Ukijifunza, fundisha


 
Kufahamu mambo bila kuifundisha familia yako ni kuiacha familia hiyo iangamie. Kufahamu mambo bila kuifundisha jamii yako ni kuiacha jamii hiyo ipotee. Kufahamu mambo bila kulifundisha taifa lako, ni kuliacha taifa hilo lipotee. Ukijifunza, fundisha. Ukifahamu mambo, jitahidi na watu wanaokuzunguka wafahamu mambo hayo.
Ili kutengeneza taifa la watu walioendelea, ni vema tukawapa watu maarifa tuliyonayo, hii itasaidia watu kujikomboa katika mambo mbalimbali hasa ujinga na umaskini.
Hakuna sifa yoyote utakayoipata endapo unajua kitu fulani na jamii inayokuzunguka inapitia majanga ambayo unaweza kuyatatua kwa muda mfupi lakini wewe umeficha kile unachokijua.
Unapowafundisha watu wengine mambo unayoyafahamu, unapata nafasi ya kukua kiakili zaidi na unajenga uwezo wa kujua lipi linafanya kazi na lipi halifanyi kazi. Unapowafundisha watu wengine kile unachokijua, unawafungulia fursa mpya ambazo zinaweza kuwasaidia kutengeneza kipato.
Mshumaa haupotezi chochote kwa kuwasha mishumaa mingine bali unaongeza mwanga katika chumba ulichomo. Wewe pia haupotezi chochote kwa kuwafundisha watu kile unachokifahamu bali unaongeza na kukuza idadi ya watu wengi wenye maarifa. Kama unavyofahamu, pasipo na maarifa watu huangamia.
Imani yangu ni kwamba kila mtu kuna mambo fulani anayafahamu ambayo yanaweza kuisaidia jamii inayomzunguka, taifa na dunia kwa ujumla. Elimu yako, maarifa yako na ujuzi wako havitafaa kitu kama ukiendelea kubaki navyo wewe mwenyewe.
Jitoe na kuwafundisha watu kile unachokijua. Ukiwa tayari kutoa kile unachokijua ni rahisi sana kupata wafuasi wa kile unachokifanya. Kila mtu anahitaji kufahamu kuwa mambo anayoyafahamu kuna watu mahali fulani wanahitaji kujua mambo hayo ili yawatoe hatua moja na kuwapeleka hatua nyingine.
Unajua mambo yanayohusu biashara, wafundishe wengine. Fundisha watu namna ya kutafuta soko, fundisha watu namna ya kuona fursa, fundisha watu namna bora ya kudhibiti mzunguko wao wa fedha, fundisha watu namna ya kupata wateja. Haya ni machache tu, orodha ya kujifunza na kufundisha ni ndefu.
Kama wewe ni mtaalamu wa mambo ya kilimo, wafundishe watu mbinu bora za kilimo, washauri ni mbolea gani inafaa kwa mazao yao. Tunao wakulima wengi sana ambao wanalima kiholela, tatizo kubwa ni kwamba tunao wataalamu wa kilimo na wengine wasomi katika fani za kilimo lakini elimu na taaluma hiyo wameificha na kuikalia kama yule mtumwa aliyeficha talanta moja.
Nilipokuwa ninasoma kitabu cha Dk. Reginald Mengi kiitwacho I Can, I Must, I Will, kuna taarifa niliisoma ilinishtua kidogo, aliandika hivi: “Takwimu zinaonyesha kwamba bonde la Mto Ruvu linaweza kuzalisha chakula cha kulisha nchi nyingine za Afrika Mashariki, eneo la Kilombero linaweza kuzalisha mchele wa kulisha Afrika ya Kati yote, Wilaya ya Kyela inaweza kuzalisha mchele wa kulisha Afrika Magharibi yote, bonde la Mto Rufiji linaweza kuzalisha chakula cha kulisha Afrika ya Kaskazini ukijumuisha na nchi za Sudan, Ethiopia na Somalia, pia maeneo ya Wami na Arusha Chini yanaweza kuzalisha mchele wa kutosha unaoweza kuilisha Afrika Kusini yote. Kwa namna nyingine tunaweza kusema, Tanzania inayo ardhi yenye rutuba na maji ya kutosha yanayoiwezesha kuzalisha chakula cha kutosha kuilisha Afrika nzima.”
Takwimu kama hizo alizoziandika Dk. Mengi zinakwama kutokana na watu kufahamu mambo ya kilimo lakini hawapo tayari kutoa utaalamu wao kwa wengine ili taifa liendelee.
Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa alijua mambo mengi lakini hakupenda kubaki nayo. Mambo aliyoyafahamu aliyafundisha kwa njia ya hotuba na akaenda mbali zaidi na kuyaweka katika maandishi ambayo hadi leo yanaishi. Ukijifunza, wafundishe na wengine.
Patrick Bitature ni mfanyabiashara mkubwa kutoka nchini Uganda, pia ni mkurugenzi wa makampuni ya Simba. Bitature amekuwa akiwafundisha watu mambo mengi kuhusu biashara na mambo yanayohusu fedha. Huyu ni mfano wa kuigwa kwetu, anafahamu mambo mengi kuhusu biashara na anawafundisha wengine. Mfuatilie katika mtandao wa Youtube, ninaamini kuna mambo mengi utapata na kujifunza kutoka kwake.
Siku hizi dunia imebadilika na kuwa kama kijiji. Unaweza kuwafundisha watu wengi mambo unayoyafahamu kwa muda mfupi na kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha yao. Tumia intaneti kuwafundisha watu kile unachokifahamu. Hilo linaweza kukufanya uonekane mtaalamu wa jambo hilo, hivyo fursa zaidi zinaweza kufungukia upande wako.

Itaendelea

By Jamhuri