ARUSHA

NA MWANDISHI MAALUMU

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), William Mwakilema, ameagiza bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 iandaliwe kwa umakini unaozingatia malengo makuu ya taifa.

Kadhalika, amesisitiza uandaaji wa bajeti hiyo sharti ukidhi dhamira za kitaifa kama zilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Agizo hilo amelitoa mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita alipozungumza na menejimenti ya Tanapa ikiwa ni mara ya kwanza tangu Rais Samia Suluhu amteue kushika nafasi hiyo Januari 8, mwaka huu.

“Hiki ni kikao muhimu sana kwa sababu kinatoa dira na mwelekeo wetu kiutendaji na kimaendeleo kwa kipindi kijacho cha mwaka wa fedha wa 2022/2023. Tumekutana hapa ili tuweze kuainisha vipaumbele vya shirika kwa kuzingatia miongozo ya serikali,” amesema Mwakilema.

Amezitaka hifadhi zinazozalisha mapato yanayozidi matumizi kama vile Ruaha, Mikumi, Nyerere, Mkomazi na Saanane ziongeze jitihada za kutangaza utalii, hasa wa ndani kwa kuwa zinazo fursa hizo na zinafanya vizuri.

“Bajeti hii pia ilenge kufanya aggressive marketing ya kutafuta watalii na kuboresha huduma za utalii. Kwenye hili tunahitaji ubunifu ili kufikia azima ya serikali ya wageni milioni tano na mapato dola bilioni sita ifikapo mwaka 2025,” amesema.

Pia ameelekeza uchambuzi yakinifu kwa kuzingatia bei zilizopo sokoni, masilahi ya watumishi na pia kuboresha makazi ya watumishi wa Tanapa.

Amewapongeza watumishi kwa ubunifu katika kutangaza utalii na kuibua mazao mapya ya utalii kama kutumia magari ya zamani (classic cars) katika Hifadhi ya Taifa Arusha.

Huku ubunifu mwingine ni ule uliofanywa na Hifadhi ya Mkomazi ya kujitangaza kupitia mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam, pia kwa hifadhi za Serengeti, Saanane, Burigi – Chato, Ibanda – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe kwa kufanya matamasha ya vyuo vikuu kuvutia watalii wengi wa ndani.

Mwakilema ameshika wadhifa huo baada ya mtangulizi wake, Dk. Allan Kijazi, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Akiwa kiongozi mkuu wa Tanapa, Kijazi pia alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

By Jamhuri