Luwongo alilia hati ya mashitaka

Khamisi Luwongo (Meshack) mwenye umri wa miaka 38, mtuhumiwa wa mauaji ya kuua na kumchoma moto mke wake, Naomi Marijani, ameendelea kufanya vituko mahakamani.

Vituko hivyo vilianza baada ya Wakili wa Serikali, Simon Wakyo, kuiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, chini ya Hakimu Salum Ally kwamba upelelezi unakaribia kukamilika, ndipo Luwongo akiwa ametoa kitambaa cha mkononi alichokuwa ametumia kuficha uso wake alinyoosha mkono akiashiria kutaka kusema jambo.

“Mheshimiwa hakimu, hii ni mara ya tatu ninaomba hati ya mashitaka sipewi, tarehe 13, 27 na leo naomba mbele yako ninahitaji hati ya mashitaka,” amesema Luwongo.

Wankyo akijibu malalamiko hayo alimwambia hakimu ni kweli hati hiyo haijamfikia, japo aliwaomba polisi watoe nakala wampatie pengine kwa sababu za kibinadamu haikuweza kumfikia mlalamikaji.

 “Leo nitampatia mimi mwenyewe hati hiyo mheshimiwa,” alisema wakili huyo wa serikali mbele ya Hakimu Ally.

Hakimu ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24, mwaka huu. Pia ameamuru Meshack apewe mara moja hati hiyo ya mashitaka.

Wankyo aliendelea kusema upelelezi ukikamilika utafikishwa mahakamani, lakini kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.

Wakati huohuo,  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mwanajeshi mmoja wa JWTZ na Polisi watano wamesomewa shitaka la uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Victoria Mwaikambo.

Akisoma shauri hilo, Wakili wa Jamhuri, Faraji Nguka, akisaidiana na Saada Mohamed, ameiambia mahakama kuwa watuhumiwa hao wameshitakiwa kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi.

Watuhumiwa hao ambao ni SGT Ally Chimwana, CPL Swahiba, PC Elidaima Paranjo, PC Simon, PC Dickson na PC Hamza, wamesomewa shitaka la kwanza ambalo ni kuongoza genge la kihalifu wakiwa bado ni watumishi wa umma.

Askari hao sita wametenda kosa la pili la kuiba lita 2,180 za mafuta ya ndege (Jet A-1/IK) yenye thamani ya Sh miliomi 4. 7. Mafuta hayo yaliibwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, ni mali ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

 Shitaka la tatu ni utakatishaji fedha kiasi cha Sh milioni 4.7 zilizotokana na shitaka la pili kati ya makosa yanayowakabili watuhumiwa hao.

Kosa hilo ambalo ni kinyume cha sheria ya mwaka 2006, kifungu cha 12, adhabu yake ni kutoa faini au kuhukumiwa kwenda jela.

Wakili Nguka amesema upelelezi bado unaendelea, hivyo watuhumiwa hawakuruhusiwa kujitetea kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kuendesha shauri hilo la uhujumu uchumi, isipokuwa kwa ruhusa ya DPP.

Kesi imeahirishwa hadi Septemba 24, mwaka huu itakapotajwa tena.