Kilichomng’oa bosi Jeshi la Magereza

url-8Aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, John Minja, hakuomba kujiuzulu kwa ridhaa yake, JAMHURI limethibitishiwa.

Badala yake, kiongozi huyo amefikia hatua hiyo baada ya kuwapo tuhuma kadhaa za matumizi mabaya ya madaraka zinazomkabili.

“Ziara ya ghafla ya Rais John Magufuli, pale Ukonga haikuwa ya bahati mbaya. Alijua nini anachokwenda kukifanya maana tayari taarifa zote zinazomhusu Minja, alishakuwanazo,” kimesema chanzo chetu cha habari kutoka Magereza.

Wiki iliyopita, Ikulu ilitoa taarifa kwamba Kamishna Jenerali Minja, alikuwa ameomba kujiuzulu, na kwamba Rais Magufuli, aliridhia ombi hilo. Nafasi yake kwa sasa inakaimiwa na Dk. Juma Malewa.

Mwaka mmoja uliipita, JAMHURI liliandika baadhi ya tuhuma zinazomkabili Minja, zikiwamo za kuwatumia wafungwa kwenye miradi yake binafsi.

Wakati huo, vyombo vya uchunguzi vya Serikali vilikuwa vimeanza kufuatilia ujenzi wa nyumba zake tano zilizokuwa zikijengwa Salasala, Dar es Salaam.

Nyumba hizo ziliibua maswali kadhaa kutoka kwa watu walio karibu naye, na hata watumishi ndani ya Magereza.

Taarifa zilisema Minja alikuwa akitekeleza ujenzi huo kwa kutumia magari ya Jeshi la Magereza, mafundi na vibarua ambao miongoni mwao wanatajwa kuwa ni wafungwa. Miongoni mwa wafungwa wanaotajwa ni wale waliokuwa na vifungo vya nje; na kwamba walikuwa hawalipwi.

Jirani na nyumbani kwake, amejenga ukumbi mkubwa wenye bwawa la kuogelea. Ujenzi wa ukumbi huo unadaiwa kugharimu mamilioni ya shilingi.

JAMHURI lilifika Salasala na kushuhudia ujenzi huo ukiendelea, huku gari kubwa la mizigo aina ya Scania na magari mengine madogo, mali ya Jeshi la Magereza yakihusika kwenye ujenzi huo.

Baadhi ya mafundi walidokeza kuwa ujenzi huo umekuwa wa kasi kutokana na kupatikana kwa vifaa vya ujenzi na amri ya mwenye mali.

“Hapa tangu tuanze kujenga hatujawahi kusimama hata kidogo, kila kitu tunapata. Wewe mwenyewe si unaona haya mambo yalivyokuwa makubwa?” alisema mmoja wa mafundi.

Wakati hayo yakiendelea, kulikuwapo taarifa za uhakika za kuchunguza chanzo cha ukwasi wa Kamishna Jenerali Minja.

Habari za uhakika zilionesha kuwa tayari timu ya uchunguzi iliweza kufika katika makazi yake kujionea ujenzi huo.

“Yeye binafsi hajui kama tayari mambo yameharibika, vijana wameshafika site (eneo la ujenzi) na wamemaliza kazi yao, wameshangazwa na jamaa anavyoweza kufanya mambo makubwa haraka kiasi hicho, lakini tunaamini chochote kinaweza kutokea,” alisema mtoa taarifa wetu Desemba mwaka jana.

Pamoja na kutumia rasilimali za Magereza, pia ilidaiwa wakati huo alikuwa akiandaa taratibu za kujitwalia gari ambalo amekuwa akilitumia.

“Tayari kunafanyika njama za yeye kuondoka na hilo gari analolitumia hivi sasa, hilo shangingi (Toyota Land Cruiser) lililonunuliwa likiwa jipya, na hivi ninavyokwambia (Desemba 2015) ameshalifanyia matayarisho ili aweze kulimiliki, na kuna kigogo anamsaidia kufanikisha hilo,” anasema mtoa taarifa.

Kamishna Jenerali Minja alizungumza na JAMHURI, lakini akagoma kufafanua kinachoendelea. Badala yake alimtaka mwandishi azungumze na maofisa habari wa Jeshi la Magereza.

Hata aliposisitiziwa kuwa ni suala linalomhusu yeye binafsi, alisema: “Kwa sasa sina nafasi hivyo ni vyema kuwasiliana na Kitengo cha Habari na kama kuna siku nitapata fursa nitazungumza, lakini si sasa.”

Vyanzo vya habari vya uhakika vimelizokeza JAMHURI kwamba rais aliamua kufanya ziara ya ghafla ili kuweza kujiridhisha na kile ambacho kimemfikia kuhusu uchunguzi uliofanywa kuhusiana na Kamishna wa Magereza.

Pia Minja anadaiwa kutumia madaraka yake kuuza mazao yanayolimwa na wafungwa sehemu mbalimbali nchini kwa manufaa yake.

“Magereza inayo mashamba makubwa, inalima na kuvuna mazao kila mwaka, lakini sehemu ya mazao imekuwa ikiuzwa na wajanja huku fedha hizo zikiishia pasipojulikana, na Serikali inalazimika kutoa pesa ya chakula,” amesema mtoa taarifa wetu.

Miongoni mwa mashamba yanayotajwa ni la Gereza la Kitengule lililopo mkoani Kagera. Lingine ni Gereza la Mifugo, Ubena mkoani Pwani.

Kamishna Jenerali Minja, anashutumiwa kwa kufumbia macho kitendo cha wafungwa kutumiwa kuzalisha mali ambazo mwishowe huishia mikononi kwa maofisa Magereza.

“Si kweli kuwa wafungwa hawafanyi kazi. Wanafanya kazi nyingi na ngumu, tatizo ni kuwa kazi wanazofanya zinawanufaisha wakubwa tu. Wafungwa wamekuwa ‘mashine’ za uzalishaji za wakubwa wa Magereza,” kimesema chanzo chetu.

Pamoja na kilimo, shughuli nyingine zinazodaiwa kuwanufaisha wakubwa ni za ujenzi na ufundi wa fani mbalimbali.

JAMHURI limethibitishiwa kuwa miongoni mwa mambo yanayomchefua, hasa katika Jeshi la Magereza na Polisi, ni kitendo cha sare na vifaa vya askari wa majeshi hayo kuhodhiwa na watu wachache.

Kumekuwapo taarifa za kutengwa kwa fedha kwa ajili ya sare za askari Magereza, lakini mara kadhaa askari hao wamelazimika kununua kwa fedha zao wenyewe. Pamoja na nguo, pia wananunua viatu. Vifaa hivyo vimekuwa vikipatikana katika maduka ya watu binafsi, wakiwamo wanasiasa na maofisa waandamizi katika Magereza na Jeshi la Polisi.

 

UZALISHAJI KATIKA JESHI LA MAGEREZA 

Kilimo, Mifugo na Utunzaji Mazingira

Jeshi la Magereza lina eneo lenye ukubwa wa hekta 130,482 ambalo hutumika kwa shughuli za Kilimo, Mifugo na Hifadhi ya Mazingira. Juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuhakikisha kuwa kilimo kwenye Magereza kinakuwa cha kisasa na chenye tija, lengo kubwa likiwa ni kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na ziada kuuzwa kwa wananchi wengine.

Aidha, mashamba haya pia yameendelea kuwa mashamba darasa ya kujifunzia kilimo kama mbinu mojawapo ya urekebishaji wa wafungwa.

Kwa sasa yapo mashamba makubwa 43 ambayo yamegawanyika kama ifuatavyo:-

• Mashamba ya kilimo – 14 (Idete, Ludewa, Kwitanga, Kibiti, Mkwaya, Kimbiji, Pawaga, Kitete, Kalila, Mng’aro, Bagamoyo, Kihonda, Ngwala na Mang’ola;

• Kilimo na Mifugo (mixed farms) – 16 (Songwe, Arusha, Mollo, Butundwe, Kitai, Ilagala, Kibondo, Nachingwea, Wami Kuu, Kiberege, Ushora, Msalato, Kilimo Urambo, Kitengule, Isupilo na Kiabakari;

• Ranchi za Mifugo – 11 (Mugumu, Mbigiri, KPF, King’ang’a, Namajani, Maji – Maji, Ubena, Rusumo, Kilwa na Kingurungundwa na Mollo;

• Mashamba ya ng’ombe wa maziwa – 2 (Isupilo & KPF).

Kati ya mashamba haya 43; mashamba 15 ya kilimo na mifugo yanaendeshwa na Shirika la Magereza kwa mpango wa “Revolving Fund”.

Mashamba 28 yaliyobaki yanaendeshwa chini ya utaratibu wa Serikali, ambako Serikali Kuu hutoa fedha za kuhudumia uzalishaji. Mazao yanayolimwa katika mashamba haya huuzwa na fedha kuingizwa serikalini kama maduhuli.

Mazao yanayozalishwa katika mashamba ya Magereza ni mahindi, mpunga, maharage, mtama, mbegu za mafuta (michikichi, alizeti, karanga, ufuta) na uendelezaji wa bustani za mboga mboga za aina mbalimbali na matunda.

Pia Jeshi linaendelea kutunza mashamba ya mazao mengine ya kudumu yakiwamo chai, mkonge, kahawa, minazi, korosho na miwa ambayo yapo katika mikoa mbalimbali.

Aidha, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika (Wakala wa Mbegu za Kilimo) ASA, pamoja na kampuni za Highland Seed Growers na TANSEED International, Jeshi la Magereza huzalisha mbegu za mazao ya kilimo za mahindi, maharage, mpunga, mtama, kunde, choroko, ufuta, karanga, alizeti, mbegu mbalimbali za mboga mboga na vipando bora vya mihogo.

Kwa upande wa mifugo, Jeshi la Magereza linaendeleza juhudi za ufugaji bora wa ng’ombe wa nyama na maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, kuku na bata kwa kutumia teknolojia rahisi na za kisasa ili kuwa mfano wa kuigwa.

Uvuvi: Kwa upande wa uvuvi, miradi huendeshwa katika maeneo yaliyo karibu na maziwa kama Butimba – Mwanza na Bangwe, Kigoma. Aidha, ufugaji wa samaki unaendelea katika Magereza ya Karanga, Moshi; Kwamngumi – Tanga na jitihada zipo za kufufua/ kuanzisha ufugaji huo katika maeneo mengine pia.

Katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia-nchi, Jeshi la Magereza huendesha shughuli zake kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira. Miti takribani 6,000,000 imeshapandwa katika eneo la jumla ya hekta 3,526 katika Magereza mbalimbali nchini.

Aidha, uoto wa misitu ya asili iliyopo katika maeneo yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza inayokadiriwa kufikia hekta 14,053 inaendelezwa kwa kuhakikisha mazingira yanabaki salama. Miradi ya ufugaji nyuki kwa ajili ya kuzalisha asali na nta imeanzishwa na inaendelezwa katika kuhakikisha kuwa Jeshi linapata faida kubwa katika miradi ya utunzaji wa mazingira.

Viwanda vidogovidogo

Kitengo cha viwanda kinahusika na kuwafundisha wafungwa stadi mbalimbali za ufundi kama useremala, ushonaji, utengenezaji wa sabuni, utengenezaji vifaa vya mikono (ufumaji, useketaji, uchoraji, ufinyanzi na ususi) kwa nia ya kuwarekebisha tabia ili wamalizapo adhabu zao wawe raia wema wanaoweza kujitegemea.

Lengo kuu la kitengo hiki ni kusimamia na kudhibiti uzalishaji bora wa bidhaa, kuandaa mfumo mzima wa maendeleo ya viwanda vidogo vidogo na utekelezaji wake. Programu za urekebishaji katika viwanda hutekelezwa na Wakuu wa Magereza/Viwanda kwa kushirikiana na Ofisi ya Makao Makuu.

3321 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons