Mabwawa ‘hewa’ ya Sh milioni 720 yachimbwa

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisitofautiane na wenzangu wote waliozungumza.
Hali ya Serikali yetu kwa ujumla kwa matumizi ya fedha ni mbaya na wengine wanafika mahali kwamba Serikali hii sasa, hasa kwenye matumizi ya fedha za Serikali, imebaki kuwa kama shamba la bibi. Ni kama shamba la bibi maana bibi akiwa na shamba lake hata wezi wakiingia hana nguvu za kuwafukuza, ndiyo ilivyobaki Serikali ya kwetu sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu taarifa hizi zote waheshimiwa wabunge mmezisikia na wala Serikali wasiseme hapa tunawaonea, tunasema kweli. Kila Mwenyekiti aliyesimama amelalamikia matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Hivi mimi nashangaa kuna sababu gani ya kuunda ofisi kubwa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na kutumia pesa nyingi kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa hesabu za Serikali za Mitaa, POAC na Serikali Kuu na anakwenda hadi balozi za nje.  

Wanatumia fedha nyingi sana na wanatoa taarifa nzuri sana ambazo zina mapendekezo, zinaletwa hapa bungeni, zinakaliwa hazifanyiwi kazi yoyote. Ina maana gani ya kuendelea kuwa na ofisi ya CAG?

Mimi nadhani tuifute tu maana kwa kufanya hivi tunamkatisha tamaa CAG katika kufanya kazi hii. Si tu tunamkatisha tamaa, lakini pia ni matumizi mabaya ya fedha za walalahoi – wananchi wa Tanzania – kwa sababu ni kodi zao zinazofanya ofisi ya CAG waende kufanya kazi hii nzuri wanayofanya, ambayo kazi yenyewe hiyo Serikali haitaki kuipa umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani Mheshimiwa Rais kama anatusikia ana sababu ya kufanya mabadiliko makubwa tu ndani ya Serikali yake, maana yake kwa mwendo huu hatuwezi kufika.

Lakini pia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ijue kwamba hii ni ‘advantage’ kwa vyama vya upinzani, maana tunafanya makosa wanakwenda kwa wananchi kwenye uchaguzi wanayasema haya haya na wananchi watayasikia.

Serikali inaacha kuhangaika na watendaji, wamenyamaza, limebaki shamba la bibi kama nilivyosema na Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Mrema asubuhi, kwamba nchi hii itajengwa na wenye moyo na itaendelea kuliwa na wenye meno, ndiyo hivyo sasa hivi tunavyoendelea katika nchi hii, ndiyo ilivyo!

Hivi, kwa mfano, kitabu cha hesabu kuu ambacho kimesomwa na Mheshimiwa Cheyo asubuhi matumizi ya fedha ambayo na wenzangu wamezungumza katika ukurasa wa 15, matumizi mabaya fedha za Serikali Sh 50,685,371,565.58, sasa mimi nashangaa kama kuna idara ambazo zimetumia fedha hizi vibaya wakuu wa idara hizo, mawaziri wa wizara hizo wanafanya nini mpaka sasa?

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya ‘special audit’ Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Niwaambie yaliyokutwa pale… Sh bilioni sita zimetafunwa na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Niwaambie matumizi mabaya yalivyo kwa ufupi sana. Kughushi kwa salio katika akaunti Sh milioni 235, hundi zilizoghushiwa na kulipwa zaidi ya vibutu katika akaunti za CHC Maendeleo, EGPF, TACAIDS na DASP (Sh milioni 500), fedha zilizohamishwa bila idhini ya Mkurugenzi na kutumika kinyume na malengo (Sh bilioni 1.6).

Uhamisho wa fedha ambazo hazikufika kwenye akaunti husika (Sh bilioni 1.9), uhamisho wa fedha kwenye akaunti zisizofahamika (Sh milioni 452), malipo yaliyofanyika kwa walipwaji wasiofahamika (Sh milioni 689), fedha ambazo hazikuhamishwa kutoka akaunti ya maendeleo kwenda akaunti ya maji (Sh milioni 88), matumizi yaliyofanywa kinyume na malengo katika akaunti ya maji (Sh milioni 338).

Si hayo tu kuna fedha ambazo hazikuhamishwa kutoka akaunti ya maendeleo kwenda akaunti ya Mfuko wa Afya wa Pamoja (Sh milioni 244), fedha ambazo hazikuhamishwa kutoka akaunti ya maendeleo kwenda akaunti ya TACAIDS (Sh milioni 53), na matumizi ya fedha ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) yasiyoidhinishwa (Sh milioni 126). Jumla yake ni Sh bilioni 6.7. 

Hawa wakurugenzi wamefanya makosa haya kati ya mwaka 2007 na 2008 na hadi leo wapo kazini… Bajeti ya Serikali zaidi ya asilimia 60-65 yote inaenda kutumika kwenye halmashauri zetu katika nchi hii. Sasa kama halmashauri moja inaweza ikawa na matumizi mabaya ya Sh bilioni sita si hatari hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwa utaratibu huu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi tukishinda mwaka 2015 tumshukuru Mungu. Lakini tukishinda mwaka 2015, mwaka 2020 kama ‘business as usual’ sijui kama tutakwenda.

Matumizi mabaya ya hesabu za Serikali, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali walisema wenzangu Sh bilioni 49 matumizi mabaya na yasiyoeleweka ya fedha za Serikali.

Sh bilioni 49 na hii ndiyo Idara ya Mhasibu Mkuu wa Hesabu za Serikali, hivi huyu Mhasibu wa Hesabu za Serikali hadi leo yuko ofisini? Hadi leo yuko ofisini huyu? Serikali inafanya uchunguzi, inafanya utafiti, baadaye watatuambia mchakato unaendelea wa kuangalia kama ana makosa au hana makosa.

Eeh! Lakini Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Sh milioni 320 watu wako kazini. Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza (Sh milioni 54), Wizara yenyewe ya Fedha ya Mheshimiwa Mkulo anayetutunzia fedha zetu (Sh milioni 373) bado na wao wako ofsini.

Lakini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (Sh milioni 212), Tume ya Kudhibiti Dawa (Sh milioni 40), Idara ya Magereza (Sh milioni 358)… jamani hii nchi kweli ipo hivi? Nchi ipo kweli hapa? Hatuwezi kwenda.