Kwanini Bageni anyongwe peke yake kati ya watu 13? (2)

Toleo lililopita tuliishia aya inayosema: “Kwa msingi huu, Mahakama Kuu haikumuona Bageni akifyatua risasi, kwa sababu si yeye aliyefyatua risasi, hivyo upande huo akaondolewa, lakini pia haikumuona akiamrisha risasi kufyatuliwa, kwa sababu aliyefyatua hakuwapo mahakamani kumtaja kuwa ndiye akiyemwamrisha kufyataua, hivyo upande huo nako akaondolewa. Mwisho akaonekana haingii popote kwenye kosa, basi akachiliwa huru.” Sasa endelea…

Mahakama ya Rufaa

Mahakama ya Rufaa haikukubaliana na uchanganuzi huo wa Mahakama Kuu, hivyo ilimuona Bageni ana hatia. Ilisema ni kweli Bageni siye aliyefyatua risasi, lakini Kifungu cha 22 cha Kanuni za Adhabu kuhusu namna alivyotoa amri kinamuingiza hatiani.

Mosi, askari wote waliokuwa kwenye tukio yeye ndiye aliyekuwa na cheo kikubwa kuliko wengine hivyo ndiye aliyekuwa kiongozi anayetoa amri zote. 

Pili, walipowakamata wafanyabiashara ambao baadaye waliuawa katika Barabara ya Sam Nujoma, yeye ndiye aliyeamrisha msafara wa magari mawili Defender na Pajero kuelekea Msitu wa Pande (ushahidi wa mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari).

Tatu, mtuhumiwa wa 4, CPL Rajab Hamis Bakari anasema walipofika Msitu wa Pande, Bageni alishuka kwenye gari akamuachia radio call. Wakati amekaa ndani ya gari akiwa amebaki na dereva, alisikia kupitia radio call aliyoachiwa milio ya risasi. Ikabidi ashuke kuelekea Bageni alikoelekea. Alipowakaribia alimuona CPL Saad akiwa anamalizia kumpiga risasi mfanyabiashara wa mwisho, wengine wakiwa wameshauawa wamelala chini huku Bageni akiwa amesimama anatazama.

Nne, baada ya wafanyabiashara kuuawa, ni Bageni aliyeamuamrisha dereva Sgt James kubeba maiti na kuzipeleka Muhimbili (ushahidi wa mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari na Sgt James ).

Kwa mazingira haya, Mahakama ya Rufaa ikaona kwa vyovyote vile hata kama CPL Saad hayupo mahakamani kumtaja Bageni kuwa ndiye aliyetoa amri ya kuua, bado mazingira yote yanaonyesha yeye ndiye aliyetoa amri, hivyo kuwa na kosa sawa na CPL Saad  aliyekimbia.

Mahakama ya Rufaa ilizingatia haya kwa Bageni

Moja, kwanini Bageni aamrishe wafanyabiashara kupelekwa kwenye Msitu wa Pande, sehemu ambako hakuna nyumba wala kituo cha Polisi? Nia ya kuwapeleka huko ilikuwa nini? Jibu likawa ni mpango wa kuwadhuru tu bila shaka.

Mbili, Bageni alisema kuwa walikuwa wakijibizana kwa risasi na marehemu  maeneo ya Sinza kwenye ukuta wa posta. Ushahidi na mashahidi wote akiwemo shahidi wa 20, Kisa Mohammed – mlinzi wa ukuta huo wa posta alithibitisha kuwa hakuna majibizano yoyote ya risasi yaliwahi kutokea eneo hilo. Swali lilikuwa uongo huo ulitungwa kwa lengo lipi?

Tatu, Bageni alionyesha makasha  tisa  ya risasi na kusema kuwa makasha hayo yalitokana na risasi zilizotumika katika majibizano na wafanyabiashara waliouawa maeneo ya Sinza. Wakati ushahidi wa mtuhumiwa wa 4, CPL Rajab Hamis Bakari unaonyesha kuwa makasha hayo yalitokana na risasi zilizofyatuliwa ovyo hewani  maeneo ya Bunju  na zilifyatuliwa na CPL Saad na DC Rashid na baada ya kufyatuliwa  Bageni aliwaamrisha wamkabidhi makasha  hayo ambayo ndiyo aliwasilisha mahakamani.

Bageni aomba uamuzi wa kunyongwa kurejewa

Hii ndiyo ile ya juzi ambayo mlisikia. Basi ni hivi, Mahakama ya Rufaa ndiyo mahakama ya mwisho katika kutoa uamuzi. Hakuna rufaa nyingine, baada ya uamuzi wake inakuwa imetosha na imetosha. Umeridhika, haukuridhika, uamuzi ukitoka hapo biashara imekwisha.

Hata hivyo, Sheria ya Mamlaka za Rufaa, Sura ya 141 Kifungu cha 4(4), pamoja na Kanuni za Mahakama ya Rufaa za Mwaka  2009 , Kanuni ya 66(1)(a) (b)  zinatoa nafasi ya mwisho kwa mtu ambaye hakuridhika na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuomba marejeo.

 Marejeo ni maombi ya kuiomba mahakama ileile iliyotoa hukumu kupitia tena uamuzi wake ili kujiridhisha na nukta kadhaa ambazo muombaji atakuwa ameziainisha.  Utaiomba  mahakama chini ya majaji wengine tofauti na wale waliotoa uamuzi wa kwanza kurejea tena na kuangalia vile vitu ambavyo unadhani umeonewa.

Kwa ufupi majaji hawa walimsikiliza hoja zake kupitia kwa Wakili wake Gaudiosus Ishengoma, na wakasikiliza hoja kinzani kutoka upande wa serikali/Jamhuri uliowakilishwa na Wakili Ladislaus Komanya na kusema kwamba Bageni hana hoja za msingi na anacholalamikia hakina mashiko.

Kwa uamuzi huu majaji hawa Jaji Mugasha, Jaji Wambali na Jaji Kerefu wakakubaliana na uamuzi wa majaji wa mwanzo wa mahakama hiyohiyo;  Jaji Luanda, Jaji Mjasiri na Jaji Kaijage kuwa Bageni anastahili kunyongwa hadi kufa. Hivi ndivyo SP Christopher Bageni alivyobaki peke yake kati ya watu 13 alioshitakiwa nao.