IMG_4376 copyTuhuma za ukwepaji kodi za Serikali na uonevu dhidi ya wafanyakazi zimeendelea kuibuliwa dhidi ya kampuni ya utalii nchini ya Leopard Tours yenye makao yake jijini Arusha.

Kampuni hiyo inatajwa kuwa ni nambari wani kwa ukubwa na usafirishaji wageni katika hifadhi na mapori mbalimbali nchini. Inakisiwa kuwa na Land Cruiser zaidi ya 280.

Nyaraka ambazo Gazeti la JAMHURI zimelipata zinaonyesha kuwapo kwa ukwepaji kodi uliokithiri kupitia mianya kadhaa, lakini mwanya mkubwa usiotiliwa shaka ni wa udanganyifu kwenye mishahara ya wafanyakazi.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa katika benki moja ambayo kwa sasa jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, Leopard Tours wamekuwa wakiingiza mishahara ambayo kiwango chake kinatofautiana mno na kile kinachosainiwa na kupokewa na waajiriwa dirishani.

Imebainika kuwapo kwa wafanyakazi wanaolipwa hadi dola 1,000 (Sh milioni 2.2) kwa mwezi, lakini hawakatwi chochote kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, na pia hawakatwi kodi.

Kwa mfano, mmoja waliokuwa wafanyakazi mwenye jina la Kivuyo, katika bank statement inaonyesha kuwa Leopard Tours wanamwingizia Sh 600,000 kama mshahara wake kwa mwezi, lakini kwenye nyaraka za ofisini kwa Fazal, mshahara wake anaosaini ni Sh 150,000.

Kiasi hicho kinakatwa Sh 15,000 kwa ajili ya NSSF na yeye anabakiwa na Sh 135,000. Kwa mbinu hiyo, Leopard Tours wamekuwa hawalipi kodi serikalini ya P.A.Y.E kwa kuwa kiwango cha chini kilichoidhinishwa kisheria kukatwa kodi ni Sh 170,000.

Mtumishi mwingine, Salum Said Mohamed, kuna habari kuwa alilazimishwa kuandika barua ya kuacha kazi wakati huo akiwa analipwa Sh 600,000 kwa mwezi.

Kama ilivyo kwa Kivuyo, naye alifanyiwa ‘mchezo’ kama huo. Aliajiriwa mwaka 2008, lakini nyaraka zinaonyesha kuwa fedha zake za NSSF zilianza kuwekwa mwaka 2011. Ushahidi mwingine wa kuthibitisha madai hayo ya ukwepaji kodi yako kwa mtumishi mwingine, Oswald Kimolo. Kwa jumla wafanyakazi wote, wakiwamo madereva wanaofikia 300, mtindo wa malipo na ukwepaji kodi ni huo huo.

“Suala la Leopard Tours kuhusu kodi liko wazi, sisi hapa TRA hatuwezi kulishughulikia kwa sababu mtandao wa wake ni mkubwa sana hapa Arusha, labda kama inawezekana waje wakaguzi kutoka Dar es Salaam,” kimesema chanzo chetu ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Arusha.

 

Madai ya unyanyasaji

 Watumishi wanalalamika kunyanyaswa na uongozi wa Leopard Toures kwa masuala mbalimbali. Ufuatao ni baadhi ya ushuhuda walioutoa kwa JAMHURI walipohojiwa.

 

Pancha 

“Ni jambo la kawaida kwa gari kupata pancha, ila katika kampuni ya Leopard ikitokea pancha ni lazima dereva atalipishwa tairi jipya kwa kukatwa katika mshahara wake gharama ya kununua tairi jipya.

“Cha ajabu ni kwamba hata ukilipishwa tairi jipya, lile la zamani ambalo unaambiwa umeliharibu hupewi, wanalichukua wao na kwenda kwa dealer aliyewauzia kudai walipwe jipya.

“Huu ni unyanyasaji, na bado ukidai risiti ya ulichokatwa au kulipia hupewi,” anasema mmoja wa madereva.

 

Vioo vya gari

 “Kutokana na field yetu huwa tunapita barabara mbaya, mfano ukipishana na gari lingine porini kwa bahati mbaya hilo gari likarusha jiwe na kukuvunjia kioo ni lazima utalipishwa kioo kipya- utake usitake. Fazal atamwamrisha Mhasibu Mkuu, Joel Mmbaga, akukate kwenye mshahara. Shock absorber, spring vikivunjika dereva analipa,” amedai dereva mwingine.

 

Ajali

Dereva mwingine anasema: “Kitu cha ajabu na cha kusikitisha ambacho kinatuuma ni pale inako imetokea ajali barabarani- iwe umesababisha dereva au gari jingine limekugonga wewe, ni lazima utalipishwa gharama zote za kulitengeneza hilo gari bila kujali kama hilo gari lina bima, ndiyo maana magari ya Leopard mengi yana bima ndogo maana wanajua kuwa litakalotokea dereva atalipa. Akikataa atawekwa rumande au kufukuzwa.

“Wapo madereva wenzetu waliofanyiwa haya, na ushahidi upo, lakini tunamwonyesha nani ambaye ataweza kusimamia haki na kututetea sisi madereva?

“Kwa mfano dereva anayeitwa Frank Mollel aligongwa gari lake. Baada ya kupimwa ajali alipelekwa polisi, ingawaje yeye ndiye aliyegongwa; ila yeye ndiye aliyewekwa rumande kwa amri ya Fazal.

“Kesi ilipelekwa mahakamani akapigwa faini na kesi ikaisha ila cha ajabu huyu dereva aliporudi kazini alikutana na invoice ya kutengenezea gari. Akatakiwa alipe. Ushahidi upo.

“Kuna dereva mwingine anayeitwa Mzee Lyimo, alipata ajali Musoma kwa kugongwa na basi nyuma na wageni wakafa, ila alitakiwa alilipe hilo gari na akafukuzwa kazi.

“Silva Justine akiwa safarini mbugani na wageni aliugua ghafla usiku saa 6, ikabidi atumie gari analoliendesha la kampuni ili aende kutafuta matibabu hospitali ya karibu na Serena (Manyara)- umbali kaka kilometa 3 kwenda na kurudi.

“Aliporudi ofisini aliadhibiwa kwa ‘kosa’ la kutumia chombo cha kampuni kwa matumizi yake, na alikatwa kwenye mshahara wake dola 150 kwa sababu analipwa kwa dola za Marekani,” kimesema chanzo chetu.

Viambatanisho vya madai na malipo ya fedha hizo, JAMHURI inavyo.

Chanzo chetu kimeongeza: “Wako madereva wengine wamepoteza kazi kutokana na ajali na kutokukubali kulipia hizo gharama na wapo madereva wengine ambao wanaendelea na adhabu.”

 

Mafao kwa wazee

Uchunguzi ulifanywa na JAMHURI umebaini kuwa baadhi ya watumishi, hasa madereva waliostaafu au kufukuzwa kazi; ama wamekuwa wakikosa mafao yao kwenye mifuko ya kijamii, au wanaambulia kiasi kidogo mno.

Imebainika kuwa mmoja wa madereva aliyefanya kazi kwa karibu miongo miwili (miaka 20), Lucas Kivuyo alipowenda NSSF aliambulia Sh 800,000 tu.

 

Polisi watuhumiwa

 Kuna madai kutoka kwa wafanyakazi kwamba Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, haliwezi kuchukua hatua zozote dhidi ya wamiliki na viongozi wa Leopard Tours kila wanapopelekewa malalamiko.

Baadhi ya wafanyakazi wamesema tofauti na ilivyozoeleka, Leopard Tours wakiwahitaji polisi, badala ya kuwafuata, polisi ndiyo huitwa kwenda kupewa ‘maelekezo’.

“Hapa ofisini polisi kuanzia wa vyeo vya chini hadi vya juu kabisa mkoa wanaitwa, na wanakuja hapa. Inasikitisha kuona polisi wakifika wanadiriki hata kumpigia saluti (jina linatajwa). Kama kuna wafanyakazi au mfanyakazi anayeonekana ‘mjuaji’, polisi wanaamuriwa wamkamate, na wao wanatii bila tatizo.

“Kuna magari mengi ya Jeshi la Polisi na ya maofisa wa polisi yanayofanyiwa matengenezo kwenye karakana ya Leopard Tours. Ni nadra sana gari la Leopard Tours kukamatwa barabarani, anayethubutu kulikamata atakiona cha moto,” kimesema chanzo chetu.

Majina ya polisi wanaotajwa tajwa kwenye sakata hili ni ya Faustine na Njau. Maelezo zaidi, pamoja na majina yao ya pili vitachapishwa kwenye JAMHURI matoleo yajayo baada ya kuzungumza nao.

Msemaji wa Leopard Tours, Mmbaga, ametafutwa lakini hakuwa tayari kupokea simu.

Mapema mwezi huu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Kazi na Vijana, Anthony Mavunde, katika ziara yake ya ghafla katika kampuni hiyo alipewa taarifa nyingi zinazoelezwa kwa zilikuwa za kumpotosha.

Kati ya taarifa hizo ni zile zilizohusu mishahara ya watumishi ambako Msemaji wa Leopard Tours, Mmbaga, alisema mishahara ya watumushi wa kampuni hiyo ni kati ya Sh 150,000 na Sh 300,000 kwa mwezi.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kuna tofauti kubwa kwenye mikataba ya ajira; na hati ya malipo kwa wafanyakazi wa Leopard Tours. Kilichoandikwa kwenye mikataba si kile kinacholipwa na kuonyeshwa kwenye hati ya malipo ya wafanyakazi ya kila mwezi.

“Nadhani Fazal anadhani kuwa hii serikali ni sawa na zile zilizopita Leopard Tours imesema kuwa inawalipa mishahara wafanyakazi wake kati ya Sh 150,000 na Sh 300,000. Hii siyo kweli kabisa tunaweza kuthibitisha hilo kwa sababu sisi guides tunalipwa kati ya dola 500 (Sh milioni 1.09) na dola 1,000 (Sh milioni 2.18) kwa mwezi,” amesema mmoja wa wafanyakazi wa Leopard Tours.

Pia uchunguzi umebaini kuwapo kwa idadi kadhaa ya raia wa kigeni katika kampuni hiyo wanaofanya kazi zikiwamo za kufungua malango na ulinzi; ambazo zingefanywa na Watanzania.

4184 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!