KYELA

NA MWANDISHI WETU

Bonde la Mto Songwe kijiografia lipo kusini magharibi mwa Tanzania na kaskazini mwa nchi ya Malawi, likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 4,243.

Bonde hili linajumuisha wilaya saba; kati ya hizo wilaya tano za Kyela, Ileje, Mbozi, Momba na Mbeya Vijijini zipo Tanzania, wakati Karonga na Chipita zikiwa upande wa Malawi.

Mto Songwe ni sehemu ya mpaka wa Tanzania na Malawi, wenye urefu wa kilomita 200.

Bonde la Mto Songwe lina wakazi 341,104 kwa mujibu wa tathmini ya watu iliyofanyika mwaka 2013.

Kuanzia upande wa chini wa Daraja la Kasumulu/Songwe lililopo kati ya Tanzania na Malawi wilayani Kyela (Tanzania) na Karonga (Malawi), Mto Songwe unapita katika uwanda tambarare ambao wakati wa mafuriko maji yake husambaa eneo kubwa la makazi na shughuli za kijamii na kusababisha makazi kutokalika, mali za watu kusombwa na maji na wakati mwingine kusababisha vifo.

Aidha, mto unaweza kubomoa kingo dhaifu na kubadili mkondo wake na kusababisha mpaka wa nchi hizi mbili kuhama. Hali hii husababisha jamii ya Tanzania na Malawi baada ya mafuriko kujikuta katika upande wa nchi nyingine.

Kutokana na changamoto za mafuriko, Serikali za Tanzania na Malawi zilianza majadiliano ya pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kudumu, kuanzia mwaka 1976.

Mwaka 1991 Tanzania na Malawi ziliingia makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wake ili kuimarisha uhusiano wa ujirani mwema na kuwezesha kuandaa Mradi wa Kudhibiti Kingo za Mto Songwe utakaotekelezwa kwa awamu tatu zinazohusisha upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na utekelezaji.

Julai, 2001 serikali hizo zilianza utekelezaji wa Programu ya Pamoja ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe chini ya Sekretarieti ya Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe kwa kufanya upembuzi yakinifu na kubaini changamoto hizo zinaweza kutatuliwa kwa ujenzi wa mabwawa matatu ya kuzuia mafuriko pamoja na maji yanayodhibitiwa yanaweza kutumika kwa ajili ya kunywa na matumizi mengine mbalimbali kama kuzalisha umeme, umwagiliaji, ufugaji wa samaki na kuendeleza utalii.

Uwepo wa fursa hizi katika Bonde la Mto Songwe ndilo chimbuko la kuanzishwa kwa Programu ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe, ikihusisha sekta mtambuka kupitia miradi mbalimbali na awamu ya pili itafuatia ya kufanya usanifu wa kina wa mradi, itakayohusisha kuandaa dira ya kuendeleza Bonde la Mto Songwe ya mwaka 2050 pamoja na mpango wa utekelezaji wa Programu ya Bonde la Mto Songwe katika kipindi cha miaka kumi baada ya awamu ya kwanza ya upembuzi yakinifu kukamilika.

Utekelezaji na faida za mradi

Utekelezaji wa miradi chini ya Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe imegawanyika katika maeneo makuu matatu:

i) Utekelezaji wa miradi tangulizi (lead projects) inayohusisha kuimarisha taasisi kwa kuijengea uwezo katika usimamizi wa rasilimali za maji, uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za asili, huduma ya usambazaji maji vijijini na miradi ya maendeleo ya jamiii.

ii) Utekelezaji wa miradi mikubwa (major projects) inayohusisha ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini pamoja na mradi wa umeme na miundombinu yake, miradi ya skimu za umwagiliaji na miradi ya kipaumbele kwa ajili ya jamii.

iii) Utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kiuchumi (economic development projects) itakayotekelezwa baada ya kukamilika kwa Bwawa la Songwe Chini na miundombinu ya umeme itakayojumuisha viwanda vidogo na vya kati, maendeleo ya uvuvi na utalii.

Kazi ya utekelezaji wa miradi tangulizi tayari imeanza kwa kipindi cha miaka minne tangu Machi 2020 hadi Juni 2023 na inahusisha uimarishaji wa taasisi na usimamizi wa majishirikishi, uboreshaji wa mfumo wa utoaji wa taarifa za awali za majanga ya mafuriko, usimamizi wa pamoja wa rasilimali za asili unaoshirikisha jamii unaolenga uhifadhi wa misitu, kidaka maji (water catchment) ardhi na kuimarisha mifumo ya usimamizi/upatikanaji wa taarifa na ramani kupitia Geographical Information System (GIS) na Management Information System (MIS).

Aidha, mradi wa ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini utakaogharimu takriban dola za Marekani milioni 550 unajumuisha miundombinu ya kuzalisha umeme na skimu mbili za umwagiliaji hekta 3,150 kwa upande wa Tanzania na hekta 3,050 upande wa Malawi.

Vilevile mradi wa usambazaji majisafi na salama katika miji midogo ya Kasumulu (Tanzania) na Songwe (Malawi) utakaonufaisha wananchi 260,000 unakwenda pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la Songwe Chini. 

Lakini kwa kuzingatia umuhimu wa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa miji hii miwili ya mpakani, serikali zote mbili zimepanga kutafuta njia mbadala ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi wake. 

Kwa sasa hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa One Stop Border Post (OSBP) utakaotoa maji kwenye chemchemi na visima katika miji hiyo zimeanza.

Pia miradi ya usambazaji maji katika wilaya zote saba za Bonde la Mto Songwe ambayo haiendani na Bonde la Songwe Chini itakayonufaisha wananchi 200,000 ambapo kazi ya upembuzi yakinifu wa awali (Pre-feasibility Study) imekwisha kukamilika na mawasiliano yanaendelea na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kupata fedha zaidi kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu.

Uwekezaji mkubwa wa fedha kiasi cha dola za Marekani milioni 577 kwenye utekelezaji wa mradi huo utakuwa na manufaa mengi kwa Tanzania katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha huduma ya majisafi na salama kuwafikia wananchi 460,000 ifikapo mwaka 2025, kupunguza athari za mafuriko kwa wananchi wasiopungua 52,000, kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa majishirikishi, kuboresha hali ya maisha ya wananchi katika Bonde la Mto Songwe, kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa mazao utakaonufaisha kaya 5,500, kuongeza huduma ya umeme vijijini kwa asilimia 60 vilivyopo katika Bonde la Mto Songwe na kuimarisha ushirikiano na mahusiano ya ujirani mwema kati ya Tanzania na Malawi.

Makala hii imetolewa na Idara ya Habari, Wizara ya Maji.


Kaimu Katibu Mtendaji Sekretarieti ya Bonde la Mto Songwe, Mhandisi Gabriel Kalinga, akitoa maelezo kuhusu Mto Songwe kwa wajumbe wa Bodi ya Maji ya Taifa walipokuwa ziarani mkoani Mbeya.

By Jamhuri