Hatimaye maandamano ya wana-CCM wilayani Monduli kupinga Julius Kalanga kuwa mgombea pekee wa ubunge kupitia chama hicho yamegonga mwamba baada ya kada huyo kujitokeza peke yake kuchukua na kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Kalanga aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kujiuzulu na kujiunga na CCM, iwapo atapitishwa na vikao vya ngazi ya juu, atachuana na mgombea wa Chadema atakayepitishwa kesho.

Siku mbili zilizopita, baadhi ya wanachama wa CCM kata ya Isilaleo, Monduli Juu na Sepeko waliandamana hadi ofisi za chama wakimtuhumu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima kwamba kwa kushirikiana na viongozi wengine, wanapanga njama ili Kalanga apitishwe kuwa mgombea ubunge pasipo kufanyika kwa kura ya maoni.

Hata hivyo, Lengima alikanusha madai hayo akisema CCM ina utaratibu wake wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, hivyo kuwataka wanachama wa CCM kuwa watulivu.

Akizungumza jana, Lengima alisema juzi ilikuwa siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu za ubunge na ni Kalanga pekee aliyechukua na kurejesha.

“Taarifa nilizonazo ni kuwa amechukua fomu Kalanga pekee na kama kutakuwa na mabadiliko tutatoa taarifa,” alisema Lengima na kubainisha kuwa utaratibu wa kumpata mgombea wa chama hicho utafuatwa.

Wakati Kalanga akionekana kuwa mgombea pekee, ndani ya Chadema, Fred Lowassa, mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, naye amejitosa kuomba ridhaa ya chama hicho kumpitisha kugombea ubunge.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Aman Golugwa alisema jana ilikuwa siku ya mwisho kuchukua na kurejesha fomu ndani ya chama hicho.

Diwani atetea walioandamana

Akizungumzia maandamano ya wanaCCM kupinga Kalanga kuwa mgombea pekee, Diwani wa Sepeko (CCM), Kimay Mshangama alisema wananchi wa kata yake walikuwa na uhuru wa kuandamana na hawajavunja sheria, kanuni na taratibu za chama hicho.

“Walikuwa wanataka taratibu zifuatwe kwani kuna wana CCM wengi walikuwa wanataka kugombea, wapewe fursa,” alisema.

Alibainisha kuwa hatima ya mgombea ubunge katika jimbo hilo itajulikana katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Monduli kitakachofanyika kesho.

Alisema miongoni mwa watakaoshiriki kikao hicho ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, “Maswali mengi tutauliza ili tupate majibu naomba na nyie waandishi mje.”

Alisema hana uhakika kama hakuna wana CCM waliochukua fomu kuwania kupitishwa kuwania ubungena kushindana na Kalanga.

Kalanga ashukuru wana CCM

Akizungumza jana, Kalanga ambaye anaungwa mkono na viongozi wa mila na wan-CCM wenye misimamo ya kati alisema hana taarifa kama kuna mgombea mwingine aliyejitokeza ndani ya chama hicho.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare akizungumzia uchaguzi huo alisema mchakato wa uteuzi; wa nani atakagombea kwa tiketi ya chama hicho bado unaendelea .

Sanare ambaye pia ni mkazi wa Monduli alisema baada ya dirisha la uchukuaji fomu kufungwa, taratibu nyingine zinaendelea na kwamba vikao ndivyo vitakavyoamua nani atakuwa mgombea.

“Mchakato bado unaendelea na vikao vya chama bado vinaendelea vuteni subira,” alisema Sanare.

Waliochukua fomu Chadema

Alipoulizwa kuhusu mchakato wa uteuzi ndani ya Chadema, Golugwa ambaye pia katibu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, alisema mbali na Fred, wengine waliochukua fomu ni diwani wa viti maalumu na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Arusha, Cecilia Ndosi.

Alisema wengine ni Yona Laizer, Lobulu Kivuyo na Eric Ngwijo na kubainisha kwamba wagombea hao watapigiwa kura katika kikao cha kesho kitakachofanyika katika Kata ya Migungani Wilaya ya Monduli.

Alisema baada ya kikao hicho ambacho kitaratibiwa na ofisi ya Kanda ya Kaskazini, majina hayo yatapelekwa katika Kamati Kuu ya chama hicho kwa uteuzi wa mwisho.

Kuhusu Jimbo la Korogwe Vijijini ambako utafanyika uchaguzi mdogo kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wake, Stephen Nyongani ‘Profesa Majimarefu’, kiongozi huyo wa Chadema alisema aliyejitokeza hadi sasa ni Amina Saguti peke yake.

“Wengine walichukua fomu lakini hawakurejesha hadi muda wa mwisho. Hawa ni Aaron Mashuve na Dafi Dafi,” alisema na kubainisha kuwa kikao cha kumjadili Amina kitafanyika Jumapili.

Katika uchaguzi mwingine mdogo wa Jimbo la Ukonga, katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Joyce Mkaugala alisema katika makada watatu wa chama hicho wamechukua fomu akiwamo aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Mwita Waitara.

Waitara ambaye alikuwa mbunge wa Ukonga tangu mwaka 2015 hivi karibuni alijivua uanachama wa Chadema na kuhamia CCM.

Wengine waliochukua fomu ni Nassoro Kivuga na Emmanuel Mwita.

By Jamhuri