Natoa kongole kwa madereva wa bodaboda wa kituo cha Mbuyuni, Tegeta, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, kwa uamuzi wao wa kudhibitiana na kupangiana utaratibu mzuri kutii na kufuata Sheria za Usalama Barabarani, kama walivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini, wiki iliyopita.

Katibu wa Waendesha Bodaboda wa Kata ya Wazo, Stephen Ndelekwa, amekaririwa akisema kuwa mwendesha bodaboda atakayefika eneo hilo bila ya kuwa na kofia ngumu mbili – ya kwake na abiria wake – bodaboda hiyo itafungwa minyororo isitembee. Lengo la kufanya hivyo ni kusaidia Jeshi la Polisi kukabiliana na madereva wa vyombo hivyo wanaovunja sheria za barabarani.

Huo ni mwanzo wa mwendelezo maridhawa kwa madereva hao kujitambua kwamba wana dhima na dhamana, na ni wajibu wao kulinda usalama wao na wa abiria wao wanapokuwa safarini. Lakini uamuzi huo usiishie tu kwenye kofia ngumu, uendelezwe kwenye usalama wote wa barabarani.

Hizo kofia ngumu zisivaliwe kama pambo au kudanganya polisi wa barabarani kwa sababu zinaegeshwa juu ya nywele bandia za akina mama, na hata mkanda haufungwi. Aidha, baadhi ya kofia ndani ni chafu na abiria wengine wanakataa kuvaa wasije kupata magonjwa ya ngozi na n.k. Ipo haja kuangalia afya za abiria.

Tunashuhudia bodaboda zinapakia abiria zaidi ya mmoja; wawili, watatu, wanne hata watano (mshikaki), lakini kofia ni mbili tu. Kati ya abiria hao wamo watoto wa shule na pengine mama na mtoto wake. Hili nalo tunaliwekaje katika usalama wetu? 

Baadhi ya madereva wa bodaboda huendesha pikipiki kwa mwendo kasi, nao ni vijana wenye umri chini ya miaka 18 na wapo vituoni. Wakiwa barabarani hawafungi breki, breki zao ni kupiga honi kukutisha umpishe apite. Hata kama yupo nyuma ya gari hazingatii indiketa ya gari wala hapunguzi mwendo.

Yapo mengi ya kulaumu na ya kusifu kwa madereva wa bodaboda. Hilo siyo lengo. Upo ukweli; bodaboda zinasaidia sana kusafirisha abiria kwa muda mfupi sehemu za mjini ambako kuna misururu ya magari. Huko vijijini bodaboda zinafika mashambani, mabondeni na vilimani ambako magari hayawezi kufika.

Napenda kusema madereva hawa wasijitambue tu katika kuvaa kofia ngumu. Wajitambue wao ni nguvukazi ya Taifa, wahisani wakubwa wa abiria na wajenzi wa familia wanapofanya kazi zao kwa ueledi na usalama. Wajitambue wao ni walezi wa watoto wetu wanapowapeleka shuleni na wasaidizi wa polisi katika kuokoa mali za raia zinazoporwa na majambazi.

Wanapochunga usalama barabarani wanakinga ajali zisitokee na hivyo wanapunguza majeruhi, vilema na wafu hospitalini na kuondoa huzuni, umasikini na ukiwa kwa watoto, ndugu na marafiki. Wasipozingatia mtaji huu wa usalama barabarani hatuwezi kujenga Taifa lenye uchumi imara.

Kituo cha bodaboda Mbuyuni, Tegeta kiendelee kubuni mbinu nyingine za kudhibiti ajali holela za pikipiki. Si Tegeta tu, vituo vingine vya bodaboda nchini viige mfano huo na kuweka mipango  mizuri ya kukwepa ajali za barabarani. Usalama barabarani kwanza kabla ya kuendesha chombo.

Madereva wote mkifanya hivyo mtakuwa marafiki kwa abiria na polisi wa barabarani katika kufuata sheria za usalama barabarani. Hili ni jambo linalowezekana huko vituoni. Mkichelea mwana kulia, mtalia wenyewe na kutuingiza sisi abiria katika umasikini na ukiwa. 

Ushauri wangu; viongozi wa vituo vya bodaboda nchini kote, wekeni kanuni zitakazowaongoza kufanya kazi zenu kwa ueledi na kuwajengea uhusiano mzuri baina yenu na polisi na abiria. Daima kuiga na kujaribu ni mafanikio kwa mtu yeyote anayeiga.

By Jamhuri