Kagasheki akimweza huyu, ataweza kila kitu

 

Hivi karibuni, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), aliubua bungeni mkataba ulioingiwa baina ya kampuni za Uranium Resources PLC, Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited, mkataba ambao umetengenezwa na kampuni ya Kitanzania ya Rex Attorneys na kusainiwa Machi 23, 2007.

Mkataba husika, ambao vipengele vyake vinaainisha kwamba unatakiwa uwe wa siri, unaihusu kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Bwana Mohsin M. Abdallah na ndugu Nargis M. Abdallah.”

 

Mohsin Abdallah ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja wa wafadhili wakubwa wa chama hicho. Huyu ni Makamu Mwenyekiti wa Chama wa Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA).

 

Chama hiki ni kile kinachofanya juhudi kubwa sana kuhodhi tasnia ya uwindaji wa kitalii. Kwa miaka mingi chama hiki ambacho wanachama wake wengi ni wageni, kimehodhi tasnia hii na kujitahidi kuwafanya Watanzania kuwa wachovu na wasioweza kuishiriki.

 

TAHOA ina vibaraka wake kadhaa wazalendo. Hawa ni wale wanaohaha huku na kule kuwarubuni, kuwahonga na kuhakikisha wanawaweka “mfukoni” viongozi wengi ndani ya CCM na Serikali. Haya ya TAHOA kwa leo nayaacha. Kuna makala zake zitakuja.

 

Mohsin ni mmoja wa watuhumiwa wakuu wa rushwa na ukwepaji kodi. Haya si maneno yangu! Mwaka 1996, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliunda Tume ya Kuchunguza Kero ya Rushwa nchini. Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe kenda, iliongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba. Tume ilibainisha namna Mohsin alivyo na nguvu na ushawishi kuanzia kwa viongozi wa vyombo vya usalama hadi kwa wanasiasa. Tume iliainisha namna alivyoweza kukwepa kodi.

 

Anayetaka kuyajua vema hayo, asome ripoti ya Jaji Warioba. Tangu wakati huo hatujapata maelezo kama ameacha tabia hiyo. Jumamosi iliyopita inaweza kuwa Jumamosi ngumu kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki. Nasema inaweza kuwa Jumamosi ngumu kwa sababu alitoa ahadi bungeni ambayo kwa ukweli wa mambo ni ngumu kutekelezeka.

 

Balozi Kagasheki amesema kampuni ya Mohsin imekiuka Sheria ya Wanyamapori kwa kukodisha kitalu cha uwindaji ilichopewa, kwa kukiingiza kwenye shughuli za utafiti wa madini ya urani. Kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 kukodisha tu kitalu ni kosa! Alichokisema Balozi ni kwamba leseni ya kada huyo wa CCM itasimamishwa kutokana na kukiuka sheria.

 

Sina shaka na uwezo na nia njema ya Waziri Kagasheki katika kulishughulikia suala hili kisheria. Kwa muda mfupi aliopewa kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii ameonyesha nia thabiti ya kuleta mapinduzi ya kweli na yenye tija kwa Taifa.

 

Shaka ninayoipata ni kwamba Waziri hamuwezi Mohsin na kundi lake. Huyu mtu ni kada wa Chama Cha Mapinduzi. Ni jeuri (soma tangazo lake katika The Guardian, Agosti 11, 2012). Kuna ushahidi wa wazi kwamba mambo mengi machafu katika nchi hii yanafanywa na watu walio ndani ya chama hicho.

 

Juzi, Bunge limeelezwa kwamba mmoja wa vinara wa mtandao wa ujangili nchini ni kada wa Chama Cha Mapinduzi aliyepo Karatu mkoani Arusha. Mohsin ana ukwasi. Ni mmoja wa wafadhili wakuu wa Chama Cha Mapinduzi. Kuanzia kwake mkoani Kigoma hadi ngazi ya Taifa hakuna asiyemjua. Hakuna mgombea awaye yeyote ndani ya CCM Kigoma ambaye hajawahi kunufaishwa moja kwa moja au kwa njia nyingine kwa misaada yake.

 

Mohsin anajulikana kwa kuwa karibu na viongozi wote wakuu ndani ya CCM na Serikali yake. Anajulikana kwa watendaji wengi wakuu wa idara na taasisi za Serikali. Amepata vitalu vingi vya uwindaji wa kitalii. Mtu huyu, mwenye sifa zote hizi, mwenye ukaribu huu na wakubwa ndani ya CCM na Serikali, ndiye Kagasheki anayetuhakikishia kuwa atamnyang’anya kitalu. Wallah kama kweli Balozi Kagasheki ataliweza hilo, na Mohsin akaridhia, basi Waziri atakuwa amevunja rekodi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

 

Ndugu zangu, kama nilivyosema, watu wengi wanaovuruga mambo katika Taifa letu wamo ndani ya CCM. Nje ya chama hicho hakuna anayeweza kufurukuta kukwepa sheria na kanuni za nchi. Ukiona mfanyabiashara mkubwa asiye mfuasi wa CCM au kama alivyo Mustafa Sabodo anayeisaidia Chadema mamilioni ya shilingi, basi huyo mtu ni msafi wa kweli. Kupambana na mtandao wa watu aina ya Mohsin ambao ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ni kazi inayompasa Waziri kuwa jasiri kweli kweli.

 

Nitatoa mfano mmoja wa kweli wa nguvu za makada wa CCM. Kuna kampuni moja kutoka nchi jirani iliyokwenda Arusha na kukabidhiwa moja ya viwanda vyetu vya maziwa. Kampuni ikaahidi kwa mbwembwe zote kwamba italeta mashine za kisasa kusindika maziwa. Ikapewa kiwanda.

 

Matokeo yake ikaamua kugeuza kiwanda hicho ambacho ni mali ya Watanzania kuwa ghala la kuhifadhi maziwa yake inayoyasindika nchini mwao. Ikawa na gari kama la kubebea “maziwa ghafi” kutoka Tanzania ili yaonekane yanapelekwa nchi humo kusindikwa na baadaye yarejeshwe nchini Tanzania bila kulipiwa ushuru, maana yameongezwa thamani!

 

Kampuni hiyo ikapewa kibali cha kuvuka mpaka kinachowazuia wafanyakazi wa forodha kulikagua! Likawa linajazwa maji, linavuka mpaka! Baada ya muda (hadi leo) maziwa yakawa yananunuliwa kwa wafugaji wa nchi hiyo. Yanasindikwa na kuingizwa hapa nchini kwenye soko! Kiwanda chetu Arusha kimegeuzwa kuwa ghala la maziwa ya wafugaji wa nchi hiyo. Wakulima wetu wanahangaika kuuza maziwa yao kwenye hoteli!

Waziri mmoja wa Serikali yetu alilitambua hilo.

 

Akaamua kuwabana ili wanunue maziwa ya Watanzania na wafunge mashine kama walivyoahidi. Wale wenye kiwanda, kwa kulijua hilo, wakamfuata mmoja wa mawaziri wakuu wastaafu. Waziri Mkuu mstaafu akamkemea waziri wetu asiendelee kufuatilia jambo hilo. Sinema ikaishia hapo! Maziwa bado yanatoka ng’ambo. Yanatunzwa kwenye “maghala” ya Watanzania.

 

Hakuna mashine iliyofungwa. Waziri akakanwa kwa sababu Waziri Mkuu mstaafu ana maslahi binafsi kwenye kampuni hiyo ya wageni. Hii ndiyo Tanzania. Ndiyo maana nasema Balozi Kagasheki ametoa ahadi ngumu na nzito mno kwake. Sidhani kama atamweza Mohsin. Akimweza, atawaweza pia makada wa CCM wanaoendesha ujangili.

 

Atawaweza wale wanaohangaika ili vitalu vya uwindaji vigawiwe upya. Atawaweza TAHOA wanaoamini kuwa Mungu kawapa wanyamapori wa Tanzania! Atawaweza majangili wanaofugwa kwa msaada mkubwa wa vyombo vya usalama nchini.

 

Na akishaonyesha mfano huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, naye anaweza kuiga ujasiri wake. Atamwondoa mbunge mmoja anayejitanabaisha kuwa ni mlokole ambaye kajenga hekalu katika mdomo wa bahari! Atawaondoa wote waliovamia maeneo ya wazi, vikiwamo viwanja vya watoto kucheza.

 

Nasema kama Balozi Kagasheki ataweza kumbana Mohsin, basi mawaziri na watendaji wengine wote serikalini wenye nia njema ya kulitumikia taifa letu, wataiga ujasiri wake. Watawashughulikia makada wa CCM wanaoongoza kwa kuvunja sheria na kanuni katika Taifa letu. Jeuri ya fedha ni mbaya. Inalindwa na mtandao ulio ndani ya CCM na Serikali. Wenye lugha yao wanasema hivi ‘Funika kombe mwanaharamu apite’.

 

Katika nchi hii ukitaka kufunika mabaya yako, ukitaka kutapanya mali, ukitaka usiguswe, ukitaka mambo yako yakunyookee hakikisha unakuwa kada wa CCM! Kwangu mimi na wengine, hili ni suala la kusubiri tu kuona kama kweli Balozi Kagasheki ataliweza. Akiliweza, nitakuwa wa kwanza kumpongeza. Lakini nani aliyesema hakuna lisilowezekana?  Yawezekana Balozi Kagasheki ndiye nabii tuliyemsubiri kwa muda mrefu kuikomboa Wizara hii.