KATIBU MKUU WA CUF, MAALIM SEIF AMPONGEZA RIS MAGUFULI


Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kwa kuiongoza nchi vizuri kwa mwaka uliopita wa 2017.

Seif ametoa pongezi hizo katika salamu zake za mwisho wa mwaka ambapo alisema kwamba, kwa mwaka 2017, Rais Magufuli ameweza kuiongoza nchi vizuri kwa kudhibiti rushwa pamoja na ubadhirifu wa mali za umma.

Akitolea ufafanuzi suala la makinikia, Seif alisema kuwa, Rais Magufuli ameweza kupigania rasilimali za nchi hasi madini ili kuhakikisha wananchi wote wanafaidika, hatua ambayo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema, licha ya kuwa rushwa bado haijaisha, lakini juhudi zilizofanywa haziwezi kubezwa kwani imepungua ikilinganishwa na kipindi cha serikali ya awamu ya nne.

Pia, aliwataka wanasiasa kutokuona shida kusifia mazuri ambayo yamefanywa na serikali wakati wakifanya tathmini ya mwaka 2017. Seif alieleza namna serikali ilivyowafikisha mahakamani vigogo wa rushwa, kurejesha nidhamu ya fedha lakini pia kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kwa kuwalipa watumishi hewa.

Mbali na hayo, Seif pia alizungumzia changamoto za mwaka 2017 na kusema kuwa, uhuru wa kufanya siasa nchini umebanwa kufuatia kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa pamoja na maandamano.

Lakini akielezea suala la Zanzibar, alisema, ubaguzi katika visiwa hivyo bado ni changamoto kubwa kwani hata ajira zinatolewa kwa kufuata mrengo wa kisiasa badala ya utaalamu wa mtu.