Kujenga Tanzania: Nini kifanyike? (3)

Mwalimu pale pale Arnaoutoglou alisema – “Jeshi la Kujenga Taifa liko mfano wa Jungu Kubwa (Moulding Pot) ambamo vijana wa tabia na mienendo mbalimbali wanatakiwa kupikwa pamoja na kuundwa kuwa vijana wa Taifa moja lenye nguvu na wenye tabia na mwenendo sawa. 

Hiki ni chombo cha kuwatayarisha vijana kuwa na ARI YA KUJITOA siku zote, kwa nguvu zao zote kushiriki katika shughuli za kuendeleza Taifa hili changa. Kwa hali hiyo KILA KIJANA MTANZANIA alikuwa hana budi kupitia katika JESHI LA KUJENGA TAIFA! Jibu lile linatosheleza na linajieleza wazi.

Hapo tena pana swali juu ya ubaguzi? Mbona Baba wa Taifa keshatamkia vijana katika mkutano kuwa kila kijana hana budi kupita katika JKT! Hii kila kijana maana yake ni VIJANA WOTE sivyo?

Matokeo ya hotuba ile ya Mwalimu pale Arnaoutoglou, yalileta matukio kadhaa. Serikali mara moja ililifanyia kazi tamko lile la Rais kwa kurekebisha ile Sheria Na. 16 ya mwaka 1964 iliyoanzisha JKT. Bunge mwaka 1966 likapitisha sheria inayowabana wavulana na wasichana wote wasomi kuwajibika kulitumikia Taifa katika JKT kwa miaka miwili. 

Sheria mpya Na. 64 ya mwaka 1966 ilitungwa na Bunge nayo ilisema wazi wazi uwajibikaji wa wasomi wote katika nchi hii. Sheria yenyewe vijana wakaibatiza kwa jina la “Compulsory” yaani kuitwa kuwajibika kwa “Mujibu wa Sheria”. 

Sasa ubaguzi miongoni mwa vijana wasomi na wale wa darasa la 7 uliondolewa kwa sheria hii. Kila msomi mvulana/msichana ilimradi kahitimu elimu ya juu, kidato cha VI, chuo kikuu au chuo kingine chochote cha elimu ya juu alipaswa kutumikia Taifa kama wale vijana wa kujitolea katika kambi za JKT. 

Jambo jingine lililotokana na ile hotuba ya Mwalimu ni lile pale Mheshimiwa Edward Sokoine alivyoguswa na maelezo yale mbele ya mkutano wa TYL pale Arnaoutoglou. Mheshimiwa Sokoine akiwa Naibu Waziri wakati ule aliona vijana wake wa Arusha, Wamaasai na Wamang’ati watakuwa wamejibagua wasipopita katika JKT- lile jungu kuubwa la kuwafinyanga vijana wote wa Tanzania kuwa wa Taifa moja. 

Alichokifanya Mzee Sokoine ni kwenda Arusha mara tu baada ya mkutano ule. Huko alishauriana na uongozi wa mkoa – kwa maana ya Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha siku zile Mzee Mwakang’ata na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya TANU Mkoa Arusha, Mheshimiwa Ole Konchela wakusanye vijana toka mkoani wakawalete Mgulani JKT kujitolea kama vijana wa mikoa mingine. Hii ilikuwa kuondoa ubaguzi kimakabila. Na kweli Desemba 1965 hiyo hiyo wakaletwa vijana 60 Wamaasai na Wamang’ati kujiunga JKT. Wakaingizwa katika Operesheni Umoja (vijana waliojiunga kwa kujitolea tangu Novemba 15, 1965 waliitwa Operesheni Umoja. 

Kama wanavyoonekana katika picha hii vijana wamekamata “KITBAG” zao zenye zana zote za kuruta wa JKT, wako tayari kuanza mafunzo ya jeshi na wenzao katika Operesheni Umoja katika Kambi ya Mgulani, Dar es Salaam. 

 

Operesheni ile ilipata ‘volunteers’ wa kwanza waliohitimu kidato cha IV. Hivyo ukawa MSETO kweli – wasomi wa form IV, vijana wa Std VII na wasiojua kusoma wala kuandika kutoka Mkoa wa Arusha. Ndiyo kuthibitisha wazi ndani ya JKT hakuna ubaguzi wa elimu- wote ni vijana wa JKT tu wanalelewa sawa.

Hapa kihistoria nalazimika kuchombeza tukio jingine pale Mgulani Desemba ile ile ya 1965. Licha ya kuwa na vijana wa Operesheni Umoja, walikuwapo na Makatibu wa Wilaya wa TYL kwenye kozi maalum ya uongozi. Basi kwa kuguswa na ile hotuba ya Mwalimu pale Arnaoutoglou, Katibu Mkuu wa TYL, Elly Anangisye (Kidevu) na Katibu Msaidizi wa Mwalimu Nyerere katika Ofisi Kuu ya TANU Lumumba, Fortunatus Masha walisisimka wakajitolea kujiunga na yale mafunzo ya JKT hapo Mgulani. 

Huo ulikuwa ni uamuzi wa kishupavu kwa viongozi wakuu namna ile na waliweka mfano wa kuigwa katika kule kujitolea kwao kutumikia (kwa miezi mitatu) Taifa kama vijana.

Kuanzia pale kwa Mzee Sokoine kupata fursa kuwashirikisha vijana wa kutoka Mkoa wa Arusha ili wasiachwe nyuma katika hii huduma ya kizalendo kwa Taifa mpaka viongozi wakuu wa chama cha TANU wanasisimka na kuchangamkia ile fursa ya kulihudumia Taifa katika kambi za JKT, tujiulize moyo ule wa uzalendo upo pia kwa watoto wa yale makabila matatu ya ‘wakuja?’ Ni uelewa wa hali halisi katika kujenga UTAIFA wetu siku zile za mwanzo mwanzo za Uhuru wetu.

Ninajiuliza vipi viongozi wa yale makabila matatu la Wazungu, Wahindi na Waarabu wasifanye nao kama alivyofanya Sokoine siku zile? Waoneshe uzalendo nao walete wavulana/wasichana wao kujiunga katika JKT /JKU. Tueleweje, hawana mwamko au hawaoni njia ya kujichanganya na wazawa? JKT/JKU ni jungu kubwa (a moulding pot) la kuwafinyanga watoto wa Tanzania kuwa raia wazalendo wa Taifa hili (become NATIONALS). Kwani raia wenzetu (our fellow citizens) toka yale makabila matatu ya ‘wakuja’ (Wahindi, Waarabu na Wazungu) hawajawa na mwamko mpaka leo?

Kumbe Taifa letu mara baada ya Uhuru lilichukua hatua hizo nilizozieleza katika makala hii tangu mwaka wa kwanza wa Uhuru kuelimisha umma namna watoto wa nchi hii wanavyotarajiwa kulelewa ili kuunda Taifa tunalotarajia (psychological awareness kwa hotuba ile ya Mwalimu ya Desemba 10, 1962). “The Tanganyika we have to build kwa maneno yake Baba wa Taifa. 

Kule kuundwa kwa intergration committee, kule kuunda upya mfumo mmoja wa elimu; kule kubuni na kuundwa MANYATA YA TAIFA (JKT) yalilenga kuwandaa wananchi katika mageuzi makubwa katika Taifa letu. Baba wa Taifa alidhamiria kujenga Taifa moja lenye utaifa na uzalendo, lenye kufanya kazi yoyote ile kwa pamoja ili mradi kuinua uchumi wa nchi yetu na kulifanya lenye umoja na mshikamano wa kitaifa. 

Swali langu sasa ni je, tumefanikiwa kiasi gani katika azma hiyo? Utaifishaji wa shule na uanzishwaji wa JKT vimesaidia kiasi gani kujenga utaifa wetu? Isije ikawa utaifishwaji wa shule umeishia kwenye kubadilisha majina tu kutoka shule za Wazungu/Wahindi na za madhehebu, lakini tabia bado ni zile zile za ubaguzi wa mbari na dini?

Katika miaka 55 ya Uhuru je, tumeambulia tu kusema shule ya Wazungu ile ikiitwa St. Michael na St. George Iringa sasa ni mali yetu inaitwa Mkwawa. St. Joseph’s Convent tukiita shule ya Magoa sasa inaitwa Forodhani. Zile zilizokuwa zikiitwa shule za Ismailia tukiita H.H The Aga Khan Schools leo ni Shaaban Robert au Zanaki au Tambaza, zile Indian Schools leo zinaitwa Mzizima, Kisutu au Jangwani Girls wakati ile St. Mary’s School Tabora (alikofundisha Baba wa Taifa) sasa ni Milambo. Hayo majina hayatoshi kuonesha utaifishwaji wa shule za madhehebu na za mataifa zilivyoelimisha watoto wetu kupata Utanganyika. Je, wasomi wale Wahindi na Waismailia kutoka shule zile wamepikwa katika Utanganyika?

 

Mbona Wazungu, Wahindi au hata Waarabu hatuwaoni katika kambi za Kujenga Taifa au za Kujenga Uchumi? Sera yetu ya utaifishaji shule au ya uundaji wa JKT zimeshindwa wapi? Zimetuunganisha kutoka makabila hata tukaja kuwa wataifa?

Ieleweke huu ni mwaka wa 55 baada ya Uhuru je, tumepata Katibu Mkuu Mhindi/Mzungu au Mwarabu katika Serikali? Kwanini hawapo? Katika mikoa kuna ma-RAS wa mbari hizo? Kama hakuna, kwa nini hawapo? Baada ya kidato cha VI au vyuo vikuu hawa jamaa wanayeyukia wapi? Si wamesomeshwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania? Kama kuna dosari katika mfumo wetu wa malezi ya vijana tunasahihishaje? 

Chama na Serikali wameliona hilo? Mimi katika makala hii ninashangaa tu na ndipo ninauliza NINI KIFANYIKE ili taifa hili liwe moja na la raia WAZALENDO? Maoni na mawazo yenu wasomaji yanaweza kusaidia kulistua Taifa letu ili liongeze nguvu kuwafanya wananchi wote na wa rangi zote tuwe Taifa moja la Wazalendo – Watanzania. 

 

>>ITAENDELEA…

455 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons