Siku chache baada ya Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, wakala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuzifunga ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kushindwa kulipa kodi, wadau wamesema hali hiyo inaweza kuchangia kudhoofisha ushiriki wa timu ya Serengeti Boys katika fainali za Afrika nchini Gabon.

Viongozi na wafanyakazi wa TFF wamekuwa wanafanya kazi chini ya miti, huku vitendea kazi vyao vikiwa vimefungiwa katika ofisi hizo zenye makao yake makuu, Mtaa wa Shaurimoyo, Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam. 

Mmoja wa maafisa wa TFF ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, ameliambia JAMHURI kuwa Shirikisho hilo limekuwa likifanya kazi katika mazingira magumu, hasa kutokana na maandalizi ya timu ya vijana, Serengeti Boys, yanayoendelea.

“Ni zaidi ya wiki moja sasa tuko nje ya ofisi, hapa tunaendelea na maandalizi ya Timu ya Vijana, tunahitaji kuwasiliana na Makao Makuu ya CAF, Cairo, Misri. Hatuwezi kupokea wala kutuma barua pepe,” kimesema chanzo chetu.

Hata hivyo JAMHURI limepata taarifa kwamba miongoni mwa madeni yaliyosababisha ofisi hizo kufungwa, ni pamoja na kodi zitokanazo na mishahara ya makocha wa kigeni (Marcio Maximo, Kim Paulsen), mishahara ambayo ilikuwa inalipwa na Serikali.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wadau wa soka nchini wamesema kitendo hicho kinaweza kuwa na athari za kiutendaji kwa upande wa viongozi kiasi cha kulazimika kufanya kazi wakiwa nje ya ofisi  na kujikuta wakikabiliwa na wakati mgumu kiutendaji.

Kocha wa zamani wa timu ya taifa, Charles Boniface Mkwasa, amesema kuna umuhimu wa kuwapa ushirikiano wa hali na mali TFF katika kipindi ambacho timu ipo katika maandalizi ya kuelekea katika mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika nchini Gabon.

Amesema TRA wanapaswa kuwapa TFF kitu kinachoitwa ‘exception’ ili waweze kulipa kidogokidogo kuliko kuanza kukimbilia kufunga ofisi zao hasa katika kipindi hiki ambapo Shirikisho lipo katika maandalizi ya kuhakikisha timu inakwenda kushindana.

“Ni lazima tuwe wakweli; TFF wanakabiliwa na wakati mgumu wa kuiandaa timu yetu ya Serengeti Boys, kitendo cha kuzifunga ofisi za TFF ni kukosekana kwa uzalendo kana kwamba timu hiyo haiwahusu, suala ambalo si sahihi,” amesema Mkwasa.

Mkwasa amesema fedha wanazodaiwa TFF na Mamlaka ya Mapato Tanzania ni madeni yanayosemekana kuanzia kipindi cha aliyekuwa kocha wa Timu ya Taifa, Macio Maximo, hali inayoiweka hata mamlaka hiyo katika katika maswali ya kujibu ya ‘walikuwa wapi mpaka wajitokeze wakati huu?’ 

Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Chaurembo Palasa, ameliambia JAMHURI kuwa kitendo hicho kinaweza kuwa na athari kubwa kwa maandalizi ya vijana wa Serengeti Boys kuelekea katika mashindano hayo.

Katika mashindano hayo, Serengeti Boys imepangwa Kundi B. Kundi hilo linajumuisha timu ambazo zinatoka katika nchi zilizopiga hatua katika mchezo wa soka.

“Timu hii ni ya Watanzania wote, inayohitaji sapoti ya kila Mtanzania, kitendo cha TRA kufunga ofisi za TFF na kusababisha watendaji kufanya shughuli zao wakiwa majumbani katika kipindi hiki, ni ukosefu wa uzalendo,” amesema Palasa.

Kocha wa Serengeti Boys, Bakari Shime, amenukuliwa akisema wachezaji wote wameripoti kambini kwa ajili ya maandalizi ya kujipatia tiketi ya kucheza Kombe la Dunia kwa vijana kama watafanya vizuri katika mashindano hayo.

“Tumeona tuanze mapema maandalizi yetu, maana siku zinakwenda na mambo ni mengi, lengo letu siyo kwenda kushiriki bali ni kushindana na hatimaye kutwaa ubingwa, hayo ndiyo matarajio ya Watanzania wengi,” amesema Shime.

Amesema michezo ya kirafiki ya kimataifa itakayocheza ikiwa mkoani Kagera ni mchezo dhidi ya Rwanda (Machi 28), Burundi (Machi 30,) na Uganda (Aprili 2). Michezo yote itafanyika Uwanja wa Kaitaba, ulioko Bukoba mkoani Kagera.

Amesema timu itaunganisha kwenda Cameroon, Mei mosi, mwaka huu ambako Mei 3, 2017 itacheza mechi ya kwanza na Cameroon kabla ya kurudiana Mei 6 na siku inayofuata itakwenda Gabon tayari kwenda kushindana.

Serengeti Boys imepangwa Kundi ‘B’ ikiwa pamoja na mabingwa watetezi Mali, Niger na Angola. Hali hiyo inafanya kundi kuonekana kuwa gumu.

1217 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!