Magufuli anakubalika kwa Watanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, wiki iliyopita alidhihirika kukubalika kwa wananchi kupitia utafiti wa Shirika la Twaweza, uliobainisha utendaji wake kukubalika kwa asilimia 71.
Utafiti huo uliopewa jina la ‘Matarajio na Matokeo; vipaumbele, utendaji na siasa nchini Tanzania’, umetokana na sauti za wananchi waliohojiwa maswali tisa tofauti kuhusiana na utendaji wa Rais Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, utafiti huo ambao umetokana na sauti za Watanzania 1,805 kutoka Tanzania Bara, unakionesha pia Chama Cha Mpinduzi (CCM) kuwa karibu zaidi na wananchi kwa asilimia 63 kikivizidi vyama vya siasa vyote nchini.
Utafiti huo uliofanyika mwezi Aprili mwaka huu, unaonesha kuwa Rais Magufuli anakubalika kwa  Watanzania saba kati ya kumi. Wanaume wanaukubali utendaji wa Rais Dk. Magufuli kwa asilimia 70, wanawake asilimia 73, Rais Magufuli anakubalika mijini kwa asilimia 70 na vijijini kwa asilimia 72.

Vijana wenye umri wa miaka kati ya 18-29 wanaukubali utendaji wa Rais kwa asilimia 68, wenye umri kati ya 30-39 wanamkubali kwa asilimia 67, wenye umri kati ya 40-59 wanaukubali utendaji wa Rais kwa asilimia 75, ambapo wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wanamkubali kwa asilimia 82.
Rais anakubalika kwa maskini sana kwa asilimia 75, masikini kwa asilimia 72, maisha ya kati asilimia 72, matajiri asilimia 72 na matajiri sana asilimia 66. Wasiokuwa na elimu ama wenye elimu ya msingi wanaukubali utendaji wa Rais kwa asilimia 75, waliohitimu elimu ya msingi wanamkubali kwa asilimia 74 na wenye elimu ya sekondari, elimu ya juu na ufundi wanamkubali kwa asilimia 63.
Wastani wa viwango vya kukubalika kwa marais wa Afrika kama vilivyorekodiwa katika tafiti 128 za utafiti wa ‘Afrobarometer’ tangu mwaka 1999 ni asilimia 63, hivyo Rais Dk. Magufuli anakubalika kwa zaidi ya asilimia tisa juu.
Miongoni mwa mambo ambayo yanamfanya Rais Magufuli kukubalika zaidi kwa wananchi ni pamoja na juhudi zake za kupambana na rushwa kwa nguvu zake zote ambapo utafiti huo unaonesha rushwa imeshuka kutoka asilimia 28 mwaka 2015 hadi asilimia 10 mwaka huu.

Utafiti huo unaonesha kuwa wananchi wamesema kuwa changamoto katika sekta za afya, elimu na maji zimepunguzwa kwa kiwango kikubwa tangu Rais Magufuli aingie madarakani.
Pamoja na mambo mengine, utafiti huo umeonesha kuwa CCM inakubalika zaidi kwa Watanzania na kwamba ni chama ambacho kipo karibu zaidi na wananchi kuliko vyama vyote nchini.
Utafiti unaonesha asilimia 63 ya wananchi wanasema wapo karibu zaidi na CCM kuliko chama kingine chochote. Asilimia 17 wapo karibu na chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na idadi ndogo wapo karibu na chama cha wananchi (CUF) kwa asilimia 1, ACT-Wazalendo kwa asilimia 1 na NCCR-Mageuzi kwa asilimia 1. Asilimia 17 wanasema hawana ukaribu na chama chochote.
Utafiti unaonesha kuwa asilimia 32 ya wananchi waliosema wapo karibu na chama cha Chadema mwaka 2013 ni asilimia 17 tu ya wanaosema hivyo mwaka huu. Wakati huohuo, uungwaji mkono chama cha CUF Tanzania Bara umeshuka kutoka asilimia 4 hadi asilimia 1 mwaka huu.

Utafiti unaonesha kuwa pale CCM inapoungwa mkono kwa kiwango kidogo haimaanishi kuwa Chadema inaungwa mkono kwa kiwango kikubwa, hasa katika maeneo ya mijini na miongoni mwa wasomi.
Hata hivyo, utafiti unaonesha kuwa miongoni mwa makundi yaliyofanyiwa utafiti huo, wananchi wasiofungamana na chama chochote ni wengi kuliko wale walio karibu na Chadema.
Kwa kuzingatia kigezo cha CCM kuwa chama tawala na Chadema kuwa chama kikuu cha Upinzani nchini, utafiti unaonesha katika kipengele cha kuwa karibu na wananchi kama ifuatavyo:
Mwaka 2012, Chadema ilikuwa karibu zaidi na wananchi kwa asilimia ishirini na sita ambapo CCM ilikuwa karibu kwa asilimia sitini na tano. Mwaka 2013 Chadema ilikuwa na asilimia 32 na CCM asilimia 54.Mwaka 2014 Chadema asilimia 27 na CCM asilimia 54. Mwaka 2015 Chadema asilimia 25 na CCM asilimia 62 na mwaka huu Chadema ipo karibu na wananchi kwa asilimia 17 na CCM asilimia 63.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara, anaupinga utafiti huo wa Twaweza unaoonesha Chadema kushuka, akisema kuwa ni wa ajabu kwani katika kipindi hiki Chadema ndiyo ina wabunge na madiwani wengi kuliko muda wowote ule.
“Sisi hatujui wametumia vigezo gani, wamemhoji nani na maelekezo ya nani? Sisi tumezuiliwa kufanya siasa nchini kote. Tungeruhusiwa kufanya mikutano yetu kama wenzetu tungelinganisha wingi wa watu wanaotuunga mkono. Sisi hatujashuka katika kiwango chetu,” amesema Waitara.

“Wewe unaona nchi nzima tumefungwa midomo. Hatuwezi kusema lolote. Siasa ni kuzungumza na wananchi kuhusu mambo yanayolihusu Taifa lakini sisi tumezuiwa. Hii ni ripoti ya kutengenezwa, watu wameitwa na wameelekezwa wahoji watu ambao wako Chama Cha Mapinduzi ndiyo wanakuja na majibu hayo,” amesema Waitara.
Hata hivyo Waitara ameikubali ripoti hiyohiyo kwa upande wa takwimu zinazohusu kiwango cha chakula nchini.
“Hilo ni sahihi na sisi tumelizungumza sana ila lilionekana kuwa ni jambo la kisiasa,” amesema Waitara.
Utafiti hup pia umeonesha kuwa umaarufu wa Rais Magufuli umepungua kidogo kutoka asilimia tisini na sita mwezi Septemba mwaka jana hadi asilimia 71 April mwaka huu.
JAMHURI limezungumza na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Humphrey Polepole, kuhusiana na Rais Magufuli kukubalika miongoni mwa wananchi na madai ya kwamba vyama vya Upinzani vimeporomoka katika hadhi ya kukubali kwa wananchi, kuwa kumechangiwa na zuio la mikutano ya siasa.

Polepole anasema kuwa mikutano ya hadhara yenye maudhui ya kisiasa haijazuiliwa kwa wapinzani pekee bali hata kwa wanaCCM.
“Wenzetu wanasema kuwa wamefungwa midomo, siasa si kupiga domo, siasa ni kutoa uongozi safi na si kupiga domo, ndiyo maana hata mimi siongei sana. Tunasimamia utekelezaji wa sera, hii kupiga domo ndiyo imetufikisha mahala tumeharibikiwa kiasi hiki.”
“Mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya Ubungo, hapo Kibamba na Ubungo wenzetu walikuwa wakiandamana kila leo, hawataki utekelezaji wa mambo ya maendeleo. Wanachojua ni kuhamasisha wananchi kuandamana. Mbona Arusha, Kilimanjaro na Mbeya hawawahamasishi watu wao waandamane?” amehoji Polepole.
“Rais na CCM wameendelea kukubalika katika jamii ya Watanzania kutokana na utekelezaji wake na siyo kupiga domo. Wanang’ang’ania wapige domo na waandamane kwenye maeneo ambayo CCM imeaminiwa na wananchi kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo,” amesema Polepole.

Amesema Rais na CCM wamejipanga zaidi katika mwaka ujao wa bajeti kuwafikishia huduma muhimu Watanzania.
Jackson Pete (27), mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam, amesema kuwa vijana wametokea kuukubali utendaji wa Rais Magufuli kutokana na udhibiti anaoufanya katika rasilimali za Taifa na kudhibiti nidhamu ya watumishi wa umma.
“Rais Magufuli mimi mwenyewe namkubali sana. Huo utafiti waliofanya wa kukubalika kwa Rais nauunga mkono. Siku hizi kwenye ofisi za umma tunaheshimiana. Kafuta safari za nje, kaondoa wafanyakazi hewa na kuzuia madini ni mambo ambayo yamenifurahisha sana,” amesema Peter.

1330 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons