Madai ya Tundu Lissu yachunguzwe

Katika gazeti la leo kuanzia ukurasa wa kwanza tumechapisha ripoti maalum yenye kuonyesha hali ya wasiwasi katika muhimili wa tatu wa dola uliokasimiwa jukumu la msingi la kutoa haki. Wasiwasi huu umeibuliwa na taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge.

Lissu ameonyesha jinsi taratibu za uteuzi wa majaji zilivyokiukwa. Ameonyesha kwa majina majaji zaidi ya 11 walioongezewa muda wa utumishi kinyume cha sheria. Ameonyesha bila kificho msimamo wa Timu ya Wataalam kutoka Ikulu dhidi ya kuongeza muda majaji Wastaafu na msimamo wa aliyekuwa Jaji Mkuu, Agustino Ramadhani juu ya kutoongeza muda wa utumishi kwa majaji. Kwa kuongezewa muda baada ya kustaafu kila hukumu wanayotoa majaji hawa, kisheria inakuwa batili.

 

Ukiacha hilo, Lissu amegusia hoja muhimu ya uadilifu kwa baadhi ya majaji walioteuliwa kushika wadhifa huo unaoendana kimamlaka na Mungu kwa hapa duniani. Huyu ni mtu anayepewa fursa ya kutoa hukumu ya kuondoa uhai wa mtu bila yeye kuhukumiwa kuwa ameshiriki katika mauaji kazi ambayo Mungu pekee alipaswa kuifanya.

 

Ameeleza majaji wapya walivyoteuliwa ilhali uadilifu wao ukitililiwa shaka kuwa ama walikuwa na upendeleo katika kushinikiza ndugu zao wapewe hukumu zenye upendeleo au walikuwa wakituhumiwa ndugu au jamaa zao kuchukua rushwa kwa malengo yanayoweza kudhaniwa kuwa wamewatuma wao. Si hilo tu, baadhi ya majaji wamekuwa mawakili na kushinda kesi katika mazingira yenye kuashiria mizengwe na kusababisha baadhi ya mahakimu kuadhibiwa.

 

Tuhuma kama hizi zinapotolewa kwa muhimili muhimu kama Mahakama, sisi tunadhani si za kufumbia macho. Kama nchi tunaweza kuendelea na siasa za maji taka kama tulivyozoea kwenye ukumbi wa bunge na nyumba za ibada, lakini hatuwezi kuruhusu watu wasio waadilifu (kama ni kweli tuhuma dhidi ya majaji hawa ni za kweli) wakasimiwe kazi ya kutoa haki.

 

Kama ni kweli, hawa wanaotuhumiwa leo kuwa walikuwa wanashinikiza mahakimu wakazi, walikuwa wanawaelekeza mahakimu jinsi ya kuandika hukumu zenye kutoa upendeleo waliweza kufanya hivyo wakiwa na mamlaka kidogo, je, kwa kupewa ujaji ambao uteuzi kuufuta ni kazi ngumu kwa mujibu wa katiba watafanya fujo kwa kiwango kipi katika mahakama zetu?

 

Sisi tunasema Bunge linayo haki kwa mujibu wa kifungu cha 100 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) kufanya jambo lolote. Ingawa si haki kuingilia mihimili mingine, tunasema Kamati ya Bunge ikijiridhisha kuwa Lissu hakughushi taarifa hizi, basi iundwe Kamati Teule ya Bunge, ichunguze taarifa hizi na kuanika ukweli. Kisha zikiishawekwa wazi, Watanzania ambao ni waajiri wa Rais Jakaya Kikwete kupitia wabunge wao wamtake Rais kuanzisha uchunguzi kwa mujibu wa sheria.

 

Pia tunasema kinyume chake iwe sahihi. Bunge pia katika uchunguzi wake likibaini kuwa Lissu amegushi katika taarifa hii, itatupasa kuweka historia kwa kutumia Sheria ya Adhabu ya Viboko ya Mwaka 1989, inayozuia mtu (hata mbunge) kuzusha jambo lenye kuleta hofu isiyo ya lazima katika jamii. Kwa vyovyote kama taifa ikiwa tunataka mahakama iendelee kuaminiwa ni lazima sasa uchunguzi rasmi juu ya suala hili uanze.

468 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons