Mabula atoa onyo kwa viongozi wanaochochea migogoro ya ardhi

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Bagamoyo

WAZIRI wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi Angelina Mabula ametoa onyo kwa baadhi ya Viongozi wa ngazi za vijiji na vitongoji wanaokuwa chachu ya migogoro kwa kuuza ardhi zaidi ya mara moja ili kujinufaisha matumbo yao hali inayosababisha ongezeko la migogoro ya ardhi.

Vilevile ameeleza,Mkoa wa Pwani ni mkoa wenye fursa nyingi za kimaendeleo na kiuchumi lakini changamoto kubwa ni migogoro ya ardhi, ambayo inapaswa kuvaliwa njuga ili kupata ufumbuzi.

Waziri Angelina ametoa onyo hilo mara baada ya kuwakabidhi ripoti Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdallah ripoti iliyoandaliwa kuhusu migogoro ya ardhi ya kata ya Mapinga ili iweze kufanyiwa kazi.

Amewaasa viongozi wote wa vijiji na vitongoji kuacha mara moja kujivika mamlaka kinyume na taratibu za sheria na wanatengeneza miliki bandia ili kujipa kipato.

Ameendelea kusema ”uvamizi wa ardhi ni uhalifu kama uhalifu mwingine hivyo hawatakuwa tayari kuona shamba la mtu linavamiwa kisa ni shambapori.”

Pia Mabulla ameshauri wananchi kutokufanya maamuzi ya haraka bila kufika Halmashauri husika na kufuata taratibu.

Nae mwanakamati Peter Richard Matagi kiongozi mkuu wa tume iliyoundwa kwaajili ya kuandaa ripoti na kushughlikia migogoro hiyo alipata fursa ya kuwasilisha mrejesho mfupi kuhusu agizo walilopewa na Waziri kuhusu migogoro ya ardhi ikiwemo baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji kutumia mamlaka zao Kuwa chachu ya vyanzo vya migogoro ya ardhi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amepokea ripoti hizo na kuwasisitiza wananchi wa Mapinga kuwa makini na wasikubali kupewa suluhisho kwa mdomo bali masuluhisho yawe kwa maandishi.

Kunenge amewatoa hofu wananchi wa kata ya Mapinga na kuhakikisha analibeba tatizo linalowakabili,“niwahakikishie Ili si la mkuu wa Wilaya bali la kwangu ”amesema Kunenge.

“Kuhusu suala la haki “watu wengine kwa makusudi wanakuja kuleta kero bila sababu kwa kutokuzingatia sheria hakuna aliyejuu ya sheria ”Mhe. Waziri nikuhakikishie watu wawe na utulivu nitapitia na tutaona mapendekezo tofauti na tutaangalia njia bora zaidi ya kutatua haki ya watu haitapotea ” amesema Kunenge.