Serikali ‘yapigwa’


Wizi wa mapato Airport

NA MWANDISHI WETU

Umewahi kujiuliza tofauti ya tozo za maegesho ya magari, iliyopo baina ya wale wanaokwenda Mlimani City pamoja na watumiaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)? Ni ajabu na kweli kwamba tofauti iliyopo ni kama mbingu na ardhi.

Wakati mtumiaji wa maegesho ya magari ndani ya eneo la Mlimani City, bila kujali amekwenda kustarehe ama kujipatia mahitaji muhimu, chini ya dakika 15, hakuna tozo ya maegesho atakayodaiwa, huku wale wanaotumia maegesho ya JNIA hata kama ukitumia dakika moja kumshusha msafiri, dereva atadaiwa Sh 2000.

Hoja kubwa hapa si nani anafanya matumizi ya anasa, isipokuwa jinsi taratibu zinavyojikanganya, mfano pale Mlimani City mtumiaji wa maegesho anapata kadi ya plastiki ambayo huitumia kwenda kulipia, wakati JNIA anaishia kuchukia ‘karatasi’ ambayo husainiwa na mkusanya tozo katika vibanda pale JNIA.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la JAMHURI umebaini kwamba wakati wa alfajiri, ambapo watumiaji wa maegesho hayo ya magari ushuru wa magari wamekuwa hudaiwa tozo bila kupewa stakabadhi za malipo.

 

Pamoja na kulipia maegesho hayo, lango moja la kutokea hubaki wazi ambapo huwa anakuwepo mtu mmoja kwa ajili ya kupokea kadi za malipo na kuwaelekeza madereva kupita katika lango hilo ambalo lipo wazi.

 

JAMHURI, limebaini kwamba wastani wa Sh milioni 5.2, hukusanywa kila siku, hiyo ikiwa na maana kwamba kwa gharama ya Sh 2000, basi magari 2600 huegesha JNIA kwa siku.

 

Kiasi cha magari yanayoegeshwa uwanjani hapo, si hoja kabisa isipokuwa kasoro kadhaa ikiwamo mfumo wa ukusanyaji fedha wa kampuni ya Kenya Airport Parking Services (KAPS) usioiwezesha Serikali kubaini mapato halisi yanayopatikana kutokana na maegesho.

 

Karatasi za maegesho zinazotolewa hutiwa saini au kuandikwa namba kwa kutumia kalamu na anayepokea malipo hivyo kutambuliwa na mtu mwingine ambaye anakuwa katika lango la kutokea.

 

Uchunguzi huo umebaini pamoja na kadi hizo kulipiwa na mteja kupatiwa stakabadhi ya malipo, kadi hizo hazina uwezo wa kufungua lango la kutokea. JAMHURI limebaini kampuni hiyo kuwa na karatasi za kuingilia uwanja wa ndege zenye alama za utambuzi tofauti.

 

Kadi zinazotumika kuingia uwanja wa ndege wa zamani (terminal 1) zinaonyesha mpaka namba ya gari lililoingia eneo la uwanja wakati kadi zinazotumika kuingia uwanja wa ndege wa JNIA hazina namba ya gari.

 

Chanzo cha habari uwanjani hapo kimeliambia JAMHURI, kamera za usalama zilizopo kwenye milango ya kuingia na kutoka uwanjani hapo hazifanyi kazi kutokana na ‘kuhujumiwa’.

 

Chanzo chetu kimesema kutofanya kazi kwa kamera hizo ni kumetokana na kufanyika kwa hujuma na kuziharibu ili zisiweze kufanya kazi hivyo kukamilisha mkakati wa udanganyifu wa tozo uwanjani hapo.

 

Pia ameeleza kuwa suala la mapato kuibiwa na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu ni jambo linalofahamika na kwamba hata wafanyakzai wanaokusanya ushuru kupitia kampuni hiyo ya KAPS ni vibarua tu.

 

“Unajua hili ni jambo la kushangaza, hao wanafanya kazi ya kukusanya tozo hapa uwanja wa ndege ni vibarua tu. Hakuna mwenye ajira. Inakuwaje mtu anayepewa kazi ya kukusanya pesa tena sehemu nyeti, na wateja wengi anakuwa kibarua?” amesema mtoa taarifa.

 

Aidha amebainisha kuwa baadhi ya vibarua hao wanadaiwa kuwa na nasaba na baadhi ya vigogo wa mamlaka ya viwanja vya ndege au mamlaka zinazohusiana na usafiri na usafirishaji wa ndege nchini.

 

“Kuna watu wamewaweka ndugu zao hapo, kwahiyo wanajua kinachoendelea, ni vibarua wanaonufaika kutokana na kuwepo mianya mingi ya kupata pesa nyingi bila kushtukiwa na serikali.

 

“Kuna watu wanaondoka na pesa nyingi kila siku. Pia kupata kazi hapa si rahisi kwani huyu kibarua pesa anayoikusanya kwa mwezi ni zaidi ya mtu aliyeajiriwa. Hawa hawana tofauti na wale jamaa waliokuwa wanawaambia wake zao wainjike ugali jikoni wanakuja na mboga,” amesema.

 

Amesema kuwa kampuni hiyo pamoja na kuendelea kukusanya tozo za maegesho mkataba wake ulimalizika tangu Septemba mwaka jana lakini bado wameendelea kuwepo.

 

“Hii kampuni iliwahi kuhojiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Alihoji kwanini tunakuwa na kampuni kutoka nje ya nchi kuja kutukusanyia pesa, inaonekana ilimkera. Lakini mtandao wake si mdogo, imeendelea kuwepo mpaka hivi unavyoiona. Hapa watu wanakusanya chao huku serikali ikipata kidogo, ndiyo maana hata kamera hazifanyi kazi.

 

“Hapa kulikuwa na Mkurugenzi ambaye aliona wizi umezidi, akaamua kubadili mbinu mapato yakaongezeka. Lakini katika hali ya kushangaza kutokana na kuanza kuwa mwiba kwa mtandao walimfanyia fitina mpaka akaondolewa. Asikwambie mtu hapa pana pesa ila mtandao ndio unasumbua,” amesema mtoa taarifa.

 

JAMHURI limezungumza na Meneja Uendeshaji Viwanja vya Ndege nchini, aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Kadea ambaye amesema suala hilo lipo chini ya Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa JNIA, Paulo Rwegasha.

 

“Hili suala atakayekupa majibu mazuri ni Mkurugenzi wa JNIA, we nenda kamuone atakueleza kila kitu. Mimi sihusiki na uwanja huu, nahusika na viwanja vingine sio huu. Nenda mimi nitampigia simu kwamba unaenda kumuona,” amesema Kadea.

 

Gazeti hili lilifika JNIA na kuzungumza na Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi wa JNIA ambaye alikiri kupokea maagizo kuwa bosi wake hawezi kuzungumzia suala hilo, hivyo JAMHURI liwasiliane na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA).

 

JAMHURI limefanya mahojiano na Kaimu Mkurugenzi TAA, Richard Mayongela ofisini kwake ambaye amesema kwamba ni kweli kampuni hiyo imekuwepo kwa muda mrefu uwanjani hapo na kwamba yeye ameshika nafasi hiyo kwa miezi sita sasa.

 

Mayongela amesema anachofahamu ni kwamba kampuni hiyo imemaliza mkataba wake tangu mwaka jana na tayari ofisi yake ipo kwenye hatua za mwisho kumpata mkandarasi mzawa ambaye atakidhi vigezo vinavyohitajika.

 

“Zabuni ilishatangazwa na tupo kwenye hatua za mwisho. Haya mapungufu unayoyasema nimeyaona na nimeyasikia pia, hivyo nilishasema lazima hatua stahiki zichukuliwe, hatuwezi kuona watu wanafanya wanavyotaka nasi tunawanyamazia. Mkandarasi atakayepatikana atakuwa kwenye viwanja vya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha,” amesema Mayogela.

 

Pia amebainisha kwamba kampuni hiyo itatakiwa kutoa ajira kwa wazawa ili kuweza kupunguza tatizo la ajira. Ameeleza kwamba kamera zote zilizopo kwenye viwanja vya ndege zinatakiwa kufanya kazi kwa muda wote ikiwa ni pamoja na kufanyiwa marekebisho pale zinapokuwa na hitilafu.

 

“Unajua tatizo mimi binafsi siwezi kujua kila kitu kinachoendelea katika viwanja tulivyonavyo, niko na wasaidizi tunasaidiana. Kuhusiana na hili la kamera nilikuwa silifahamu lakini yote uliyosema nitahakikisha nayafuatilia kwa umakini ili kuondokana na huu uzembe na hujuma kama zipo,” amesema Mayongela.

 

Alipoulizwa kuhusiana na mapato yanayopatikana JNIA amesema kwamba, hapo awali kila siku walikuwa wanakusanya kiasi cha Sh milioni 3.8-4 lakini mwaka jana mwezi wa sita, aliyekuwa Mkurugenzi wa JNIA alifanya mabadiliko madogo mapato yakaongezeka mpaka kufikia shilingi million 5- 5.2 kwa siku.

 

Alipoulizwa ni mabadiliko yapi amesema anachofahamu ni kwamba kila kiongozi ana mbinu zake za kufanyakazi hivyo huo ulikuwa ni mkakati wa mkurugenzi huyo ambaye alitaka kuona ufanisi katika tozo zinazotolewa na kutaka kuona iwapo kutakuwa na mabadiliko.

 

“Ni suala la muda kila kitu kitakuwa sawa, haya unayoyasema yatakwisha na huo mtandao unaousema mwisho wake umefika. Mimi binafsi nipo hapa kumsaidia Rais na nchi yangu, sipo tayari kuona mambo yakienda ndivyo sivyo nikayaacha.

“Nimewekwa hapa kutimiza malengo ya TAA hivyo nitahakikisha hizi kero na mambo mengine ninayatatua. JNIA ni uwanja mkubwa, haya mambo hayatakiwi kuwepo kabisa,” amesema Mayongela.

 

JAMHURI limefanya mahojiano na mmoja wa walinzi wa lango la JNIA ambaye amesema kwamba kadi hizo kutofungua ni kutokana na wakusanya tozo kutoziingiza kwenye mashine (kuziscan) kwa ajili ya kuziruhusu kufungua lango.

 

“Unajua hawa jamaa wanapokea pesa tu lakini hawaziingizi katika mfumo. Inabidi tuwaruhusu mpite tu kutokana na kuwa zimesainiwa na wao hivyo tunajua kuwa zimelipiwa,” amesema mlinzi.

 

Alipoulizwa wanajuaje kama kila anayepita hapo anakuwa amelipia, amesema ni vigumu kwa madereva wanaokwenda uwanja wa ndege kushindwa kulipia kutokana na aina ya watu wanaofika eneo hilo.

 

JAMHURI limefanya juhudi za kutafuta ofisi ya KAPS ambapo lilifika kwenye ofisi za Chui Security ambao wamesema kwamba kampuni hiyo ofisi zake zipo Nairobi nchini Kenya.

 

“Labda uende uwanja wa ndege kwenye vibanda vyao, lakini ofisi zao zipo Nairobi na hawana hapa hawana ofisi. KAPS wana hisa kwenye kampuni yetu chui, lakini sisi hatuhusiki nao.

 

“Ingawa wao wanahusiana nasi. Lakini kama unataka kuwasiliana na uongozi wao unaweza kuwatafuta kwenye mtandao na kuwasiliana nao,” amesema mmoja wa viongozi wa Chui Security.

 

Kampuni ya KAPS inajinasibu katika tovuti yake kwamba inafanya kazi ya ukusanyaji mapato katika uwanja wa ndege wa JNIA kwa kufunga mfumo unaohusisha namba za magari yanayoingia katika uwanja huo jambo ambalo ni tofauti na uhalisia.

 

JAMHURI limewalisiliana na KAPS kwa barua pepe wiki mbili zilizopita lakini kampuni hiyo haikujibu maswali yaliyotumwa.

 

Wiki iliyopita, JAMHURI liliwasiliana na kampuni ya KAPS kwa njia ya simu na kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi aliyejitambulisha kwa jina moja la James, ambaye amesema kampuni hiyo ina mwakilishi wake nchini mwenye mamlaka ya kuzungumza chochote kinachohusiana na kampuni.

 

“Naomba uwasiliane na Solomon, yupo hapo Dar es Salaam ndiye mwakilishi wetu huko. Nakupatia mawasiliano yake ili uweze kuzungumza naye, atakusaidia kukupatia ufafanuzi wowote unaoutaka kuhusu kampuni,” amesema James.

 

JAMHURI limewasiliana na Solomon, ambaye hakutaka kutoa ushirikiano wowote.

 

 SOMA GAZETI LOTE LA JAMHURI HAPA

5454 Total Views 9 Views Today
||||| 7 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons