Lissu Apanda Ndege, Apelekwa Ubelgiji

Ndugu, jamaa, marafiki na wabunge wakimuaga Lissu hospitalini hapo kabla ya kuepelekwa Ubelgiji.

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema) na Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Tundu Antipas Lissu ameondoka kutoka katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya leo Jumamosi saa 2:30 asubuhi na kwenda nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.
Lissu amepelekwa na Ndege ya Shirika la Kenya akiambatana na mke wake, Alicia ambapo amesindikizwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na watoto wake pacha, Augustino na Edward, ndugu zake, viongozi na wanachama wa Chadema.
 “Nawashukuru sana madaktari wa Nairobi Hospital na wale wa Dodoma wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Mpoki Ulisubisya waliookoa maisha yangu. Nakwenda Ubelgiji kwa matibabu, nikirudi mapambano yanaendelea, nawashukuruni nyote mlioniombea, nawashukuru Wakenya na serikali yao ambao kwa miezi minne nikiwa hapa walinipa ulinzi wakati wote. Chapeni kazi, mimi nitarudi kuendeleza mapambano haya,” alisema Lissu kabla ya kuondoka.

Mbunge John Heche (Tarime Vijijini), aklikuwepo kumsindikiza Lissu.

 Kuhusu gharama, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema gharama za safari na matibabu zimegharamikiwa na Chadema pamoja na TLS. Miongoni mwa waliokuwapo hospitalini kumsindikiza Lissu uwanjani hapo kaka yake Alute Mghwai, mdogo wake, Vincent Mghwai, Dk Mashinji, John Mnyika (Bara), Salum Mwalimu, Susan Kiwanga (Mlimba), Godbless Lema (Arusha Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Rose Kamili (Viti Maalum), Anna Gideria (Viti Maalum) na ndugu wengine.

Tundu Lissu akitolewa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa ajili ya safari ya kuelekea nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

 

Akizungumza kwa niaba ya familia, Alute amesema “Tunamwomba Mungu ajalie huko anakokwenda akapate matibabu, kwani alivyokuja hapa sivyo anavyoondoka na tunawashukuru wananchi wa Tanzania na Kenya kwa ushirikiano wao.”
Lissu ametoka hospitalini hapo ikiwa baada ya matibabu aliyoyapata tangu Septemba 7 mwaka jana baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana kwenye makazi yake Dodoma.