Kesi iliyofunguliwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Warioba, dhidi ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), imeahirishwa hadi Februari 11, mwakani.

Jaji Warioba ambaye pia amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anapinga kufukuzwa katika nyumba Na. 501/13 iliyopo Barabara ya Ghuba, Oysterbay jijini Dar es Salaam kutokana na mgogoro wa kodi ya pango.

Kesi hiyo ilitajwa Novemba 15, mwaka huu mbele ya Jaji Elvin Mgeta, lakini upande wa utetezi uliomba iahirishwe hadi mwakani ambapo Jaji Warioba ataanza kutoa ushahidi.

Jaji Warioba kupitia Kampuni yake ya Nyalali Warioba & Mahalu Law Associates anapinga madai ya TBA dhidi ya kampuni hiyo ya uwakili ya Sh milioni 54.7. Taarifa kutoka ndani ya kampuni hiyo zinasema hadaiwi kiasi chochote cha fedha, kwani mara ya mwisho malipo ameyafanya ya mwaka mzima – Desemba 2017 hadi Desemba 2018.

Mapema mwaka huu, JAMHURI liliandika taarifa ya kufukuzwa kwa Jaji Warioba kwenye nyumba aliyopanga kwa miaka mingi.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, aliiandikia barua Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart akiiagiza itumie nguvu kuiondoa Kampuni ya Nyalali Warioba & Mahalu Law Associates kwenye nyumba hiyo.

Barua ya Mwakalinga ya Machi 19, mwaka huu ambayo JAMHURI limepata nakala yake, Mtendaji Mkuu huyo anawaagiza Yono kwa kusema: “Kwa barua hii unatakiwa kuandaa utaratibu wa kumuondoa kwa nguvu mpangaji huyu, ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha Polisi pamoja na taarifa kwa Serikali za Mitaa, kwani nyumba hiyo inahitajika haraka iwezekanavyo kwa ajili ya matumizi ya Serikali.”

Chanzo cha mgogoro kwa pande hizo mbili ni uamuzi wa TBA wa kupandisha kodi kutoka Sh 700,000  hadi Sh milioni 3.5; kiwango ambacho kampuni hiyo inasema ni kikubwa mno. Kwa kuheshimu mkataba wa awali usio na mgogoro, taarifa zinasema kampuni hiyo imeendelea kulipa kodi zote kuanzia mwaka 2001 hadi Desemba, mwaka huu.

Kutokana na mvutano huo, Kampuni ya Nyalali Warioba & Mahalu Law Associates ilifungua shauri katika Mahakama ya Ardhi ikipinga ongezeko hilo la kodi ya pango.

Wakati shauri la msingi Na. 91/2014 likiendelea mahakamani, TBA walianza taratibu za kumwondoa mpangaji katika nyumba hiyo, na ndipo alipofungua kesi Na. 136/2015  kupinga hatua hiyo.

Desemba 30, 2015 Mahakama ya Ardhi chini ya Jaji Winfrida Korosso, ilitoa uamuzi wa kuzuia mpango wowote wa kuibugudhi au kuiondoa kampuni hiyo kwenye nyumba husika hadi kesi ya msingi itakapotolewa uamuzi.

Kesi ya msingi imepangwa kuendelea katika Mahakama ya Ardhi mbele ya Jaji Edson Mkasimangwa Mei 28, mwaka huu. Wakili wa upande wa mlalamikaji ni Michael Ngalo.

Hata hivyo, licha ya kuwapo hukumu ya mahakama ya kutoiondoa Kampuni ya Nyalali Warioba & Mahalu Law Associates, TBA imeendelea kushikilia msimamo kwa kusema: “…Mpangaji alipewa notisi ya kusitisha mkataba na kukabidhi nyumba tangu Desemba 2015, jambo ambalo hajatekeleza hadi leo [Machi 19, 2018]. Pamoja na kutotekeleza agizo hilo amelimbikiza kiasi cha Sh 54,700,000.00 hadi Februari 2018.”

Hata hivyo, taarifa kutoka Kampuni ya Nyalali Warioba & Mahalu Law Associates, zinasema kodi zote za pango kwa muda huo ambazo ni Sh milioni 1.1 kwa mwezi zimekuwa zikilipwa kama kawaida, na kwamba hadi sasa haidaiwi senti yoyote. Fedha hizo zimekuwa zikiingizwa kwenye akaunti ya TBA kama ilivyokuwa kwenye mkataba baina ya pande hizo mbili.

Wakati TBA wakiitaka Yono iiondoe Kampuni ya Nyalali Warioba & Mahalu Law Associates kwa nguvu, kuna taarifa kuwa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni umesita kutoa askari wa kusimamia kazi hiyo baada ya kubaini upungufu wa kisheria.

Kutoka Polisi Oysterbay, JAMHURI limeambiwa kuwa Yono walifika kuomba askari kwenda kumwondoa Jaji Warioba kwenye ofisi hizo, lakini ilishindikana baada ya kampuni hiyo ya udalali kukosa barua ya mahakama ya kuhalalisha hatua hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne, alizungumza na JAMHURI kuhusu sakata hili na kusema hakumbuki kuwapo kwa tukio la kuondolewa Jaji Warioba katika nyumba aliyopanga, lakini akasema hiyo haina maana halipo.

“Tunapokea matukio mengi ya aina hiyo, lakini ukweli ni kuwa tunasimamia sheria, hatuwezi kumwondoa mtu hivi hivi bila maelekezo ya mamlaka za kisheria. Inawezekana hilo jambo lililetwa ofisini na likaishia kwa askari wanasheria, kwa sababu nimehakikisha tunafuata sheria.

“Waulize hao Yono walikuja na barua ya mahakama? Kama hawakuja nayo, basi ujue hilo shauri linaweza likawa limeishia kwa askari wanasheria kwa sababu hatutaki kumwonea mtu au kufanya kazi kwa shinikizo.

“Mtu anaweza kuja kuomba askari ili wasimamie kumwondoa mtu fulani mahali fulani, sasa kwa kawaida ya kazi zetu lazima tufuate sheria. Kitu tunachokifanya cha kwanza ni ku – cross check (kuhakikisha) na mahakama kama kweli kuna amri hiyo. Kama haipo hatuwezi kupeleka askari,” amesema na kuongeza:

“Polisi ni wasimamizi wa sheria, hilo naomba ulijue – tunapokea maelekezo ya kisheria kwa documents [nyaraka] za kimahakama – hauwezi kuamka tu na uamuzi wako. Nikiletewa nitauliza, amri imetolewa na chombo gani cha kisheria? Na katika hili ni mahakama.

“Atakuwa polisi wa ajabu kutekeleza jambo ambalo halipo kwenye miongozo ya kisheria. Yono wakuonyeshe ‘order’ ya mahakama kama wanayo uje nayo maana isionekane tumekataa maelekezo ambayo ni halali kisheria.

“Tunafuata mfumo wa kisheria ili kutenda haki kwa pande zote kwa mujibu wa sheria. Mimi sina kumbukumbu na hili unalonieleza, na kama walikuja bila ‘order’ yawezekana waliishia kwa wanasheria wetu.”

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart, Stanley Kevela, na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Scholastika Kevela, wote wamekiri kupokea barua ya TBA ya kumwondoa Jaji Warioba kwenye nyumba husika.

By Jamhuri