Kila upande hautaki kusikia haya!

Leo naandika Sitanii ngumu. Ni ngumu kwa misingi kwamba kila atakayesoma makala hii ya leo, kuna mambo ataburudika hadi atamani kunipigia simu ya pongezi, lakini pia, kuna mambo atasoma kama si mvumilivu, atatamani kunipigia simu kunitukana. Nitatahakiki suala hili la madini kwa mawanda mapana. Hakika sitatasiliti, bali nitatashtiti.
Sitanii, msamiati uliotangulia katika aya ya kwanza nausitisha kidogo, kuepusha usisome makala hii ukiwa umeshika kamusi, ila si mchezo, kwamba Kiswahili kina utajiri wa maneno, si haba. Nashauri kila neno ulilopata ugumu kulielewa, gusa Kamusi angalau mara moja ndani ya mwezi huu, nawe uongeze neno jipya katika msamiati ulionao.

Leo (Jumapili), nimetokea kanisani, ndipo naandika makala hii. Masomo na Injili ya leo vililenga kutiisha waamini, kwa kuwafunda juu ya neno utii. Paroko wa Parokia yetu ya Roho Mtakatifu Kitunda, Dar es Salaam, Fr. James Mweyunge, ametoa mahubiri yaliyogusa wengi, juu ya utii.
Amegusa utii na uvumilivu ndani ya familia, kanisani na mamlaka ya nchi. Katika mahubiri hayo, kila mara alisisitiza neno ukweli. Dhana ya kusema ukweli na utii kwa mamlaka ya nchi, ndivyo vimenisukuma kuandika makala hii yenye pande mbili.

Sitanii, wiki iliyopita niliandika juu ya sheria mbili zilizotungwa kwa hati ya dharura na nimefafanua kwa nini udharura ule ulistahili. Miswada iliyopitishwa na Bunge ni Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms)] Bill, 2017].
Muswada wa pili ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty)] Bill, 2017] na wa tatu ni Muswada wa Marekebisho ya Sheria, 2017. Nilizungumzia kwa kina miswada miwili, na nikaahidi kuendeleza mada hii leo kwa ajili ya muswada huu wa tatu.
Sitanii, naanza na upande ambao ni mzuri kwa Serikali na Watanzania, ambao ni marekebisho ya Sheria Mbalimbali Mwaka 2017. Kimsingi sheria hii, ni nzuri kwa sisi Watanzania. Nilicho na uhakika nacho, hakuna mwekezaji wa madini hata mmoja anayeweza kuipenda sheria hii ilivyokaa.

Nafahamu si kila Mtanzania ni Mwanasheria na si kila Mwanasheria Mtanzania amepata fursa ya kuipitia na kuisoma sheria hii. Nimepata fursa ya kuisoma, hivyo niruhusu msomaji nikupitishe japo kwa ufupi juu ya sheria hii inaanzisha nini na ikiwezekana nieleze ina faida gani kwa nchi.
Nikiri sitagusa kifungu kwa kifungu, maana ukurasa huu ni mdogo na marekebisho ni mengi. Kifungu cha 21 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kimerekebishwa kwa kuanzisha Tume ya Madini badala ya Bodi. Marekebisho haya, yameipa nguvu kubwa sekta ya madini. Nchi ya Ghana ilifanya hivi na baada ya marekebisho haya, ukifika Accra, Ghana unaona matunda ya madini.
Tume inakuwa na mawanda mapana katika uamuzi kuliko Bodi. Tume ni chombo cha kiuamuzi na usimamizi, bali Bodi ambayo ni chombo cha usimamizi na ushauri. Tume inakuwa na fursa ya kutunga Kanuni za uendeshaji, lakini Bodi inategemea Kanuni zilizotungwa na Waziri. Nasema uamuzi huu ni sahihi, na ulichelewa. Hongera Serikali kwa kuufanya.

Sitanii, sitazungumzia masuala kama kuzitaka kampuni za madini kusajiliwa na kuwa na akaunti hapa nchini, lakini kubwa nigusie kuwa huduma na utaalam wa Watanzania katika migodi au sekta ya uziduaji sasa utalazimika kutumika kisheria na haitabaki kuwa hiyari kama mwanzo. Ni jambo zuri mno.
Serikali imeniburudisha katika marekebisho iliyofanya kwenye Kifungu cha 10 (1). Kwamba chini ya sheria hii mpya sasa, katika kila mgodi Serikali itapata asilimia 16 ya hisa bila kuzilipia. Wapo wanaoweza kupinga hili, lakini wakumbuke kuwa mwekezaji anakuja na mtaji, Watanzania kupitia Serikali wanamiliki madini, hivyo mtu anaweza kusema hata hiyo asilimia 16 ni ndogo. Madini ni yetu.
Kifungu cha 10(2) kimeleta dhana mpya. Kwamba mwekezaji katika migodi anayetaka kusamehewa kodi, anaweza kusamehewa, lakini hiyo asilimia ya kodi anayosamehewa inapigiwa hesabu na kuingizwa katika hisa. Utaratibu huu wa hisa zinazotokana na misamaha ya kodi unairuhusu Serikali kumiliki hadi asilimia 50.

Chini ya sheria hii anateuliwa Naibu Mwanasheria Mkuu (Madini), ambaye muda wote atakuwa na kazi ya kuangalia mikataba. Kimsingi huu ni uamuzi mzuri, mzito na wa maana kweli kwa taifa letu. Sheria hii inaanzisha Hifadhi ya Taifa ya Madini na Vito.
Kifungu cha 87 cha Sheria ya Madini 2010, kama ilivyorekebishwa mwaka 2017 sasa kinatoa wajibu wa kutosema uongo. Wakati wa kutoa mrahaba (mrabaha), kampuni inapaswa kuhakikisha mrahaba unaotolewa unalingana na bei halisi ya soko.

Sitanii, sheria hii inaipa mamlaka Serikali ikibaini kuwa bei iliyotumika kukokotoa mrahaba ni ndogo, basi Serikali yenyewe inayanunua madini hayo kwa bei iliyotangazwa na mwekezaji kuwa ndiyo ya kuuzia. Hii maana yake ni kuwa kuanzia sasa mchezo wa kushusha bei ya madini kulipa mrahaba kidogo unafikia ukomo.
Naendelea kueleza yale mazuri kwetu. Kuanzia sasa chini ya Kifungu cha 100A(3) kampuni zinazochimba madini kila zikipata madini zitapaswa kukaa nayo si kwa zaidi ya siku 5 mgodini. Zinapaswa kuwa zimeyapeleka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Madini na Vito katika muda huo.
Kifungu cha 100C(2) kinamtaka mwekezaji kusafirisha madini kutoka mgodini hadi kwenye Hifadhi ya Taifa kwa kutumia usafiri ulioidhinishwa na Serikali na si bora liende. Pia Kifungu Kidogo cha 100C(3) kinasema hakuna leseni itakayotolewa kusafirisha nje ya nchi madini ghafi au makinikia.

Kifungu cha 100E kinazuia mkataba wowote kuyeyusha mamlaka ya nchi katika kuendesha kesi yoyote iwapo kumetokea kutoelewana kati ya Serikali na Mwekezaji, kesi zote zitaendeshwa katika mahakama za ndani na si nje ya nchi. Pia mwekezaji atalazimika kutoa ripoti kila mwaka kuonyesha amechangia nini katika uchumi na ametumiaje bidhaa za ndani na Watanzania.
Sitanii, yapo mambo mengi mazuri ndani ya sheria hii ambayo ningeweza kuandika nikajaza gazeti zima. La msingi niseme nimefurahishwa na hatua ya Serikali kufumua mikataba hii ya madini na hakika nia hii kama nilivyosema katika makala ya wiki iliyopita, milele Rais Magufuli historia haitamsahau.
Nimemaliza sehemu tamu kwa Watanzania. Kama ni jipu, ilikuwa nalikamua kwa mkono wa kushoto, sasa naanza kulikamua kwa mkono wa kulia. Uko tayari? Naanza. Haya najua kuna ambao hawatayapenda, lakini ni vyema niyaseme kwa maana nchi yetu ijue kuwa yapo.

Nikianza na sheria iliyorekebishwa, Kifungu cha 28 cha Sheria ya Madini, sasa kimerekebishwa na kuwa kitanzi kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari. Kifungu hiki kinazuia utoaji wa taarifa zinazohusiana na mikataba ya madini bila ridhaa ya mwekezaji.
Kinasema mtu yeyote atayaketoa taarifa kwa mtu asiyehusika, na au kama taarifa hizo zimetolewa na wabia au vikundi vya kijamii (NGOs), mhusika atatozwa faini isiyopungua Sh milioni 200 au kifungo jela kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja. Ina maana ukomo wa faini Mungu ndiye anajuaye.
Ikiwa taarifa hizo zimetolewa na mtu wa kisheria (a body corporate), hii ina maana pia ya vyombo vya habari, basi mtu huyo (chombo) atapigwa faini isiyopungua Sh bilioni moja. Ukomo wa adhabu hii, Mungu ndiye anayeujua. Ingawa kwa kutumia Sheria ya Huduma za Habari (2016) Kifungu cha 7(2), habari za mikataba hazijawekewa kinga.

Sitanii, napenda kuamini hiki kifungu kimechomekwa. Tumepigwa mno kwa mikataba hii kuwa siri. Sitaki kuamini kuwa hata Rais Magufuli ameridhia usiri anaoupinga uliotufikisha hapa uendelee. Hapana shaka atapata fursa, ikibidi marekebisho yafanyike kuondoa dhana hii ya usiri nchi ipate habari za moto moto.
Jambo la pili ni hii mikataba ya madini ambayo ipo tayari. Mikataba hii mingi imejengwa katika msingi wa Mikataba ya Uendelezaji wa Madini (Mineral Development Agreements –MDAs). Mikataba hii ina kitu kinaitwa Stabilization Clause (Kifungu cha Utangamano), kifungu hiki hakiruhusu mabadiliko katika mikataba na kinayeyusha mamlaka ya mfumo wetu wa sheria.
Ni kifungu hiki hiki kinazipa kampuni za wawekezaji haki ya kufungua kesi nje ya nchi ikiwa zitapata mgogoro na Serikali. Chini ya mikataba hii, mwekezaji anakuwa na haki zote juu ya madini na eneo analomiliki kimkataba kuchimba madini. Ndipo kuna wasiwasi kuwa hata madini yaliyoko ardhini anaweza kuyaweka rehani, akachukua mikopo mikubwa.

Aina nyingine ya mikataba ya madini ni Mikataba ya Uzalishaji (Production Sharing Agreements – PSAs). Chini ya mikataba ya aina hii, Serikali inaendelea kumiliki madini na mwekezaji anakuwa mkandarasi, hivyo analipwa kwa alichozalisha, sawa na mkandarasi wa barabara au ujenzi wa bomba la mafuta. Aina hii ya mikataba ndiyo iliyopo kwenye gesi na mafuta hapa kwetu.
Sitanii, ukweli ni sawa na ncha ya mkuki. Ukiambiwa usiuupige konzi ukapuuza “ekilakugambila olakishanga omwikoti za Kagoza.” Aina ya mikataba tuliyonayo ya MDAs, ni kwamba tunalo. Sheria za Kimataifa hazitambuli lolote iwapo umebadili sheria za ndani baada ya kuingia mkataba.
Mwaka 1923 ilihitimishwa kesi ya kihistoria kati ya Serikali ya Uingereza na nchi ya Costa Rica. Kesi hii maarufu kama Tinoco Arbitration Case, katika hili la madini inatuhusu. Unaposoma sasa tulia kama vile upo kwa kinyozi, ukijitikisa ukanatwa na wembe. Sikia.
Si mambo mazuri kuyasema, lakini kwa kuwa nafahamu kisheria, kama mwanasheria, kuwa kwa vyovyote iwavyo Acacia watafungua kesi kwa kutumia msingi huu wa kimataifa, ukweli uko hivi; tusijiandae kupata tu, bali hata kukosa.

Mwaka 1917, Serikali ya Costa Rica chini ya uongozi wa Rais Alfredo Gonzales Flores, ilipinduliwa na mtu aliyefahamika kama Federico Tinoco Granados. Jina maarufu ni Tinoco.
Tinoco alipochukua madaraka alibadili Katiba ya Costa Rica. Chini ya uongozi wake, Tinoco aliingia makubaliano (concessions) ya kutafuta mafuta na kampuni ya Uingereza. Alipitisha sheria zilizoanzisha sarafu mpya, na kwa njia za biashara benki za Uingereza zikajikuta zinashikilia kiasi kikubwa cha fedha za sarafu ya Costa Rica.
Mwaka 1919, wananchi waliandamana kwa kiasi kikubwa wakipinga sera na uendeshaji wa Serikali wa Rais Tinoco. Serikali ya Tinoco ilikuwa na upungufu na uendeshaji wa aina yake. Iliwaweka watu ndani kwa saa 48, ikaua watu, na wengine waliswekwa ndani bila ukomo wa muda wa jinai au madai.
Maandamano yaliendelea kwa miezi zaidi ya 9. Ilipofika Agosti 13, 1919, Tinoco alikimbia nchi. Askari Juan Quirós Segura, alishikilia nchi kwa wiki mbili tu hadi Septemba 2, 1919 aliporithiwa na Rais wa Mpito, Francisco Aguilar Barquero (Sept 2, 1919 – May 8, 1920).

Baada ya hapo mambo yalichangamka, akapatikana Rais wa kuchaguliwa, Julio Acosta García (May 8, 1920 – May 8, 1924). Rais Garcia, Agosti 22, 1922 alipitisha sheria ya kubatilisha Sheria ya Sarafu iliyopitishwa na Rais Tinoco. Sheria hii ilibatilisha miamala yote iliyofanywa chini ya Serikali ya Rais Tinoco.
Kesi ya usuluhishi ilianza chini ya Sheria za Kimataifa, Serikali ya Uingereza ikiwakilisha kampuni zilizofanya biashara na Serikali ya Costa Rica, chini ya Uongozi wa Rais Tinoco. Kampuni hizi zilikuwa ni: – Royal Bank of Canada na Central Costa Rica Petroleum Company.
Kampuni ya Uingereza iliyofahamika kama Royal Bank of Canada, ilidai kuwa inaidai Benki ya Costa Rica ya Kimataifa (Banco Internacional of Costa Rica) na Serikali ya Costa Rica kupitia hati fungani. Pia Central Costa Rica Petroleum Company [CCRPC), ilidai inamiliki haki za kutafiti na kuchimba mafuta nchini Costa Rica kwa mujibu wa hati fungani zilizotolewa na Rais Tinoco.

Katika utetezi wake, Serikali ya Uingereza, ilissema kuwa Serikali iliyofuata baada ya Tinoco inapaswa kutambua mikataba iliyoingiwa na Serikali ya Costa Rica chini ya uongozi wa Tinoco. Uingereza walisema wakati wa utawala wa Tinoco, watu walitii mamlaka na kila kitu kilikwenda kwa mujibu wa sheria, huku Serikali ya Costa Rica ikiwa madarakani.
Katika utetezi wao, Waingereza waliongeza kuwa kila Serikali inayoingia madarakani inaikuta na kuiacha – NCHI. Walijenga hoja kuwa kampuni hizo ziliingia mikataba na nchi na si Serikali iliyokuwapo madarakani, hivyo Serikali iliyokuwapo madarakani (wakati wa madai) haikuwa na mamlaka ya kufuta (repudiate) mikataba iliyoingiwa na Serikali iliyoitangulia.
Kwa upande wao, Costa Rica walisema mikataba hiyo haikuwa halali kwa sababu, ilikiuka na haki ya umiliki wa asili, lakini pia Uingereza ilikuwa haimtambui Tinoco kama Rais wa Costa Rica hivyo, mikataba aliyoingiwa si halali. Pia, walijenga hoja kuwa Tinoco alivunja Katiba ya Costa Rica, hivyo hakuwa na haki ya kuingia mikataba, na kwamba Uingereza isingeweza kuingia mikataba na serikali haramu.

Sitanii, haya ndiyo maneno yasiyopendeza katika masikio ya wanaharakati. Mahakama mwaka 1923 ilikataa, utetezi wa Costa Rica na kutoa uamuzi ufuatao. Kwamba wakati hoja ya Uingereza kutoitambua Serikali ya Tinoco ulikuwa ushahidi uliotiliwa maanani katika kufikia uamuzi wa sifa za Serikali, lakini haikuwa lazima kuwa uhalali wa Serikali ulipaswa kuangaliwa kwa kutumia ushahidi huo pekee.
Mahakama ilisema Serikali ya Tinoco ilikuwa Serikali halali kwa kipindi chote ilichokuwa madarakani. Kwamba kwa miaka miwili iliyokuwa madarakani, Serikali ya Tinoco ilitimiza wajibu wake kwa utulivu. Hayakutokea mapinduzi, kupinga serikali hiyo au chochote kiwacho ndani ya uhai wake.
Mahakama ilibaini kuwa Serikali ya Tinoco ilikuwa Serikali halali. Kuanzia wakati huo, ilianzishwa Kanuni ya Mwendelezo (The Principle of Continuity). Kanuni hii ina maana kuwa Serikali iliyoko leo ikitenda sawa au makosa kisheria, Serikali ijayo haina nafasi ya kuyapinga.

Kwa hiyo, Costa Rica iliamuriwa kulipa kila deni ililokuwa linadaiwa na kampuni za Kiingereza au Benki zilizopata kandarasi wakati wa utawala wa Tinoco. Hoja iliyojengwa ni kuwa iliyokopeshwa au kuingia mikataba ni nchi ya Costa Rica na si Serikali ya Tinoco.
Sitanii, pamoja na Costa Rica kutiwa hatiani, kuna jambo bado liliwasaidia hawakulipa deni husika. Mahakama ilisema kuwa pamoja na nchi hiyo kuwa na deni halali, Rais Tinoco alivunja Katiba iliyokuwapo mwaka 2017 wakati anachukua madaraka.
Kwa mantiki hiyo, kampuni hizo ziliingia mikataba kinyume cha Katiba ya Costa Rica. Sasa hapa ndipo ilipo hoja yangu ilipolala. Je, sisi tunayo nafasi ya kutokea kama Costa Rica? Mikataba hii tuliyoingia kuna jinsi inavyokiuka Katiba na sheria za nchi yetu? Ukiniuliza, nasema ndiyo, ila ngoja wanasheria wa Serikali yetu wapitie kisha watujulishe.

Fursa iko wapi ya kutokea? Sina jibu la moja kwa moja ila tuangalie mikataba ya kimataifa inasemaje? Sheria zetu zimekaaje? Wakati tunaingia mikataba hiyo tulikuwa na sheria halali? Je, tunayo nafasi ya kutokea kama Costa Rica? Tunafahamu matokeo ya kushindwa kuwa na majibu sahihi kwa uamuzi ambao tayari tumeufanya?
Sitanii, narudia kama nilivyoanza. Tunaweza tusiyapende maneno yangu, ila ikiwa tutashindwa katika kesi hizi, nikiamini zitakuwa zaidi ya moja kutoka kwa wawekezaji, tujiandae kulipa fidia nono au kulipa kupitia puani.
Sheria za kimataifa ukishidwa, kama unakataa kulipa ulichoamuriwa kulipa, yanatokea yafuatayo. 1. Kama una pesa nje ya nchi katika benki za kimataifa kama nchi zinakamatwa. 2. Kama una majengo (kama majengo ya ubalozi) yanaweza kunadiliwa. 3. Kama una vitega uchumi kama ndege, ikitua katika moja ya nchi zao walizo na mikataba nazo inazuiliwa kuruka, kisha zinauzwa kulipia deni.
Je, nchi yetu imejipanga kwa madhira haya? Nasema Serikali iwe tayari kusikia hata isiyoyapenda. Ikiwa itaendelea kushikilia msimamo, na ikatokea hakuna mwenye kuthibitisha kuwa uamuzi tulioufanya ulikuwa kwa mujibu wa sheria, basi tujiandae kulia na kusaga meno.