Luiza Mbutu aeleza siri ya kutozeeka

Luiza Mbutu wakati wote huonekana msichana kutokana na umbo lake dogo linalomtuma kunengua jukwaani.

Ni msanii wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, aliyejiongezea sifa lukuki kwa kujichanganya na wanenguaji wenzake jukwaani, sambamba na sauti yake nyororo anapoimba.

Licha ya umri mkubwa, wajihi wake hauonekani kuzeeka wala kuchuja. Anasema siri nyuma ya hali hiyo ni kutotumia vilevi pamoja na mazoezi ya kila mara.

Alianza kufahamika baada ya kuonekana kwenye runinga miaka ya tisini akicheza na kuimba pamoja na mwanamuziki Chemundugwao, wimbo wa ‘Tulitoka wote Mahenge.’

Wakati huo alijulikana kwa majina ya Luiza Nyoni, lakina baada ya kuolewa na Farijala Mbutu, muungurumishaji gitaa la besi, bendi ya Kilimanjaro Connection, akatambulika kwa majina ya Luiza Mbutu.

Alizaliwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam.

Alianza masomo katika Shule ya Msingi ya Mkamba, Kilombero – Morogoro, darasa la kwanza hadi la tatu.

Baadaye alihamishiwa Shule ya Msingi ya Mzinga, Morogoro mjini na kusoma hadi darasa  la sita. Alimalizia darasa la saba katika Shule ya Msingi Mushono iliyopo Arumeru, mkoani Arusha.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi aliendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Baadaye Mbutu alijiunga na masomo ya utunzaji wa stoo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam na kuishia kiwango cha Stashahada kutokana na changamoto ya ada.

Baadaye alijiunga na masomo ya Kompyuta katika Kituo cha Msimbazi, jijini Dar es Salaam, alikopata ujuzi wa kuandaa kurasa za magazeti.

Pamoja na hayo, fikra zake zilimuelekeza katika muziki na akajiunga katika masomo ya muziki yaliyokuwa yakitolewa na Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.

Hapo alisoma masomo hayo hatua ya kwanza hadi ya tatu, na akiwa darasa la nne akawa mwimbaji wa kwaya na aliendelea hadi alipojifungua mtoto wa kwanza, Brain.

Kwa sasa ameacha kuimba kwaya, lakini anasema anaweza kurejea.

Pamoja na kuanza kuimba muziki wa dansi mwaka 1997 katika bendi ya Magoma Moto, pia dada yake wa kwanza, Modesta Nyoni, aliimba kwenye bendi ya Kalunde inayoongozwa na Deo Mwanambilimbi.

Watoto hao wawili kati ya saba wa familia ya mwanajeshi Nyoni, ndio pekee waimbaji, lakini Modesta ana watoto wake Rose na Joseph, ambao wamerithi uimbaji wakifanya kazi katika hoteli tofauti.

Tangu alipojiunga Twanga Pepeta mwaka 1988 akitokea Magoma Moto Sound iliyokuwa ikimilikiwa na mwenye Hoteli ya Travertine, hajawahi kuhama.

Luiza anasema amebaini wenzake wengi ambao wamekuwa wakihama baada ya kipindi kifupi hurejea tena Twanga, na kwamba wanapohama hupoteza mashabiki na wengine kupotea kabisa katika tasnia ya muziki.

“Changamoto zipo kwenye bendi, lakini hupaswi kuzikimbia kwa kuwa hazikosekani hata kwenye nyumba tunazoishi, hiyo ndiyo siri ya kukaa Twanga Pepeta kwa miaka 20 mfululizo,” anasema Luiza.

Katika kuelekea onyesho la bendi hiyo – African Stars kutimiza miaka 20 ya mtindo wao wa Kutwanga na Kupepeta (Twanga Pepeta) lililofanyika Oktoba 20, 2018, Dar es Salaam, Luiza alikumbuka aliyowahi kuyashuhudia kwenye bendi hiyo.

“Kuna wenzetu wametangulia mbele ya haki, Mungu awape pumziko la milele,” anasema.

Pamoja na mafanikio yake, hakusita kuusifu uongozi wa Kampuni  ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET).

Lakini pia anazongwa na kumbukumbu za majonzi akisema: “Nakumbuka marehemu Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ aliondoka Twanga na kwenda TOT, wakati huo tulikuwa tunaandaa albamu ya pili ya ‘Jirani’, akahama, haikuwa vema japo alitupa funzo,”  anasema na kuongeza:  “Abuu Semhando alikuwa kiongozi, babu, meneja, katibu wa bendi aliyekuwa akituunganisha vizuri wanamuziki na uongozi wa bendi.”

Anasema hayo Luiza akimkumbuka Semhando aliyefariki dunia kwa ajali ya pikipiki akitokea kazini usiku wa manane Dar es Salaam.

Huyo ndiye Luiza Mbutu, ambaye hadi sasa hupanda jukwaani akiimba na kuwaongoza wanenguaji wenzake wakiwa wenye nyuso za furaha na bashasha tele.

litakuwa jambo zuri kwa kina dada wengine walio katika tasnia hiyo kuiga mfano wa Luiza kwa kutojihusisha na vilevi.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0713331200 na 0713331200.

572 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons