Korosho bado ni ‘umiza kichwa’! (2)

Sehemu iliyopita, mwandishi alieleza
namna suala la korosho lilivyoibua
mjadala miaka iliyopita. Sehemu hii ya
pili anaanza kueleza namna baadhi ya
magazeti yalivyoripoti habari za korosho
miaka ya 2000; na makala aliyoiandika
wakati huo kuelezea historia ya zao hilo.
Endelea…
“Bei ya korosho inashushwa kwa njama”
(Uhuru Jumatatu 25 Desemba, 2000 uk. 6),
“Cashewnut Industry in Crisis” (Business
Times, Friday March 2, 2001 front page);
“KOROSHO: Soko huria au soko holela?”
(Rai, Alhamisi 4 – 14 Machi, 2001
Upembuzi Yakinifu uk. 7); “Korosho:
Biashara kichaa Tanzania” (Rai, Alhamisi
15 – 21 Machi 2001, uk. wa mbele); “Serikali
yaokoa wakulima wa korosho” (Majira,
Jumapili 18 Machi 2001, uk. 3); “Kahama
akubali mambo si sawa kwa zao la korosho”
(Mtanzania, Jumapili 18 Machi 2001 uk. 5);
“Bodi ya Korosho yawafuta machozi
wakulima (Alasiri, Jumatatu 19 Machi 2001

uk. 6); “Masasi MP accuses Asian traders of
exploitation” (The African, Monday 26,
March, 2001 front page). “Ukichaa wa
biashara ya korosho ni matokeo ya uroho
wa wafanyabiashara” (Rai, Alhamisi Machi
29 – 4 Aprili 2001 uk. 11); “Korosho
biashara kichaa Tanzania (Rai, Alhamisi 5 –
11 Aprili 2001 uk. 7); “Serikali ituokoe
wakulima wa korosho Mtwara” (Mwananchi,
Jumatatu Aprili 11, 2001 uk. 7); “Wakulima
wa korosho Mtwara tumeyumbishwa”
(Mtanzania, Jumanne 17 Aprili, 2001 uk.
11); “CBT: Kwa wenzetu korosho ni
biashara, mpango wa ajira, sisi?”
(Mtanzania, Jumatano Aprili 18, 2001 uk. 7).
Vichwa hivi vya habari kuhusu korosho
vinatoa ujumbe kwa serikali na kwa
Watanzania wote kulishughulikia zao hili la
korosho kikamilifu. Kila mtu anayo haki ya
kutafsiri vichwa hivyo vya habari za korosho
anavyoona yeye. Mimi binafsi ninajiuliza
swali kubwa akilini mwangu, katika msimu
huu wa 2000/2001. “Korosho: Kulikoni?”
Kutokana na swali hili nimeona nikumbushe
Watanzania wenzangu historia ya zao la
korosho kutoka miaka ile ya 1940
lilipoanzishwa katika nchi yetu.
Katika miaka hiyo ya 1940 (nineteen forties
to sixties) mpaka kufikia mwanzoni mwa

miaka ile ya 1960 (1945 – 1960) kule Jimbo
la Kusini (Southern Province) hakukuwa na
zao maalumu la biashara, ukiachilia mbali
tumbaku kule Songea na kahawa sehemu
za Umatengo, wilaya hiyo hiyo ya Songea
na mkonge kidogo kule Lindi.
Serikali ya mkoloni ilijaribu zao la pamba
ikathibitika halifai kwa sababu ya wadudu.
Likapigwa marufuku kabisa ulimaji wake.
Hali hiyo ilifanya kiwanda kidogo cha
kuchambulia pamba pale Tunduru (The
Kikanda Cotton Mill) na kile Kiwanda cha
Mvangavanga (sasa Narunyu), Lindi Vijijini
kufungwa kabisa. Hivyo sisi wa ukanda wa
Tunduru mpaka Lindi hatukuwa na zao la
biashara isipokuwa ufuta, karanga, alizeti,
kunde na nafaka – hasa mpunga.
Serikali ya mkoloni ilijaribu kutuletea neema
kwa zao la karanga chini ya mpango
maalumu wa kikoloni (Uingereza) ulioitwa
‘The groundnut scheme’. Kampuni ya
kikoloni iliyoitwa OFC (Overseas Food
Corporation 1946 – 1949) iliandaa mpango
wa kuwaajiri askari wa Kiingereza kutoka
vitani (1939 – 1945 demobilized soldiers)
kwa kuzalisha karanga kupata mafuta ya
kula kwa Jumuiya ya Madola.
Mpango ambao ungezalisha karanga

Nachingwea (Kusini), Kongwa (Kati) na
Urambo (Magharibi). Ndipo yalifunguliwa
mashamba makubwa ya karanga pale
Nachingwea mwaka 1948 – 1949. Katika
mpango huo, Nachingwea pia kilijengwa
kituo cha utafiti (research centre) cha
mbegu bora na wadudu waathirio mazao.
Mwaka 1949 Uingereza waliona wazi
mpango huo wa ‘groundnut scheme’
hautafanikiwa, wakauachilia mbali.
Mashamba yale makubwa pale Nachingwea
yakageuka mapori. Alama pekee ya OFC
iliyosalia mpaka leo pale Nachingwea ni ule
uwanja wa ndege mkubwa unaotumika
mpaka sasa.
Lakini serikali ya kikoloni ilibuni shirika la
kilimo kurithi shughuli zile za OFC. Shirika
hilo liliitwa TAC (The Tanganyika
Agricultural Corporation) ambalo lilipewa
majukumu ya kulima njegere pale
Nachingwea na kuendeleza kituo kile cha
utafiti wa mazao ya biashara kwa Kusini.
Hapo ndipo lilipobuniwa zao hili la korosho.
Baada ya utafiti wao kuonyesha mafanikio,
mbegu za korosho zilisambazwa katika
wilaya kadhaa za Mkoa wa Kusini. Mtafiti
aliyehitimu Chuo Kikuu cha Makerere
aliyeitwa Geofrey Semiti aliongoza utafiti
pale Nachingwea.

Mimi nilikuwa miongoni mwa vijana
waliopanda korosho za mwanzo mwanzo
pale Nakayaya, Tunduru mwaka 1950
(nikiwa katika likizo yangu ya mwaka kutoka
shuleni St. Mary’s Tabora).
Licha ya kujihusisha na huo upandaji wa
korosho, nilibahatika pia kujishughulisha na
uuzaji wa korosho sehemu za Chikundi,
Ndanda na Nangoo msimu wa 1954 – 1955.
Wakati ule alitokea mzee (hayati sasa)
Mwalimu Rafael Komba aliyependa
kuwasaidia wananchi kujinasua kiuchumi.
Kwa vile tulikuwa sote tunafundisha Abbey
School Ndanda, alipojishughulisha
kuwatafutia soko la korosho wakulima wa
Ndanda, Nangoo na Chikundi, nilikuwa
nafuatana naye.
Siku hizo Kusini vilikuwapo vituo kadhaa
vya makazi ya wafanyabiashara nje ya miji
ya makao makuu ya wilaya. Vituo hivyo
vilijulikana kama ‘Trading Centres’ na ndipo
mahali wakulima waliweza kuuza mazao
yao badala ya kupeleka ‘bomani’ makao
makuu ya wilaya ambako kulikuwa makao
au masoko ya biashara ki-wilaya.
‘Trading Centres’ hizi zilikuwa sehemu
kama vile Chikundi, Nangoo, Chiungutwa,
Nangomba, Lulindi n.k (Wilaya ya Masasi);

Nakapanya, Namasakata, Lukumbule,
Mbesa, Matemanga n.k (Tunduru); Mahuta,
Nanyamba, Kitangari (Newala) Mtama,
Mingoyo, Ruponda, Ruangwa n.k (Lindi) na
vingine vingi tu.
Katika vituo hivi (Tranding Centres)
wafanyabiashara wakubwa walikuwa
Wahindi na walikuwa wananunua mazao
yote ya wakulima kama ufuta, karanga,
nyonyo, nafaka, kunde, nta/sera, pembe za
ndovu, za ngiri na za kiboko na korosho.
Hapo ilikuwa soko huria kila mtu alinunua
kwa bei waliyopanga hawa
wafanyabiashara.
Korosho zile wao walizipeleka Mtwara
ambako wafanyabiashara wakubwa kutoka
nje (hapa ni India) walinunua. Katika ile
tafuta tafuta ya wanunuzi wa Mtwara, mzee
Mwalimu Rafael Komba alifanikiwa kumpata
mnunuzi wa kampuni iliyokuwa ikisafirisha
korosho India. Hii iliitwa Edgar Bowman and
Co. Ltd na iliweza kununua korosho zote
zilizokuwapo Chikundi, Ndanda na Nangoo
kwa bei kubwa kuliko iliyotolewa na wale
wanunuzi katika vile vituo vya biashara.
Kampuni hiyo ikataka kufanya mkataba na
wakulima hao wa korosho ili kila mwaka ije
kununua korosho zao. Mwalimu Rafael
Komba akaona njia pekee ya wakulima

kuuza korosho zao kwa kampuni hiyo ni
kujumuika pamoja katika chama cha
ushirika.
Basi, wakulima wale wa Chikundi, Nangoo
na Ndanda wakaungana katika vyama vitatu
vya ushirika. Liwali wa Chikundi mzee
Benedikto Achimpota (ambaye sasa ni
hayati), alimwomba DC wa Masasi siku zile
akiitwa Neath kusaidia kumpata ofisa
ushirika katika Tarafa ya Chikundi kuandaa
ushirika ili msimu wa korosho 55/56 pawepo
na mauzo bora zaidi.
Basi kwa jitihada za serikali, Chikundi
ikaletewa mkaguzi wa ushirika aitwaye
Alfons Rugaihurura (Co-operative Inspector)
aliyesimamia uanzishaji wa vyama katika
tarafa za Chikundi na Lisekese. Msimu wa
korosho wa 1955/1956 na 1956/1957
korosho zote za sehemu hiyo ziliuzwa
kiushirika katika vituo vilivyoitwa ‘Unions’.
Maendeleo ya vyama hivyo huko Masasi
yalionekana wazi na wakulima walifurahia
kupata fedha zaidi katika ‘Unions’ kuliko
kule kwenye ‘Trading Centres’.
Mwaka 1959 aliletwa Ofisa Ushirika wa
Wilaya (District Co-operative Officer),
Dickson Nkembo (hayati) kutoka Songea.
Huyu alikuwa graduate (mhitimu) kutoka

Makerere, hivyo Masasi ilibahatika kupata
mtaalamu wa juu namna hiyo. Yule Co-op.
Inspector Rugaihurura alihamishiwa
kwingine. Kuja kwa Nkembo kuliimarisha
vyama vya ushirika, hatimaye serikali
iliunda chama kikuu cha ushirika

kilichojulikana kama Mtwara – Ruvuma Co-
operative Union Ltd. (Angalizo: Dickson

Nkembo ndiye aliyekuja kuwa Katibu Mkuu
wa Ikulu miaka ya 1970.)
Ushirika huo ndio ulionunua korosho za
wakulima wa Tunduru, Masasi,
Nachingwea, Newala – Lindi na Mtwara na
kuziuza kwa mnada kwa wafanyabiashara
binafsi pale Mtwara ambao waliziuza
korosho zote India. Ndipo mwanzoni mwa
miaka ile ya 1960 serikali iliunda bodi
maalumu ya mazao kule Kusini
kushughulikia mazao yote likiwamo zao la
korosho. Hatimaye mwaka 1964 serikali
iliunda Bodi ya Kitaifa ya Mazao (National
Agricultural Products Board) (NAPB)
kushughulikia mazao yote ya nchi yetu
pamoja na korosho.

Itaendelea…

1037 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons