basi wakurugenzi wanaweza kuuza hata mali zao za urithi kulipa madeni yaliyotokana na kampuni husika (unlimited liability).

Kama nilivyoeleza wakati wa kuanzisha biashara kwa kutumia jina la biashara, kwa sasa usajili wa kampuni umerahisishwa mno. Kuanzia hatua ya uchunguzi wa jina hadi kukabidhiwa cheti cha usajili, ikiwa una kila kitu unapaswa kuchukua si zaidi ya siku 5 za kazi kukamilisha usajili. Je, unazifahamu nyaraka muhimu tatu unazopaswa kuwa nazo baada ya kusajili kampuni? Usikose nakala yako ya Gazeti la Uchunguzi JAMHURI wiki ijayo.

305 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!