KUELEKEA UCHAGUZI MKUU KENYA Ruto apangakufanya aliyoyakataa BBI

MOMBASA

Na Dukule Injeni 

Masilahi ndicho kitu kinachowaleta wanasiasa pamoja na ndivyo ilivyo hususan kipindi hiki ambapo vyama vinaungana kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu. 

Licha ya uwepo wa wagombea huru zaidi ya 40 wanaowania kumrithi Rais Uhuru Kenyatta na wengine takriban 10 ambao wameteuliwa na vyama au miungano ya kisiasa, ni wawili tu wenye mvuto; Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. 

Ruto ambaye ni kiongozi wa United Democratic Alliance (UDA), yupo kwenye ‘muungano’ wa ‘Kenya Kwanza’; wakati Odinga ambaye ni kinara wa Orange Democratic Movement (ODM) anawania urais kupitia ‘muungano’ wa ‘Azimio la Umoja One Kenya Alliance’. 

Vyama vikuu ndani ya Kenya Kwanza ni UDA, Ford Kenya na Amani National Congress (ANC) huku ndani ya Azimio la Umoja kuna ODM, Jubilee ya Rais Kenyatta, Wiper, KANU na Narc. Ni miungano miwili ambayo pia ina vyama vidogo vingi vikiwa ni vya kikanda. 

Wingi wa vyama ndani ya muungano unachangiwa kwa kiasi kikubwa na masilahi ya viongozi wa vyama hivyo na ndiyo maana kulikuwa na vuguvugu la kubadilisha vipengele vya Katiba kupitia ‘Building Bridges Initiative (BBI)’

Hata hivyo, jaribio hilo liliangushwa kwenye kuta za sheria kuanzia Mahakama ya Juu kisha Mahakama ya Rufaa na hatimaye Mahakama ya Upeo wa Juu (Supreme Court), ikiamsha shangwe kwa muungano wa Kenya Kwanza uliokuwa ukisema kuwa wenzao wa Azimio la Umoja walikuwa wakiwaza kugawana vyeo kupitia BBI. 

Kenya Kwanza waliwashutumu Azimio la Umoja kwa kutaka kubadili Katiba na kubuni nafasi za waziri mkuu, manaibu waziri wakuu wawili na mawaziri ambao lazima wawe wabunge wakiwa na lengo la kugawana vyeo baina ya viongozi wanaounda muungano huo chini ya Odinga. 

Ruto ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipinga BBI alisisitiza sera yao ni kumkomboa mwananchi na kampeni zao zinalenga kuboresha uchumi na si kugawana vyeo. 

Hata hivyo, miezi mitatu tu tangu mahakama kuzuia jaribio la kubadilisha Katiba kupitia BBI, nyaraka zilizosainiwa na vyama tanzu vya Kenya Kwanza, zimebainisha namna wanavyopanga kugawana madaraka pindi watakapochaguliwa. 

Katika nyaraka hizo, Ruto atakuwa Rais na Chama chake cha UDA kitamteua naibu rais huku kinara wa ANC, Musalia Mudavadi, akiteuliwa waziri mkuu na hii itakuwa baada ya Ruto kutumia mamlaka yake ndani ya siku 14 kubuni nafasi hiyo. 

Moses Wetangula ambaye ni kiongozi wa Ford Kenya ametengewa nafasi ya Spika wa Bunge la Seneti huku kiongozi wa Chama cha Maendeleo Chap Chap, Alfred Mutua, ambaye alihama Azimio la Umoja na kujiunga na Kenya Kwanza atapewa nafasi ya kiongozi wa wengi katika Bunge la Seneti kama muungano wao utashinda urais na endapo ukishindwa atapewa nafasi ya kiongozi wa wachache. 

Kitendo cha Kenya Kwanza kugawana vyeo, kimeibua hisia kali kutoka kwa mtu wa karibu na Odinga, Junet Mohamed, akimshutumu Naibu Rais Ruto akidai anapanga kubadilisha Katiba. 

Junet anamshanga Ruto kwa kuwa mstari wa mbele kuiponda BBI kwa madai inatumia fedha nyingi za walipa kodi kubuni vyeo kwa masilahi ya viongozi na sasa ni yeye anapanga kuirudisha BBI endapo atashinda uchaguzi mkuu wa Agosti. 

“UDA itatoa Rais na Naibu Rais wakati ANC ya Musalia Mudavadi itapewa nafasi ya Waziri Mkuu ambayo haipo. Moses Wetangula wa Ford Kenya atakuwa Spika wa Bunge la Seneti. Kutokana na kikosi hiki, mambo mawili yapo wazi kuwa Kenya Kwanza chini ya William Ruto inawaza vyeo, si mwananchi wa kawaida,” amesema Junet ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki. 

Amesema wao katika Azimio wamekuwa wazi tangu mwanzo kuwa Kenya inahitaji mfumo wa kisiasa na utawala unaounganisha jamii zote.