Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Ni ukweli usiopingika kwamba kumekuwa na tatizo la mgawo wa umeme katika maeneo mbalimbali yaliyo katika Gridi ya Taifa katika siku za karibuni.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande, tatizo hili linatokana na sababu tatu. Kwanza, kuna matengenezo. Pili, kuna ukame na maji yamepungua katika kuzalisha umeme na tatu, mahitaji ya umeme yamekuwa makubwa kuliko uwezo. 

Maana yake ni kwamba wanajua sababu, hivyo hakuna haja ya kukata umeme bila taarifa na wangeweza kutoa taarifa kwa wakati ya wapi umeme utakatika, lini, saa ngapi na kwa muda gani ili watu wajipange. 

Hivyo ndivyo nchi zenye maendeleo zinavyofanya kukiwa na matatizo ya namna hii. 

Kama nilivyogusia, kimsingi, tatizo hilo linatokana na mambo matatu kwa pamoja.

Kwanza, ni tatizo la ugavi; kwamba kwa miaka zaidi ya minne Tanesco ilikuwa halifanyi matengenezo ya mitambo na hatua hiyo ilihitaji kuzima umeme kwa staili ya mgawo (yaani unazima eneo kufanya matengenezo ili mfumo ubaki kuwa thabiti).

Matokeo yake tukaishi kwa kuungaunga, maana fedha za matengenezo zinapelekwa maeneo mengine na kukata umeme unaogopa kwa sababu utafukuzwa kazi! 

Hata kuagiza vifaa vya matengenezo ilipigwa marufuku. Mfano, kulipuka kwa kituo cha kupooza umeme kilichopo Msamvu mkoani Pwani hivi karibuni ni matokeo ya kuwa na vifaa chakavu. 

Kama unatumia mfumo kwa muda mrefu bila kuufanyia matengenezo, ni wazi kwamba kuna siku utaleta shida hata kama ungekuwa ni mwili wako.

Si busara kuwasema watu waliotangulia mbele ya haki. Lakini kama Rais Samia Suluhu Hassan angesema aendelee na lile lililofanywa na Rais Dk. John Magufuli pale Tanesco, bila shaka kuna siku isiyokuwa na jina nchi hii ingeingia gizani moja kwa moja, tena huenda ingekuwa ghafla. 

Pili, ni ukame. Kwamba tumeelezwa kuwa maji yanapungua kutokana na ukame, na hii ni athari ya mabadiliko ya tabianchi. 

Inabidi tujipange. Kwa sababu tunapoelekea hali itakuwa ngumu si kwa upande wa umeme tu, ila miaka michache ijayo itakuwa katika maji, chakula, kilimo na mifugo. 

Wakati tunawaza maji ya umeme, pia tuanze kuwaza mapigano ya wakulima na wafugaji yatakayotokana na ukame. Tuanze kuwaza ajira zitakazopotea kwa kushindwa kwa kilimo. Tuanze kuwaza kupanda kwa bei za vyakula katika maeneo ya mijini. Pia tuanze kuwaza njaa itakayoyakumba maeneo ya vijijini.

Tatu, licha ya kukosekana kwa matengenezo ya mfumo wa umeme na kushuka kwa kina cha maji kutokana na ukame, kuna tatizo kwamba kwa miaka minne na zaidi wakati tunatekeleza ujenzi wa mradi wa Bwawa la Umeme la Stigler’s Gorge lakini hatujawekeza katika chanzo kingine cha ziada cha umeme.

Hapo tukumbuke kuwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imeongeza watumiaji wapya wa umeme karibu laki tano (bila chanzo kipya cha umeme). 

Vyanzo alivyoacha Rais Jakaya Kikwete ndivyo hivyo Magufuli amevitumia na huku kukiwa na wateja wapya karibu nusu milioni. Mfumo umezidiwa. Una umeme mdogo kuliko mahitaji. 

Kwa ufupi wakati tunaweka fedha katika ujenzi wa Stigler’s Gorge jambo ambalo ni zuri lakini tunaongeza wateja na mzigo katika Gridi ya Taifa, hatuukarabati mfumo na tunajua tunatumia maji yanayopatikana kwa msimu. Matokeo yake ni matatizo haya tunayoyaona.

Ushauri wangu. Wizara ya Nishati na Tanesco waendelee na marekebisho yote ya mfumo, si tu wa umeme bali pia wa watendaji. Mifumo ikae sawa.

Tanesco iweke wazi taarifa zake za kila siku ikiwamo upatikanaji wa umeme katika maeneo yote nchini ili watu wajue wapi na nini kinaendelea kufanyika.

Pia tumalizie ujenzi wa Stigler’s kwa sababu tumekwisha kuweka fedha nyingi na tupambane na tatizo la kuharibu mazingira, vinginevyo mradi huo hautaleta ufumbuzi, kwa kuwa bwawa la umeme bila maji ni shimo la taka tu na halitakuwa na maana.

Kwa upande mwingine, tumlilie Mungu, tuishi katika ukweli, nchi imekuwa na uongo mwingi. Kwa mfano, kuna sababu gani mwandishi wa taarifa rasmi ya Tanesco mapema katikati ya wiki hii kuhusu tatizo la umeme kuchukua nusu nusu kauli ya Chande?

Au watu mbalimbali kuichukulia kauli ya mtendaji huyo vipande vipande? Kwamba ni ukame tu badala ya kutaja sababu zote tatu kama ambavyo ameeleza?

Katika video yake anasema shida ni hizo tatu ambazo ni matengenezo, ukame na uwezo wa ziada ila ndani ya Tanesco wakaandika taarifa kwa vyombo vya habari bila kueleza kama bosi wao alivyosema. Kuna hujuma? Kwa nini? Kama ipo inafanyika kwa lengo lipi?

Inawezekana kabisa ipo hujuma inafanyika na hapa lazima tuwe makini na kwenda mbali zaidi kwamba hujuma hizi si kwa Chande tu au Waziri wa Nishati, January Makamba, ila ni hujuma dhidi ya Rais Samia. 

Tanesco inatumika kama njia tu. Ni wazi kwamba kuna hujuma kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa karibu na Magufuli, akiwamo waziri mmoja wa zamani aliyeondolewa na Rais Samia. 

Hawa walichota mabilioni ya fedha kupitia ‘single sources tenders’ na uzuri ni kwamba vyombo vya ulinzi na usalama tayari vinawatazama kwa karibu. 

Lengo lao wanajaribu kuonyesha Rais Samia hafai, hana uwezo. Uzuri ni kwamba hili walilionyesha katika kipindi cha mpito baada tu ya kifo cha Magufuli, kwa sababu baadhi yao walitaka Samia asiwe Rais na Katiba inajisiwe, ila vyombo ya ulinzi na usalama pamoja na jeshi letu makini vikaweka mguu chini na kuwaambia wasithubutu. 

Hawa ni watu waliokomba mabilioni ya fedha ila ‘system’ inawasitiri, na kimsingi ni wahaini pia (Rais Samia ana huruma kwa sababu tungeweza kuwa tunaongea lugha nyingine sasa hivi).

Ushauri wangu kwa kundi hili ni kwamba waamke mapema na kutembea kwa tahadhari. Mfano, kule katika mtandao wa YouTube kuna mtu mmoja yuko London, Uingereza ana televisheni mtandao.

Mtu huyo analipwa kabisa kufanya anayofanya na ushahidi upo akimnanga Rais Samia na watendaji wake kwa mambo ya hovyo na yasiyo na ukweli kila uchao akipitia mawaziri kama January. Ndani ya CCM pia wako vijana wanafanya aibu hii, tena wengine wakitumia rasilimali za chama ndani ya ofisi za chama. 

Tukimrejea January na kwa nini baadhi ya wana CCM na watu wa kundi hilo hapo juu wanamshambulia Rais na yeye, ni kwamba anaonewa kwa sababu ni mmoja wa vijana waliosukwa na mfumo kimalezi na kimkakati na anaonekana kama tishio kwa watu wa rika lake ndani ya chama hicho wenye ndoto za nafasi za juu za uongozi. Pia baadhi ya watu wa karibu na Magufuli wanaodhani ikitokea siku January akapata nafasi kubwa ya uongozi,  atalipa kisasi. Kwa hiyo wanamuona kama tishio kubwa. 

Ukinzani huu na kupigana mishale kwa waziri huyu si tu ndani ya CCM, bali pia kutoka upinzani, kwa sababu wapo watu ndani ya upinzani wanaomuona January kama ni kiungo kati ya CCM ya wahafidhina (conservatives) na CCM ya kizazi cha waliberali (liberals), hivyo kuwanyima wapinzani nafasi.

Hawa wanaona kama CCM ikiwa na mtu wa aina hiyo anaweza kuwavuta hadi wapinzani, hivyo ni vizuri kumshambulia mapema. Kwa hiyo chochote January atakachofanya lazima kitachukuliwa kwa uzito tofauti. 

Unaweza kujiuliza kwa mfano, kwa nini anashambuliwa zaidi January katika umeme kuliko Jumaa Aweso (Waziri wa Maji) kwenye maji wakati maji ni tatizo kubwa kuliko umeme kwa sasa? 

Au kwa nini January anashambuliwa kuliko Dk. Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha na Mipango) wakati bei za vyakula zimepanda kwa zaidi ya asilimia 10 katika kipindi cha miezi sita? Jibu unalo sasa hivi. 

Hii ndiyo sababu hata akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) bado alikuwa anaonekana. 

Mchambuzi mmoja wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akihojiwa na Citizen TV ya Kenya anasema: “For Honorable January Makamba, it was not about that particular portfolio but it was about what potential he has as a shining star within CCM and the country new way of doing politics. Therefore, anyone who wants to attack the future of CCM will ideally attack its possible future stars like him.” 

Mwelekeo mzuri sasa kwa mtu kama yeye na yeyote anayemsapoti ndani ya CCM kama vijana ni kuendelea na kazi na kuonyesha kazi zake.

Wakati ule wa Magufuli, January, hakupata mishale kwa sababu umma uliona anaonewa, kwa hiyo ukawa na huruma naye. 

Hata mahasimu wake vijana ndani ya CCM waliona ameshamalizika kisiasa na nyota imezimika, hivyo wakaona hana maana, badala yake wakamtumia Musiba kummaliza kwa propaganda kupitia gazeti lake hadi ikafikia mahali ikaonekana wazi alikuwa ametumwa. 

Alipo January sasa hivi pia kuna miradi mikubwa yenye fedha nyingi. Kwa mfano kule Stigler’s watu wa karibu na Magufuli wanatuhumiwa kusomba mabilioni ya fedha kutoka kampuni moja ya China ili wapate kazi. 

Pamoja na mambo mengine, watu wa karibu na January wanamjua kama mtu makini na asiyependa kona. Kama ameingia wizarani hapo na kufuta kula kwa watu, mishale atapigwa. 

Hii itaendelea hadi pale wakapojua kwamba mishale hiyo haitawarudishia kula kwao. Mkakati mzuri kwa January sasa hivi ni kutoafikiana nao na aendelee kukaza hicho anachofanya.

By Jamhuri