Kamishna atishiwa kuuawa

Kamishna wa Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Dawa za Kulevya, William Sianga, ametishiwa kuuawa.
JAMHURI limethibitishiwa kuwa mfanyabiashara wa madini, Timoth Mwandigo, ambaye ni mkazi wa Kijitonyama, Dar es Salaam anashikiliwa polisi akihusishwa na tishio la kumuua Sianga.
Pamoja na tuhuma za kumuua Kamishna Sianga, Mwandigo anakabiliwa na tuhuma nyingine ya kukutwa na kilo 108.67 za madini yanayodaiwa kuwa ni ‘dhahabu feki’.
Habari kutoka vyanzo vya uhakika zinaonesha kuwa Mwandigo amekuwa akishirikiana na baadhi ya askari polisi waandamizi (majina tunayo), wengi wao wakitoka katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni.
Kituo cha Polisi Oytserbay kwa muda mrefu kimewekwa kwenye orodha ya vituo vichache nchini vyenye askari na maofisa wa polisi wanaoshirikiana na matapeli wa madini, watuhumiwa wa biashara za dawa za kulevya na makosa mengine ya ushawishi wa fedha.
Mawasiliano kati ya Mwandigo na polisi hao tayari yamenaswa, yakiwamo ya siku ambayo kulikuwa na mtego wa kumkamata.

Imeelezwa kuwa Kamishna Sianga alishiriki kumkamata mtuhumiwa Mwandigo, na ndipo alipotishiwa maisha na mfanyabiashara huyo.
“Lengo lilikuwa kwenda kukamata dawa za kulevya baada ya kupata taarifa, Kamishna akaondoka, na kikosi chake; lakini kwenye msako huo yakapatikana madini yanayodhaniwa kuwa ni feki yakiwa kwenye mabegi mawili na ndoo nne,” kimesema chanzo chetu.
Imeelezwa kuwa wakati upekuzi ukiendelea, baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakiwasiliana na ‘polisi wanaowalinda’, watuhumiwa hao.
JAMHURI limefanikiwa kupata majina ya maofisa wa polisi wanaotuhumiwa, lakini kwa sasa linaendelea kuhifadhi majina hayo. Nafasi zao ni; ofisa mwandamizi kutoka Kituo cha Polisi Mabatini, ofisa mwandamizi kutoka Ofisi ya RPC Kinondoni, ofisa mwandamizi kutoka Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya; na ofisa mwandamizi aliyeko Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Chanzo chetu cha habari kilichokuwa eneo la tukio kinasema: “Alikuja (ofisa mwandamizi kutoka Polisi Mabatini) akaanza kupiga simu kwa muda mrefu sana, wakati huo Kamishna (Sianga) kwa bahati huyo askari wakati anapiga simu hakumuona Kamishna na inaelekea hamfahamu.

“Aliendelea kuongea na simu nje ya nyumba hiyo, ndipo Kamishna alipomfuata na kumweka chini ya ulinzi. Alijitetea kuwa yeye ni askari na akataja cheo chake, lakini Sianga hakujali, alimweka chini ya ulinzi.
“Akiwa chini ya ulinzi alitokea kigogo mwingine wa Jeshi la Polisi (kutoka Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya) akaanza kumtetea yule askari. Hapo ndipo Sianga alipoonesha makucha yake kwani naye aliwekwa chini ya ulinzi na kazi ya upekuzi ikaanza,” kinasema chanzo chetu.
Imeelezwa kuwa baada ya kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo pamoja na ‘dhahabu’, wanamtandao walifanya jitihada ili aachane na mfanyabiashara huyo kwa kupeleka kesi hiyo Kituo cha Polisi Oysterbay, bila mafanikio.
“Hawa jamaa walianza kulazimisha kesi hiyo ipelekwe Oysterbay kwani mtuhumiwa alikamatiwa Wilaya ya Kinondoni, Kamishna akakataa, madini akakabidhiwa Kamishna wa Madini…mtuhumiwa alikuwa ameshaandaliwa mazingira ya kutokomea na mzigo wote,” kimesema chanzo chetu.

Taarifa za kiusalama zinamtuhumu Mwandigo kwa kuwa na mtandao madhubuti ndani ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Nishati na Madini unaomsaidia kufanikisha uuzwaji ‘madini feki’ kwa raia wa kigeni.
JAMHURI limezungumza na Sianga, na kukiri kuwapo kwa tukio hilo.
“Ni kweli niliongoza kikosi kazi ambacho kilifanya upekuzi nyumbani kwa Mwandigo, tuliweza kukamata dhahabu nyingi na tumezikabidhi kwa Kamishna wa Madini.
“Hili suala la huyu mtu kuapa kwamba ataniua nimelipata tayari, lakini hilo haliwezi kunizuia kutimiza wajibu wangu. Pamoja na kwamba ana mtandao mkubwa hilo halinitishi hata kidogo na wala si mara ya kwanza kukutana na vitisho vya aina hii. Mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu, hivyo sina shaka na nitaendelea kuongoza mapambano ya uhalifu na wahalifu niliyokabidhiwa na Rais,” amesema Sianga.
Amesema suala la mtuhumiwa huyo kukamatwa na vitu hivyo vinavyodhaniwa kuwa ni dhahabu, linashughulikiwa na mamlaka zinazohusika kisheria.

Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, amethibitisha kupokea mifuko miwili na ndoo nne za vitu vinavyodaiwa kuwa ni madini kutoka ofisi ya Kamishna wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Mchwampaka ameliambia JAMHURI kwamba uzoefu wake unamwezesha kutambua kuwa madini yaliyokamatwa si dhababu halisi, bali ni feki. Hata hivyo, amesema uchunguzi wa kimaabara unafanywa ili kubaini ukweli.
Hadi tunakwenda mitamboni Mwandigo alikuwa amezuiwa katika Kituo cha Polisi Chang’ombe akiwa ametolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikolazwa kwa siku kadhaa kabla ya kuondolewa Juni 16.
Katika Wodi ya Kibasila Na. 13 ambako alikuwa amelazwa, baadhi ya wauguzi waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina walisema mtuhumiwa huyo alikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Tuhuma Polisi Oysterbay
Mwaka jana, JAMHURI, kwa mara nyingine, liliandika habari iliyohusu magenge ya matapeli kwenye biashara ya madini, yaliyoibuka na kuendesha shughuli zake bila hofu.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI ulibaini kuwapo kwa matukio ya utapeli na kuifanya sifa ya Tanzania izidi kuchafuka mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Mwaka 2013, JAMHURI lilichapisha majina na kampuni za matapeli wa madini; hatua iliyoifanya Serikali ikunjue makucha kupambana na magenge hayo.
Wiki kadhaa zilizopita, raia wawili wa Singapore walitapeliwa dola 45,000 (shilingi zaidi ya milioni 90), baada ya kuuziwa dhahabu feki.
Wageni hao, Yang Jun Ho Joshua na Thiam Seng Oh, wanasema walitapeliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa kampuni ya Tamasha Mining (T) Ltd ya jijini Dar es Salaam. Haieleweki vema mahali ziliko ofisi za kampuni hiyo kama ni Tangi Bovu au Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Wanasema kwenye utapeli huo wahusika wengine ni polisi na maofisa wa forodha. Uzoefu unaonesha kuwa mara kadhaa utapeli kwenye biashara ya madini hujumuisha mtandao mkubwa kuanzia kwa matapeli wenyewe, polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hata maofisa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama.
Kituo cha Polisi Oysterbay kinatajwa kuongoza katika matukio ya utapeli, huku kesi nyingi, ama zikiishia hapo, au zikivurugwa na askari na maofisa katika kituo hicho.
Matukio mengi na makubwa ya utapeli wa madini yamekuwa yakitokea Wilaya ya Kinondoni, na hivyo kukifanya Kituo cha Polisi Oysterbay kuwa kwenye orodha ya sehemu zinazotajwa kukubuhu kwenye uhalifu huo.

Vita dhidi ya mirungi
Katika hatua nyingine, Sianga amesema anashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwenye operesheni ya kuteketeza mirungi wilayani Same, Kilimanjaro.
Kamishna wa Operesheni wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela, ambaye anaongoza kikosi kazi kilichopo Same, amesema kwa siku moja (Juni 15) waliteketeza ekari 25 za mirungi zinazomilikiwa na familia 10 katika Kijiji cha Kaye.

Mihayo amesema kwamba katika vijiji vya Likweri, Ngara na Kahe wanavijiji wamezikimbia nyumba zao na kuishi mafichoni.
“Huku ni kama kulikuwa hakuna Serikali, kila kaya inamiliki mashamba ya mirungi, tena inahudumiwa kwa kuwekewa mbolea na kunyunyiziwa dawa ili iweze kustawi vizuri.
“ Wanavijiji huku walikuwa wanaendesha maisha yao kwa kufanya biashara hii haramu, ikitokea msafara wa kiongozi walikuwa hawaruhusu kwani waliwahi kuwazuia viongozi kuja huku kwa kurushia mawe msafara wao na hivi tunavyoongea Mkuu wa Wilaya walimwambia akithubutu kufika huku watamuua,” amesema Kamanda Mihayo.

Amesema wanahitaji mashine za kukata miti kwani kwa kutumia shoka na mapanga ni vigumu kuweza kufikia lengo kutokana na umri wa miti hiyo ya mirungi.
“Kuna miti yenye miaka mitano au zaidi, mashina ni makubwa sana, hatupati msaada kutoka kwa wananchi kwani wao na viongozi wao wamekimbilia milimani kujificha zaidi tunapishana na watoto wadogo ambao hata uwaulize nini hawakujibu,” amesema Mihayo.
Anasema sasa wanashirikiana na mgambo 100, idadi ambayo anasema bado ni ndogo katika kukabiliana na ukubwa wa kazi.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Same ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Rosemary Senyamule, ameliambia JAMHURI kuwa pamoja na vitisho kutoka kwa wanavijiji, amedhamiria kutokomeza zao hilo haramu.
“Hivi vitisho nimevisikia kuwa nikikanyaga huko wataniua, lakini hayo ni maneno tu hayawezi kunitisha. Na hii imetokea sasa kwa vile tumetimiza wajibu wetu wa kupambana na biashara haramu ambayo walikuwa wameihalalisha,” amesema DC Senyamule.
Anasema kwamba kwa siku tatu wameteketeza ekari 48 za mashamba ya mirungi katika kata tatu za Tahe, Ekonte na Likweni. Watuhumiwa sita, akiwamo mwanamke mmoja, wanashikiliwa wakituhumiwa kushiriki kilimo cha mirungi.
“Zoezi hili [kazi] tumelifanya tangu Juni 14 mpaka Juni 16, kwa sasa tunasimama, tutaendelea tena maana kuna watu wao wanajitapa kwamba wameshindikana hakuna wa kuwafikia wala kuwagusa.
“Tathmini iliyofanyika mwaka jana mwezi Julai, vijiji 45 vilikuwa vinajihusisha na kilimo cha mirungi kama zao la biashara, hii ni hatari. Baada ya zoezi [kazi] hili tumebakiza vijiji 13 tu ambavyo hatujavifikia ili kuweza kutokomeza zao hili,” anasema DC huyo.

1733 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons