Moja ya faida kubwa ambayo huwavutia wengi kuacha kufanya biashara kama mtu binafsi na kuamua kufanya biashara kwa kutumia kampuni ni hii ya kuwa kampuni na mmiliki ni vitu viwili tofauti, hivyo kosa la kampuni halimhusu mmiliki na kosa la mmiliki haliihusu kampuni. Maana yake hata ukikopa kwa kutumia kampuni na ukashindwa kulipa, mali zako binafsi haziguswi isipokuwa za kampuni tu. Kadhalika makosa mengine yatahesabika kutendwa na kampuni na itashtakiwa kampuni na si wewe mmiliki. Hili huwavutia wengi, yumkini tupate funzo kutoka kesi za Sumry High Class na kesi ya Manji.  Tukianza na hii ya Sumry.   

Katika Mahakama Kuu ya Biashara Kanda ya Dar es Salaam mwaka 2012 kulifunguliwa maombi ya biashara (Misc. Commercial Cause No. 20/2012) kati ya MUSSA SHAIBU MSANGI vs SUMRY HIGH CLASS LIMITED. Mlalamikaji/mleta maombi  Mussa Shaibu Msangi alikuwa akiiomba mahakama kumkamata na kumfunga jela mmiliki/mkurugenzi  Hamoud Muhammed Sumry kwa kushindwa kumlipa deni lake linalofikia Sh. 179,379,980 lililolimbikizwa kwa zaidi ya mwaka mmoja japokuwa mahakama ilikwisha kuamua alipwe.

Katika utetezi wake Sumry alisema kuwa inayodaiwa ni kampuni, hivyo ni kosa kisheria kutaka kumpeleka jela kwa kutolipa, kwa kuwa kisheria kuna tofauti kati ya kampuni na mmiliki wake, hivyo kosa la kampuni ni kampuni ihusike, na kosa la mmiliki ni mmiliki ahusike.

Katika hukumu yake Jaji Songoro, alisema kuwa ni lazima Hamoud Muhammad Sumry akiwa mmiliki na mkurugenzi alipe deni hilo hata kama mkataba ulikuwa kati ya Mussa Shaibu na kampuni, kwa sababu akiwa mkurugenzi ameshindwa na inaonekana anaifanya kampuni ikwepe kumlipa mlalamikaji kwa zaidi ya mwaka.

Mahakama ikasema kuwa pale inapoonekana kampuni inakwepa kutekeleza majukumu yake ya kisheria kama kumlipa mlalamikaji, basi ukuta unaotenganisha kampuni na mmiliki unaondolewa na hapo wamiliki wanawajibika moja kwa moja kwa makosa ya kampuni.

Hivyo ndugu Hamoud Muhammad Sumry akapewa siku 30 kuwa amemlipa Mussa Shaibu vinginevyo afungwe jela.

Mwaka 2002 Yusuf Manji alikata rufaa katika CIVIL APPEAL No. 78/2002 kati ya Yusuf Manji dhidi ya Edward Masanja na Abadallah Juma. Kupitia Wakili wake, Mpaya Kamara, alikuwa akiilalamikia Mahakama Kuu kwa kumuamuru awalipe ‘overtime’, pesa ya usafiri na posho ya pango Edward Masanja na Abdallah ambao walikuwa walinzi kwenye Kampuni yake ya Metro Investment Limited. Hoja mojawapo kati ya hoja alizokuwa nazo ni kuwa kwa nini Mahakama Kuu imtake alipe yeye wakati walinzi wana mkataba na kampuni, na kwa mujibu wa sheria yeye na kampuni ni vitu viwili tofauti.

Mahakama ya Rufaa chini ya majaji watatu ilisema kwamba,  kwa kuwa kumbukumbu zinaonyesha kuwa Manji amekuwa akificha mali za kampuni ili zisiweze kukamatwa ili kuwalipa walalamikaji, ni sahihi akamatwe yeye ili kulipa, na akishindwa aende jela hata kama mkataba ulikuwa kati ya walinzi na kampuni.

Katika kesi hizi mbili sisi wajasiriamali tunaofungua kampuni tunajifunza kuwa kanuni ya kisheria ya kumtenganisha mmiliki wa kampuni na kampuni haiwezi kutumika kuvunja sheria, ukiamini kuwa hautaguswa kwa kuwa kampuni ndiyo imetenda. Kanuni hii ina ukomo na mipaka yake, na moja ya mpaka ni pale kampuni inapotumika kuvunja au kukwepa taratibu za kisheria. Kwa hivyo ni muhimu kulijua hili na ukajihadhari.

By Jamhuri