KISA SH 3,000… Azuiwa kufanya mtihani wa taifa

*Mzazi aja juu, ataka Mkuu wa Shule achukuliwe hatua

*Mwenyewe ajitetea, asema sababu ni utoro, utovu wa nidhamu

Dar es Salaam

Na Aziza Nangwa

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kinyamwezi iliyopo Pugu, Dar es Salaam, Sophia Said, amezuiwa kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu kutokana na malimbikizo ya deni la Sh 3,000.

Mzazi wa Sophia, Said Ngundangu, ameliambia JAMHURI kuwa deni hilo linatokana na masomo ya ziada.

“Mkuu wa shule alikuwa akiwadai wanafunzi kutoa Sh 200 kila siku. Jumatatu (siku mitihani ilipoanza) nilimwandaa Sophia kwenda kufanya mitihani ya mwisho na mimi kuelekea kwenye shughuli zangu.

“Niliporudi nyumbani jioni, nikamkuta. Akaniambia Mkuu wa Shule amemrejesha nyumbani kwa kuwa anadaiwa fedha za masomo ya ziada. 

“Nilisikitika na kukasirika sana. Kulipokucha, nikamchukua na kwenda naye moja kwa moja kwa Mkuu wa Shule ili kujua kulikoni Sh 3,000 isababishe mtoto asifanye mitihani ya mwisho?” anasema Ngundangu akimtaja Sifa Mwaruka kuwa ndiye Mkuu wa Shule ya Sekondari Kinyamwezi.

Mzazi huyo anasema Mwalimu Sifa alitaka kufahamu Sophia alimpa majibu gani kama sababu ya kuzuiwa kufanya mtihani, naye akamwambia kuwa ni deni la masomo ya ziada.

“Mwalimu akasema kuwa Sophia hakusema ukweli, akidai kuwa sababu kubwa ya kumzuia kufanya mtihani, eti mtoto wangu ni mtoro,” anasema.

Hoja ya utoro haikuingia kichwani mwa mzazi, kwa kuwa katika miaka minne ya Sophia aliyosoma, yeye kama mzazi hajawahi kuitwa shuleni.

Mbali na hilo, anasema mwanaye alisajiliwa kwa ajili ya kufanya mitihani ya mwisho; kwa nini azuiwe?

“Ubishi ukawa mkubwa. Nikaona kwa kuwa mwalimu mwenyewe ni mtoto wa kike nisije nikampiga kwa hasira; nikaondoka na kwenda kwa Mtendaji wa Kata, lakini hakuwapo ofisini,” anasema Ngundangu. 

Siku iliyofuata, Ngundangu akaenda kumuona Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya aliyeahidi kulishughulikia suala hilo kwa kuwa si haki mwalimu kumzuia mwanafunzi kufanya mitihani.

Baada ya muda, Ofisa Elimu akampelekea majibu kwamba Sophia alizuiwa kuingia chumba cha mtihani kwa kuwa alikwenda shule akiwa hana sare za shule huku amevaa heleni.

JAMHURI limezungumza na Mwalimu Sifa anayekiri kuwa Sophia ni mwanafunzi wake.

“Amezuiwa kufanya mtihani. Sababu si hizo anazosema mzazi wake. Sophia ana tabia ya utoro. Kwa takriban miezi miwili alikuwa hajafika shuleni.

“Na alipokuja kwenye mitihani, hakuvaa sare za shule! Alikuwa amevaa nguo za nyumbani. Kwa hiyo nilimrudisha ili akavae sare, kisha aje kwenye mitihani kwa kuwa kwa hali aliyokuwa nayo asingeruhusiwa kufanya mitihani.

“Lakini cha kushangaza, yeye akaondoka moja kwa moja. Hakurudi mpaka kesho yake alipokuja na mzazi wake,” anasema Mwalimu Sifa. 

Mkuu wa Shule anasema jitihada za kumwelewesha mzazi wa Sophia sababu ya kuzuiwa kwa binti yake zilishindikana kwa kuwa hakutoa ushirikiano na kuondoka kwa hasira.

“Tulipomhoji zaidi, akasema ni yeye ndiye alimzuia Sophia kuja shuleni (kwa miezi miwili) akidai kuwa katika kipindi hicho wanafunzi hawakuwa wakisoma,” anasema.

Mwalimu Sifa anasema kwa ujumla Sophia hakuwa akifanya vizuri kimasomo na hata mitihani ya majaribio ya kidato cha nne hakufanya vizuri. 

“Baba yake hajawahi kuhudhuria vikao vya wazazi na uongozi wa shule kuzungumzia maendeleo ya watoto wao. Hakuwa akitoa ushirikiano hadi siku alipokuja kuhoji sababu ya mtoto kuzuiwa kufanya mtihani,” anasema Mwalimu Sifa.