Kichaa cha mbwa chatesa K’njaro

Mamlaka za Serikali zimetoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini dhidi ya ugonjwa wa kichaa
cha mbwa wilayani Moshi na maeneo mengine mkoani Kilimanjaro.
Februari, mwaka huu, watu watatu walifariki dunia wilayani Moshi, chanzo kikielezwa kuwa ni
kung’atwa na mbwa wenye kichaa.
Watu 64 wameripotiwa kujeruhiwa na mbwa wenye ugonjwa huo katika vijiji vya TPC, Mawala,
Oria, Mabogini na Ngasini.
Waliofariki dunia walitajwa kuwa ni Lulu Zephania (4), Grace Benny (5), mwanafunzi wa shule
ya awali katika Shule ya Msingi Mawala, na Naomi Mmanga (34) – wote wakazi wa Kijiji cha
Mawala wilayani Moshi.
Daktari wa Mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Walter Marandu, amesema
operesheni ya kuwaangamiza mbwa wanaozurura inaendelea katika maeneo mbalimbali
yaliyoripotiwa kukumbwa na ugonjwa huo.
Hadi wiki iliyopita mbwa zaidi ya 100 wanaodaiwa kuwa na kichaa waliuawa kwenye operesheni
hiyo katika vijiji vya Mawala, Mikocheni, Msarikie na Mtakuja.
Dk. Marandu anasema watu 64 waling’atwa na mbwa hao kuanzia Januari hadi Machi, mwaka
huu na kusema kwamba tatizo hilo ni kubwa.
Halmashauri imeendelea kuwaelimisha wananchi namna ya kukabiliana na mbwa hao kwa
kutumia gari la matangazo.
“Timu yetu ya wataalamu ipo vijiji pamoja na gari la matangazo, tunatoa matangazo sehemu
mbalimbali – makanisani na misikitini – juu ya kuwepo na mbwa wenye kichaa cha mbwa na
namna ya wanachi kuchukua hatua,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mawala, David Laizer, ameliambia JAMHURI kuwa tayari wameua
mbwa 19 katika kijiji hicho tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila, amesema chanjo ya kuzuia
ugonjwa huo inaendelea kutolewa.
“Tunawaomba wenye mbwa wao kuhakikisha kuwa wanapatiwa chanjo zinazostahili kuanzia
chanjo ya kichaa cha mbwa, na magonjwa mengine ili kuepusha watu wasiendelee kupata
madhara,” amesema.

Moshi Mjini hali tete
Wakati hali ikiwa hivyo katika Halmshauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, tatizo hilo pia limeripotiwa
mjini Moshi ambako watu 13 wamelazwa katika Hospital Teule ya St. Joseph, Hospitali ya
Rufaa ya KCMC na Kituo cha Afya cha Pasua baada ya kung’atwa na mbwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, amethitisha kuwapo
kwa tishio la mbwa wenye ugonjwa huo.
Amesema watu zaidi y 90 wameripotiwa kung’atwa na mbwa katika Manispaa hiyo kuanzia
Januari hadi Machi, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Hospitali Teule imepokea wagonjwa wanne wakati, KCMC
inayoendeshwa na Shirika la Msamaria Mwema (GSF) imepokea wagonjwa saba na Kituo cha
Afya cha Pasua kinao wagonjwa wawili.

“Tumeshaanza kutoa matangazo kwa wananchi na tumewataka kutoa taarifa endapo
watawaona mbwa wakirandaranda mitaani na pia tumetoa maelekezo kwa wamiliki wa mbwa
kuchukua tahadhari,” amesema.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Moshi, Dk. Soka Mwakapalala, amesema baadhi ya wagonjwa
waliolazwa katika Hospitali za KCMC na Mtakatifu Joseph hali zao si nzuri.
“Asilimia 99 ya wagonjwa waliong’atwa na mbwa hufariki dunia hivyo kunahitajika tahadhari
kubwa sana na tunawaomba wananchi pindi wanaposhambuliwa na mbwa ni muhimu kwenda
haraka kupata matibabu ndani ya saa 24,” amesema.
Hadi wiki iliyopita, Manispaa ya Moshi ilikuwa imeua mbwa 700 kwa kuwapiga risasi, na mbwa
709 wakipatiwa chanjo.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakapalala, kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 watu zaidi ya 1,000
waling’atwa na mbwa. Mwaka 2016 waling’atwa watu 434; mwaka 2017 watu 564 na katika
kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu ni watu 91.