Kocha wa kuogelea alete manufaa

Ujio wa kocha wa mchezo wa kuogelea, Sue Purchase, kutoka Shule ya Kimataifa ya Mtakatifu Felix ya Uingereza, unatarajiwa kurejesha ari ya mchezo huo ambao umeanza kupotea nchini katika miaka ya hivi karibuni.
Kocha huyo raia wa Uingereza, amekuja nchini kusaka vipaji vya mchezo huo kwenye mashindano ya Taifa yaliyofanyika wiki iliyopita, jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo ya klabu bingwa Taifa yalifanyika kwa kushirikisha jumla ya wachezaji 172 kutoka klabu 15 za Tanzania Bara na Zanzibar, hali inayotarajiwa kunyanyua ari ya mchezo huo hapa nchini.
Akizungumza na JAMHURI, Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhan Namkoveka, amesema hiyo ni fursa pekee kwa wachezaji wa mchezo huo kujitangaza kimataifa.
“Hii ni nafasi adimu na ya kipekee kwa wapenzi na wachezaji wa mchezo huu kuitumia nafasi hii kuweza kujitangaza kimataifa kwa manufaa yao na kwa faida ya Taifa kwa ujumla,” amesema Namkoveka.
Amesema, Purchase, ambaye pia  ni Mkurugenzi wa mchezo wa kuogelea wa shule hiyo, anakuja nchini akiwa na  lengo la kusaka vipaji vya mchezo huo na kuangalia namna rahisi ya kuuendeleza kwa hapa nchini.
Amesema wachezaji Sonia Tumiotto, Collins Saliboko, Anjani Taylor,  Smriti Gokarn na Aliasgar Karimjee ambao wanasoma Uingereza, tayari wameshawasili nchini kushiriki mashindano hayo na tayari wanaendelea na mazoezi Dar es Salaam,” amesema Namkoveka.
“Waogeleaji wetu walioko nje wameonesha viwango vya hali ya juu kiasi cha kumfanya Purchase kuamua kuja nchini kushuhudia waogeleaji wengine wa Tanzania katika mashindano hayo,” amesema Namkoveka.
Amesema mbali ya kushuhudia mashindano hayo na kusaka vipaji, kocha huyo atakutana na wazazi, makocha, waogeleaji wa klabu ya Dar Swim Club na kufanya nao mazungumzo.
Amesema  ni faraja kwa wadau, wachezaji, klabu  na viongozi wa mchezo wa kuogelea kwani ujio wa kocha ni ishara ya mchezo kuanza kukua kiasi cha kuanza kuvutia hata wataalamu kutoka nje.
Mashindano hayo yatashirikisha klabu 15 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambazo zitashindana katika staili za backstroke, butterfly na staili nyingine ambazo hutumika kimataifa. 
Kwa upande wake Mkufunzi mkuu wa kituo cha Dar Swimming Club, Jofrey Kimimba, amesema mchezo wa kuogelea ni miongoni mwa michezo maarufu duniani.
Amesema ujio wa mgeni huyo ni faraja kwa wanafamilia wote wa mchezo, na unaweza kuja kufungua mlango kwa wachezaji chipukizi waliopo nchini kwa manufaa ya Taifa katika siku zijazo.
“Kwa kushirikiana na chama cha kuogelea Tanzania (TSA), tunatarajia kuongeza mchezo mpya wa kuogelea baharini (Open Water) ili kuongeza idadi ya wachezaji wenye uwezo wa kuitangaza nchi kimataifa,” amesema Kimimba.
“Katika mchezo wa kuogelea, wapo watu mbalimbali ambao wamefanya makubwa na kuishangaza dunia kutokana na umahiri waliokuwa nao katika mchezo huo kiasi cha kujijengea heshima kubwa duniani,” amesema Kimimba.
Kimimba amesema mchezaji kama Michael Phelps aliyezaliwa Juni 30,  1985 katika Kitongoji cha Baltimore mjini Maryland, Marekani, ni miongoni mwa wakali wa mchezo huo anayeheshimika mno kila pembe ya dunia.
Amesema mchezaji huyo anashikilia rekodi ya muda wote kwenye michuano ya Olimpiki akiwa kama mwogeleaji aliyetwaa medali 23 za dhahabu akiwa kinara katika michuano hiyo kwa awamu tofauti.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau hawana budi kutupia macho michezo mingine kama kuogelea kuliko kuendelea kuongelea mchezo wa soka kila kukicha, ilhali umeshindwa kufikia malengo.

442 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons