Kukojoa ni njia inayotumiwa na mwili kutoa takamwili mbalimbali. Ni muhimu kwa mnyama kukojoa kwa sababu kupitia mkojo mwili unatoa uchafu mwingi usiohitajika mwilini kama vile maji ya ziada yasiyotumika mwilini.

Pamoja na umuhimu wa kukojoa, kukojoa mara nyingi kwa mfululizo kunaweza kuashiria matatizo ya kiafya, hasa kwa wanawake.

Kwenda maliwatoni mara kwa mara, kutolala vizuri wakati wa usiku au kushindwa kwenda sehemu nyingine mbalimbali kwa kuhofia kukojoa mara kwa mara au mkojo kuvuja, ni baadhi tu ya matatizo ambayo kwa kawaida yanawasumbua sana wanawake wanaopitia hii hali ya kupata haja ndogo kila wakati.

Kila mtu anaweza kukojoa kwa idadi tofauti kwa siku, kutegemea kiasi cha maji anachokunywa lakini pia kutegemea na utendaji kazi wa figo zake. Tafiti za kisayansi zinaonyesha kuwa kwa mtu mwenye afya ana wastani wa kukojoa mara sita hadi mara nane kwa kipindi cha saa 24.  Hivyo, kukojoa kunakozidi idadi hii kwa mtu, kunaashiria tatizo.

Sababu na mazingira hatarishi

Wakati mwingine kukojoa mara kwa mara kulikopitiliza kunatokana na unywaji wa vinywaji vingi ambavyo vinasababisha msukumo wa uzalishwaji wa mkojo, au vinavyovuruga utendaji kazi wa kibofu.

Baadhi ya vinywaji hivi ni kama vile utumiaji wa ‘kafeni’ ambayo inapatikana kwenye kahawa, chai, na baadhi ya vinywaji vilivyosindikwa kiwandani. Hata hivyo kukojoa mara kwa mara kulikopitiliza kunaweza kusababishwa na matatizo fulani ya kiafya kama vile uwepo wa aina fulani ya mawe mawe kwenye kibofu (bladder stones).

Uwepo huu wa mawe kwenye kibofu unatokea wakati ambapo mkusanyiko wa mkojo ni mkubwa zaidi ndani ya kibofu au kama mtu ana upungufu wa maji mwilini (dehydrated) na hii inasababisha madini kama ya ‘calcium’ na madini ya chumvi yanajikusanya na kutengeneza haya mawe. Kisukari, matatizo ya homoni mwilini, maambukizi ya kwenye njia ya mkojo pia ni baadhi ya sababu zinazochangia kukojoa mara kwa mara kulikopitiliza.

Uzito uliopitiliza pia ni sababu zinazochangia matatizo ya kukojoa kupitiliza. Uzito ukizidi unaweza kusababisha mkandamizo kwenye kibofu, hivyo kudhoofisha mirija iliyopo ndani ya kibofu na hatimaye mkojo kutoka bila kujizuia.

Pia ujauzito unasababisha kwa kiasi kikubwa sana tatizo hili. Kadiri mimba inavyokua, mfuko wa uzazi nao unaongezeka ukubwa na kuleta mkandamizo kwenye kibofu, hivyo kusababisha kukojoa mara kwa mara kwa mjazito.

Ishara zinazoambatana na tatizo hili ni pamoja na kubadilika kwa rangi ya mkojo, mathalani kuwa mwekundu, kuvuja kwa kiasi kidogo cha mkojo bila kujizuia na hata kupata maumivu wakati wa kukojoa. Na uonapo ishara hizi ni vema kumuona daktari haraka.

Tiba

Ni muhimu kumuona daktari na kupata vipimo kwa wakati, kwa sababu aina ya tiba itatokana na sababu zilizochangia tatizo hilo. Kwa mfano, kama kisukari kitaonekana kuwa chanzo cha tatizo hilo, utapatiwa tiba itakayosaidia kuratibu kiasi cha sukari kwenye damu.

Lakini pia kama tatizo litaonekana ni maambukizi kwenye figo au kwenye njia ya mkojo ambalo hili ni tatizo linalowapata watu wengi sana, hususan wanawake, mgonjwa atapatiwa tiba ya dawa zinazopambana na maambukizi hayo ambazo kisayansi zinajulikana kama ‘antibiotics’.

Baada ya vipimo daktari atakupa aina sahihi ya ‘antibiotics’ kulingana na namna maambukizi katika njia yako ya mkojo yalivyo.

Lakini pia ni kupunguza utumiaji wa vinywaji kwa wingi hususan wakati wa kukaribia kulala au utumiaji wa vinywaji vya aina mbalimbali ambavyo huwa vinatibua utendaji kazi wa kibofu kama vile pombe na vinywaji vilivyosindikwa kiwandani, ambavyo vina sukari kwa wingi, ni tiba ambayo mtu anaweza kuifanya mwenyewe bila msaada wa daktari.

By Jamhuri