Nimekwenda katika kijiji kimoja Iringa. Nadhani safari hiyo tulikuwa na Mheshimiwa Ng’wanamila – hii anayoimba anasifu mambo aliyojifunza Njombe na Iringa.

Tumekwenda katika Kijiji kimoja cha Iringa- ni kijiji cha Waziri wa Kilimo, Joseph Mungai.

Akanipeleka Joseph pale au tuseme, tumekutana pale na Joseph. Sasa, wamenionyesha shughuli zao nzuri sana. Halafu baada ya hapo, wananipeleka kwenye shamba lao la mahindi.

Lakini kabla ya hapo, Mwenyekiti ananieleza. Mwanyekiti anajivuna sana anasema, “Mwalimu mwaka huu tumelima kilimo cha kisasa – kilimo kizuri sana.

Tumevuna magunia”, sijui alisema manane au kumi (kicheko), “magunia kumi kwa eka”. Nadhani alisema magunia kumi kwa eka.

Sasa mimi tumezungumza huku tukiwa tumesimama nikamwambia “Tazama, Mwenyekiti, mimi ningelikuwa wewe, nisingalileta jambo hili.

Nisingethubutu kusema kwamba mwaka huu eti tumevuna magunia kumi- magunia kumi si ya kutamka; ni ya kukaa nayo mwenyewe tu (kicheko).

Maana wengine Tanzania, wanalima nadhani wakati huo, sijui tunatoka Njombe, au ndio tunakwenda; wanapata magunia 20, 25, 28.

Na Zambia sasa hivi, wako mabepari kule wanalima, wanapata magunia mpaka 43 eka moja. Sasa mwenzangu wewe unapata magunia kumi, unanitamkia hivi kwa makeke (kicheko).

Unanitamkia magunia kumi kwa makeke, Mwenyekiti? Mwenyekiti, mimi ningekuwa wewe, hii ingekuwa siri ya kijiji chetu na nisingetamka mpaka ukifikia magunia kumi na tano, anza kusema.

Madhali wenzetu wanafikisha 28, 30, 40; basi wewe usianze kusema mpaka umefika angalao magunia 15 hivi ndiyo uanze kusema.

Nikasema hivyo Mwenyekiti na Mwenyekiti mwungwana. Akaniambia ndiyo, ndiyo, sawasawa. Sasa, tumetoka hapo, nimekwenda nikaona mahindi yao mazuri.

Mahindi yao wakanionyesha, mazuri. Sasa hapo hapo wakati wananionyesha, ndiyo sasa wananisomea risala yao. Mwalimu, mwaka huu sisi tumefanikiwa sana, wanarudia maneno yale yale ya Mwenyekiti.

Tumepata magunia kumi kwa eka; zamani tulikuwa tunapata debe moja! Ehe! Sasa ikabidi lazima katika mkutano wa hadhara nimwombe radhi Mwenyekiti.

Nikamwomba radhi Mwenyekiti, niwie radhi, wakati unajivuna na magunia yako kumi, sikujua mnakotoka (kicheko). Sikujua mnakotoka.

Ningejua kama mnatoka kwenye debe moja na mwaka mmoja tu mmefika kwenye magunia kumi! Ningekusifu sana Mwenyekiti.

Nisingekulaumu. Basi hivyo ndivyo ilivyo katika nchi. Nimetembelea mikoa wa Mtwara. Ananitembeza Bwana Shamba. Bwana Shamba wa kijiji ananitembeza.

Ananionyesha mahindi, wameyapanga panga. Anajivuna sana, ananitembeza hivi. Bwana Shamba, siyo Mwenyekiti, Bwana Shamba; ananiambia kwamba mwaka huu magunia manane Mwalimu, tumefika.

Sasa wewe ni Bwana Shamba?” Nikamwuliza. Akasema, “Ndiyo”. “Magunia manane, sasa kwa nini unanisifia magunia manane? Akasema, “Tulikuwa tunapata gunia moja hapa kwa eka”.

Kwa hiyo ndiyo hiyo wananchi nawaambieni kwamba, anaweza mtu akaridhika na magunia yake manane haya, akaridhika na magunia yake kumi kwa sababu kwa kweli.

Hujui kilimo cha leo kinaweza kikafika wapi. Kwa hiyo nasema, nawaombeni viongozi wa TANU kwanza, mtambue kwamba tuko nyuma ajabu katika kilimo, nyuma kabisa!

Hatuna shamba zuri mahali popote! Ah, labda nikisema hivyo, naongeza chumvi. Viko vishamba, viko vishamba vizuri vizuri mahali, lakini Tanzania yenyewe haina mashamba mazuri hata kidogo – haina. Na hilo ni jambo la kutambua.

Sasa nasema kwamba, tumeanza kupiga kelele, tumeanza kujaribu kutimiza masharti ya kilimo – sasa sijui wenzangu wangapi mmesoma mwongozo ule wa Siasa ni Kilimo?

Maana mle yamo maelekezo mepesi sana ambayo yanaweza kufuatwa na kila watu mahali pao. Wenye mahindi mahali pao, wajitahidi kujua habari za mtama.

Wenye mtama mahali pao wajitahidi kujua habari za mahindi. Wenye kahawa mahali pao, wajue – sasa sijui.

Waheshimiwa humu, tumejitahidi na nasema tumefanya na ghasia nyingi tumefanya katika kujaribu kuelekeza, sasa sijui wenzangu mko darasa la ngapi la kilimo bora?

Maana huku kipofu anakwenda anamwongoza kipofu mwenzake, mwishowe mnaweza kutumbukia shimoni. Sasa, sijui wenzangu mmefika wapi.

Mbolea, tumeanza kutumia. Mwaka 1971 tulitumia mbolea tani 41,850; lakini matumizi yetu ya mbolea yaliongezeka. Mwaka huu tunasikia kutumia karibu tani thelathini elfu zaidi.

Tunakisia kutumia tani 71,300. Tunacho kiwanda, hakitoshi lakini makisio waliyoniambia ni kwamba, mwaka huu  wanaweza kutengeneza mbolea kiasi cha tani laki moja katika kiwanda chetu kile cha Tanga.

Sasa sijui. Tutapata maelezo ya kinaganaga mbele ya safari. Lakini mbolea imeanza kutumika. Na nadhani wananchi wengi wameanza kuelewa mbolea kidogo. Zamani mbolea ikitupwa. Unampa mtu mbolea halafu anatupa.

Karibu hapa, katika matembezi yangu, nadhani mlisikia katika redio, nikafurahi sana nikasikia watu wameanza kuibiana mbolea. Nikafurahi sana (kicheko).

Hakuna wizi umepata kunifurahisha kama wizi huo (kicheko)! Wizi mwingine wote unaniudhi; lakini kwamba zamani watu unawapa mbolea, wanatupa.

 Wengine  wanafanya chokaa wanapakia majumba yao – wanafanya chokaa, halafu mnafika mahali wanaanza kuibiana mbolea, nikiona tumepiga hatua kweli kweli ya maendeleo!

Watu wameanza kuelewa mbolea. Hata dawa hizi za kunyunyizia, za pamba na zingine, watu wameanza kuzielewa vizuri sana. Hata hizi mbegu bora, kina Ng’winamila wanaanza kuimba “Hybrid”!

Ng’winamila zamani alikuwa hajui “Hybrid” sasa anajua habari ya Hybrid, anaweza kuimba habari ya Hybrid (kicheko).

Kwa hiyo, hatua tumepiga, lakini ni hatua kama ingekuwa kilimo ni darasa – na zamani hizo tulikuwa ni kama mtu asiyesoma kabisa, ama mtu yumo katika kidarasa kile tunachoita cha vidudu, sasa inawezekana tuko darasa la kwanza la kilimo, lakini tumeanza kuingia katika darasa la kwanza la kilimo.

Hilo, waheshimiwa ingawa limechukua muda mrefu, ni hatua ya mazao. Sasa, msingi wetu mmoja msingi wetu mmoja tuliosema wa kuweza kuharakisha maendeleo, tulisema ni vijiji. 

Maana, tulisema maendeleo haya yana utaratibu wake. Hata hayo tunayosema shule, zahanati na mengineyo maji mtampelekea Mzanaki, porini, vilimani.

Wazanaki hukaa kaa vilimani. Zamani zile wakigombana na Wamasai. Basi wanapenda, kila mmoja anatafuta mahali pake, anajipachika kwa kuwaogopa Wamasai.

Mpaka sasa wamo vilimani huko. Sasa leo tunataka maendeleo ya kisasa. Wapeni maji. sasa, Mzanaki huyu mtampitishia maji kilimani, utayapeleka kwa dawa gani?

Kwa hiyo, tulikubaliana vizuri sana kwamba kwa kweli jama tuishi pamoja. Jambo la kuishi pamoja ni la muhimu kabisa. Tumeanza kuzungumza habari ya kuishi pamoja siku nyingi sana.

Nimewaomba wakubwa wanichapishie tena hotuba niliyopata kuitoa kwa wabunge mwaka 1962 – hotuba yangu ya kwanza baada ya wananchi kunichagua kuwa Rais wa nchi.

Nilitoa hotuba – hotuba yangu ya kwanza kabisa. Nilieleza sana habari ya kuishi pamoja katika vijiji. Sasa ninawaomba ichapwe, mpewe wananchi; make nayo tena mfukoni! (makofi).

Inaeleza mambo mengi, lakini inakumbusha mambo ya kuishi pamoja vijijini.

3366 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!