K

awaida hatimiliki (granted right of occupancy) hazitolewi kwa ardhi za vijijini. Ardhi za mijini ndizo zilizo na hadhi ya kupata hatimiliki. Lakini wapo watu ambao wamechukua maeneo ya vijijni kwa ajili ya uwekezaji.  

Wapo waliochukua ardhi kama wachimbaji wadogo, kilimo, madini, n.k. Hawa pengine wangependa wapate hatimiliki ili kukuza biashara zao sambamba na kupata faida zinazotokana na kuwa na hatimiliki. Moja ya faida ya kuwa na hatimiliki ni kupata mkopo. 

Swali ni, je, inawezekana kuipatia ardhi yako ya kijijni hatimiliki yenye hadhi sawa na ile inayotolewa kwa ardhi za mijini? 

1. Ardhi ya kijiji ni ipi

Sheria za Ardhi namba 4 na 5 kwa pamoja zimeainisha aina tatu za ardhi kwa hapa Tanzania. Kwanza ardhi ya jumla, ardhi ya hifadhi, na ardhi ya kijiji. Ardhi ya jumla (general land) ni hii ardhi ya mijini ambayo huwa na hatimiliki (right of occupancy). Hii ni asilimia 2 ya ardhi yote ya Tanzania.

Ardhi ya hifadhi (reserved land) ni kama mbuga, kingo za mito na bahari, makaburi, viwanja vya wazi n.k. Hii ni asilimia 28 ya ardhi yote. Ardhi hii huwa haimilikishwi labda isemwe vinginevyo.

Ardhi ya vijiji (village land) ni ardhi ya vijiji kama jina lake lilivyo. Sote tunajua vijijini ni wapi. Inachukua jumla ya asilimia 70 ya ardhi yote. 

2. Umiliki wa aina tatu wa ardhi ya kijiji

Ardhi ya kijiji – iwe kwa uwekezaji, makazi au vinginevyo – inaweza kumilikiwa kwa namna tatu tofauti kama ifuatavyo:

(a)Kumiliki kwa haki bila nyaraka yoyote ya umiliki (deemed right of occupancy). Kwa mtu anayewekeza kijijini huu si utaratibu mzuri kwake. Hapa mmiliki atamiliki ardhi kijijini bila kuwa na nyaraka yoyote inayomtambulisha kama mmiliki lakini hilo halitamwondolea uhalali wake katika kumiliki. Wamiliki wengi vijijni humiliki kwa mtindo huu. Wengi wana ardhi lakini hawana nyaraka yoyote kudhibitisha kumiliki. 

(b)Kumiliki kwa hati ya kimila (customary certificate). Sura ya 114 sheria na 5 ya 1999 ya ardhi ya vijiji inatambua uwepo wa hati za kimila. Hati hizi hutolewa na halmashauri za vijiji kwa utaratibu maalumu.

(c) Kumiliki kwa hatimiliki (granted right of occupancy). Hatimiliki hutolewa kwa maeneo ya mijini tu lakini hata vijijini zinaweza  kutolewa ikiwa ardhi inachukuliwa kwa ajili ya uwekezaji au shughuli nyingine za Serikali. 

4. Utaratibu wa kupata hati unaponunua ardhi ya kijiji kwa uwekezaji

(a) Kwanza miliki ardhi kijijini kwa kufuata utaratibu wote wa umiliki ardhi ya vijiji kama unavyoainishwa na Sheria ya ardhi ya vijiji, sura ya 114 pamoja na kanuni zake za mwaka 2001. Kwa ufupi uwe unamiliki ardhi ya kijiji kihalali.

(b) Baada ya hilo, utafanya maombi maalumu kwenda kwa Kamishna wa Ardhi makao makuu Wizara ya Ardhi ukiomba kupatiwa hatimiliki katika ardhi ya kijiji. 

(c)Katika maombi hayo utaambatanisha nyaraka zote za umiliki. Pia kama ni kampuni inayoomba au taasisi na si mtu binafsi, basi pia nyaraka za kuthibitisha usajili wake zitaambatanishwa.

(d)Kamishna ataangalia ikiwa kila kitu kinachohitajika kimefuatwa na ikiwezekana atawasiliana na uongozi wa ardhi wa kijiji husika ili kujiridhisha zaidi.

(e) Kama kila kitu kitakuwa vizuri, basi ardhi hiyo itabadilishwa kutoka ardhi ya kijiji (village land) na kuwa ardhi ya jumla (general land).

(f)Ikishakuwa ardhi ya jumla, basi Msajili wa Hati (Registrar of Titles)  anaweza sasa kutoa hatimiliki kwa mwombaji ambayo itakuwa na hadhi sawa na zile hati za mijini.

(g)Wakati mwingine ardhi iliyoombwa itamilikishwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) halafu kituo hicho ndicho kitakachompatia mwombaji.

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri