Kreta ya Empakaai

Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) ina eneo la ukubwa wa kilometa 8,300 za mraba – lenye mchanganyiko wa pekee wa sura ya nchi, wanyamapori, wanyama wafugwao na mambo ya kale.

Hifadhi hii ilianzishwa mwaka 1959 chini ya Kifungu cha Sheria Na. 413 kuwa eneo lenye kuhifadhi maliasili, kulinda mila na kuendeleza masilahi ya wenyeji wafugaji waishio ndani ya eneo, pia kukuza na kuendeleza utalii.

Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo pekee na maarufu katika Afrika kwa kuwa na matumizi mseto ya uhifadhi wa maliasili na watu waishio ndani ya hifadhi.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inasimamia eneo hili pamoja na rasilimali (mali zake). Imekabidhiwa kazi ya kutunza na kuendeleza kila kilichomo ndani ya eneo hili – kwa ajili ya binadamu wote wa Tanzania, Afrika na dunia. Kwenye nembo ya NCAA kuna mikono inayoishika. Hiyo inaashiria kazi za NCAA ambao ndio wasimamizi wa Ngorongoro.

Mambo au vitu muhimu katika Hifadhi ya Ngorongoro ni pamoja na Kreta ya Ngorongoro, Tambarare za Ngorongoro, Serengeti na Maasai Mara zenye idadi ya wanyamapori wengi wa aina kwa aina. Kuna Msitu wa Nyanda za Juu Kaskazini, maeneo ya Ikolojia ya Bonde la Olduvai  (Oldupai) na Alaitole.

Kwa umuhimu wake wa kuwa mseto wa binadamu, wanyamapori, misitu na mabaki ya viumbe wa kale, Hifadhi ya Ngorongoro imepewa hadhi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa Eneo la Urithi wa Dunia la Kimataifa.

Kreta ya Ngorongoro ina ukubwa wa eneo la kilometa 310 za mraba – likijumuisha miteremko mikali. Lina upenyo wa kilometa 14.5 hadi 19 na urefu kuanzia kwenye ukingo kwenda chini (sakafuni) ni wastani wa mita 610 hadi mita 760.

Kreta ya Ngorongoro ina aina nyingi za bionuai ya maliasili na wanyama wengi ambao kati yao 25,000 ni wale wanaokula nyasi, wengine zaidi ya 300 ni wanaokula nyama.

Eneo hili lina maji yanayotiririka kwenye mito, mifereji na chemchemi wakati wote wa mwaka – hali inayowafanya wanyama wasihame. Wanyama wakubwa wote – yaani tembo, nyati, simba, chui na viboko hupatikana.

Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambalo liko Kaskazini mwa nchi yetu ya Tanzania linaunda kitu kinachoitwa Jumuiya (Ecosystem) ya Serengeti – Ngorongoro na Maasai Mara (Kenya). Mpaka wa Mashariki unaunda Ukanda wa Mashariki wa Bonde la Ufa; wakati Ukanda wa Magharibi unaungana na Hifadhi ya Serengeti.

Upande wa Mashariki upo Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu kuliko yote barani Afrika, na mlima mrefu wa kwanza duniani kati ya milima iliyosimama pekee au kwa kimombo ni free standing mountain ukiwa na urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.

Inakisiwa kuwa miaka milioni 2 iliyopita eneo kubwa la sura ya nchi ya Hifadhi ya Ngorongoro imeundwa na mabadiliko kutokana na mmomonyoko na mabaki ya vitu mbalimbali. Sura na maumbile ya Hifadhi ya Ngorongoro ni muunganiko wa pamoja wa zamani za kale na hatua mbalimbali za jiolojia.

Milima ya Oldonyo Lengai (Mlima wa Mungu) imeenea hadi tambarare za Serengeti kwa miaka mamia kadhaa iliyopita. Wanasayansi wanakisia kuwa takriban miaka milioni 20 iliyopita Ukanda wa Mashariki mwa Afrika ulipasuka na kusababisha ardhi hiyo kutofautiana na nyingine ikiwa juu na nyingine chini bila kuachana.

Katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro volkano zilizokufa ni Legamat, Sadman, Oldeani, Ngorongoro, Olmoti, Loolmalasin na Empakai. Hizi zimeundwa kwa pamoja na Ufa wa Eyasi. Aina ya uji uliotokana na volkano uligeuka na kuwa mgumu na baadaye kudidimia wakati ambao miamba iligawanyika na kuunda Bonde la Ngorongoro (Cardera) inayoonekana leo.

Hii Cardera wengine huiita Kreta (Crater). Kreta za Olmoti na Empakai kwa pamoja zilididimia katika muundo sawa ingawa si mkubwa kama ilivyo kwa Bonde la Ngorongoro. Mlima wa Oldonyo Lengai bado unalipuka hadi leo kwa nyakati tofauti, hii ikimaanisha kuwa volkano yake ingali hai.

Kreta ya Ngorongoro ni mfano mzuri wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Kuna misitu katika milima inayoizunguka kreta hii hadi kwenye mbuga pana. Ndiyo maana ulimwengu umetambua upekee wa eneo hili na kuliweka kwenye orodha ya Urithi wa Dunia likiwa na maajabu mengi.

Pamoja na Olduvai ambako ndiko kwenye chimbuko la binadamu wa kale (tutatazama kwenye makala zijazo), pia kuna eneo la Laetoli ambalo kuna nyayo za binadamu wa kale. Wataalamu wameweza kugundua namna binadamu na wanyama walivyoishi miaka milioni kadhaa iliyopita.

Ng’ombe ndiyo anayetumika kama alama ya NCAA kuonyesha maisha ya wafugaji wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi. Hifadhi ya Ngorongoro si Hifadhi ya Taifa, bali ni sehemu maalumu yenye maisha ya watu na wanyamapori. Wajibu wa NCAA ni kutunza haki na maendeleo ya watu wanaoishi ndani ya eneo hili pamoja na mazingira ambayo kwa hakika ni maajabu ya Mwenyezi Mungu.

1333 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!