Nakumbuka nilipokuwa mtoto na baadaye kijana, nilielezwa na kufundwa na wazazi na walimu wangu shuleni niwe na ulimi fasaha na niogope, nitii na niheshimu mamlaka kuu tatu duniani, ili niweze kuchukuana na mamlaka hizo pamoja na walimwengu wanao nizunguuka.

Hadi leo nikiwa mtu mzima bado nakumbuka na kuzingatia maelezo na mafunzo hayo. Naamini mafunzo kama hayo yalitolewa kwa watoto na vijana wengine nchini. Ole wao! Ambao hawakubahatika kupata mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbsli. Si vyema kuzitamka hapa.

Nia yangu ni kukumbusha faida ya kupata na hasara ya kutopata mafunzo hayo. Na kabla ya kuangalia maana ya elimu hiyo nitoe maelezo mchache kuhusu Mamlaka kuu tatu ni zipi na ulimi fasaha ni upi.

Mamlaka kuu ya kwanza ni Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye wa kwanza kuogopwa, kutiiwa na kuheshimiwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuumba ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake na kuhuisha. Ni Yeye pekee yake mwenye kuamrisha jambo lolote liwe au lisiwe.

Mwenyezi Mungu ndiye anayekupa akili na fahamu, nguvu na ujasiri wa kutenda jambo na ndiye muumba mema na mabaya. Ni juu yako kila siku kutenda mema yakuongoze mahala pema na kuyaepuka mabaya ambayo yatakutia misukosuko na kukutupa mashakani.

Mamlaka ya pili ni Wazazi. Wao ndiyo wa kwanza katika kukupatia malezi bora, elimu, uchungaji na ulinzi mkubwa ili uwe mtoto mwenye adabu njema na heshima mbele ya mtu ye yote. Wazazi hufanya kazi hizo mchana na usiku kujenga nidhamu yako.

Mamlaka hii ya pili, hupata baraka zote kutoka kwa Mungu. Ni mamlaka inayosimamiwa na kuongozwa na mamlaka ya kwanza. Ndiyo inayotegemewa na mamlaka ya tatu katika kupokea watu (raia) wema na waadilifu. Ndani ya watu hao tunapata viongozi mbalimbali katika jamii.

Serikali ndiyo mamlaka kuu ya tatu yenye wajibu wa kupeleleza, kukamata, kuhukumu na kuadhibu raia ye yote atakaye kwenda kinyume na maadili ya jamii, kupitia mikono yake ya siri na ya wazi kama vile Takukuru, Polisi, Mahakama na Magereza. Mamlaka hii haina huruma (msamaha) kama zile mbili. Hii inajali na kuzingatia sheria tu.

Ama hakika ni mamlaka yenye mikono miwili ya ajabu; wa moto na baridi. Mkono baridi hulea mtu mtiifu na mnyenyekevu. Mkono moto hukamata mtu mkorofi na muovu. Ni mamlaka inayojaribiwa na vituko vibaya lakini haijaribiki. Inayopuuzwa lakini haipuuziki. Inatishwa haitishiki. Ni kali kuliko moto.

Mamlaka serikali ina tabia ya kumheshimu mtu anayetaka kuheshimiwa na kumdharau mtu anayetaka kudharaulika. Jamani! Serikali ni serikali hata kama ni ya kuku au ya siafu, bado ina sifa ile ile ya ukali, kutisha, kuogopwa, kutiiwa na kuheshimiwa. Kwa hiyo ni juu ya kila mtu kuwa macho.

Ulimi fasaha unakuchunga kutamka maneno mazuri, matamu na yenye ukweli na adabu mbele ya watu. Asili ya ulimi fasaha ni kutii maelekezo na mafunzo ya mamlaka hizo tatu. Kinyume cha kutotii maelekezo ya mamlaka hizo ni kukaribisha hadithi ya mtema kuni.

Wewe na mimi tumepata kuona na kusikia watoto wetu, ndugu, marafiki na viongozi wetu walioshindwa kutumia ndimi zao vizuri na kutotii mamlaka wametumbukia ndani ya hukumu na adhabu za mamlaka hizo..Hadi leo tupo tunaolia na kusikitika ndugu zetu wamo katika mkono moto wa serikali.

Daima tukumbuke utoaji wa kauli chafu, kuonyesha dharau kwa mamlaka husika, kutenda vitendo viovu, kutafuta sifa na kufurahisha watu ili hali unavuja sheria ni kujiingiza katika matatizo. Ni vyema na ni busara kutafakari kabla ya kutenda. Ni utajiri kupeleka vicheko nyumbani kwa kuepuka shari kuliko kupeleka umasikini nyumbani kwa kukabili shari.

Mtu anayefanya kiburi huwa kama pweza anayepalia makaa ya moto na kuungua. Unapotumia ulimi usio fasaha dhidi ya mamlaka kuu tatu hizo kufurahisha wapenzi, mashabiki au ndugu ni sawa na mshumaa unaowaka na kutoa mwanga kufurahisha jamii, kumbe wenyewe unawaka na kuteketea.

Ushauri wangu katika jambo kama hili linapotokea watu walio wajuzi na waliojaa hekima na busara hawashabikii na kulaumu, bali hutafakari na kuangatia; je, kosa la mtu lina kitovu cha sheria? Rejea maelezo yangu hapa.

By Jamhuri