Kiingereza chapigiwa debe

Imeelezwa kuwa msingi mzuri wa lugha ya Kiingereza kwa watoto wanaosoma shule za awali zinazotumia lugha hiyo ni moja ya sababu za wanafunzi wengi wanaotoka katika shule hizo kufanya vema zaidi kitaaluma kwenye madarasa ya juu.

Wakizungumza mjini hapa, baadhi ya wazazi wamesema kwa kuwa Kiingereza ndiyo lugha rasmi ya kufundishia masomo yote isipokuwa Kiswahili pindi mwanafunzi anapoingia sekondari, hivyo msingi mzuri wa lugha hiyo unamwezesha mwanafunzi kuelewa haraka masomo ya sekondari.

“Hebu fikiria, mtoto tangu darasa la awali anafundishwa Kiswahili masomo yote isipokuwa Kiingereza, halafu ghafla akienda sekondari anakutana na Kiingereza katika masomo yote isipokuwa Kiswahili. Je, unadhani ataweza kumudu vema?”  alihoji Athumani Idd, mmoja wa wazazi na kuongeza: “Hiyo ndiyo sababu wanafunzi wengi kutoka ‘English Medium’ kufanya vizuri zaidi wanapoingia sekondari kulinganisha na wale waliosoma shule za kawaida.” 

Mzazi mwingine, Helena Mussa, anaona kuwa sababu si tu msingi wa Kiingereza kuwa mzuri bali pia shule hizo  kuwa makini zaidi katika ufundishaji kwa lengo la kufanya vizuri kwenye mitihani na kuvutia wateja kutokana na kuendeshwa kibiashara. 

Aidha, wametaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na shule hizo kusheheni vifaa changamshi kwa ukuaji na ujengaji ubonago wa mtoto katika umri mdogo kama vile michoro ya kujifunzia na kufundishia darasani na uwepo wa michezo mbalimbali wakati wa mapumziko, hali ambayo ni tofauti kwenye shule za serikali.

Kutokana na hali hiyo, wengi wa wazazi wameiomba serikali kuangalia upya mfumo wa utoaji elimu katika shule zake kuanzia madarasa ya awali ili kama mtoto anafundishwa Kiswahili aendelee nacho hadi elimu ya juu, vinginevyo wanafunzi wote wawe wanaanza masomo yao kwa lugha ya Kiingereza kuanzia madarasa ya awali.  

Ofisa Elimu (Elimu ya Watu Wazima) Mkoa wa Singida, Suleiman Nkondo, anakubaliana na dhana hiyo ingawa anasema kuna sababu nyingine za ziada kama vile kujituma katika ufundishaji na baadhi ya wamiliki wa shule hizo kutumia njia za ‘ujanja ujanja’ kwa nia ya kutaka shule zao zionekane bora zaidi.

Nao wataalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wamesema Kiingereza ni nyenzo muhimu ya mawasiliano katika elimu hasa katika ngazi ya sekondari hivyo kuijua kunaweza kukawa na mchango mkubwa katika kujifunza ingawa wanasisitiza ufaulu hutegemea vitu vingi.