Nafahamu leo zimepita siku kadhaa tangu Rais John Magufuli afanye uamuzi wa kuwatumbua Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Dk. Charles Tizeba na huyu aliyekuwa na dhamana ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage. Sijaandika lolote kuhusu kutumbuliwa kwao. Wasomaji wangu mmekuwa mkiniuliza, nina kauli gani? Nikawambia subirini.

Sitanii, nakiri kwamba sina ugomvi binafsi na Dk. Tizeba au Mwijage, ila katika kutetea nchi walistahili kuondoka ofisini miezi miwili baada ya uteuzi wako. Nizungumzie mmoja mmoja. Dk. Tizeba ameua kilimo. Tangu ameshika wadhifa huu mbaazi zimekosa soko, korosho hadi umeingiza jeshi, kahawa ni maneno matupu na watu wanalia, vitunguu na nyanya vikawa haviwezi kwenda hata Kenya na mengine mengi.

Nikiacha haya matatizo ya soko la ndani, kimataifa Waziri Tizeba ametukwamisha kwa kiwango kikubwa. Niliandika kwa muda mrefu suala la soko la muhogo nchini China. Waziri huyu amekuwa akipuuza wazo la kulima muhogo nchini. Amekuwa haonyeshi kuwa na nia ya kusaidiana na Ubalozi wa Tanzania nchini China kujifunza tufanye nini muhogo na mazao mengine yapate soko China.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, amepata masoko mengi yanayohusiana na bidhaa za kilimo, lakini wapi bwana! Wizara ya Kilimo ndiye mchawi wa mkulima hapa nchini. Fursa za kutoka nje ya nchi badala ya kuzichukua kwa mikono miwili, wanabaki kuishi kwa historia. Nilitarajia wizara iombe kibali kwenda kujifunza nchini China na kwingine. Ifungue soko mtandao.

Muhogo kwa mfano nilioupigia debe, unazalisha wanga, unga wa kula, pombe, mafuta ya gari na vitu vingine vingi ambavyo vina soko si la nje tu, bali hata hapa ndani kwetu. Kinachohitajika ni Wizara ya Kilimo kujipa jukumu la kwenda kujifunza kwa wenzetu walioendelea katika sekta ya kilimo na kutekeleza tunayojifunza. Kinyume chake, Tizeba alikuwa anavaa suti na kuona Balile anayeandika makala za kumchagiza aende shambani na kufuata teknolojia na masoko nje ya nchi hamtakii mema.

Kwa upande wake Mwijage naye ni kituko cha mwaka. Nilipata kwenda kumsalimia tukiwa pale kwa Chipe kula chakula cha mchana Dodoma, majibu aliyonipa sijawahi kuyasahau. Alinionyesha nyodo za kufa mtu. Akaanza kunifahamisha kuwa yeye ni waziri. Nikajiuliza kama yuko sawa. Nikajiuliza anasahauje kwamba mimi kwa miaka karibu 24 sasa niliyofanya uandishi wa habari siwezi kuwa mwepesi wa kusahau mawaziri wa nchi hii!

Kero kubwa niliyoiona ni kuwa Mwijage alizamisha uchumi wa nchi hii katika viwanda pale aliposema: “Ukiwa na cherehani tatu tayari una kiwanda.” Hii ilinisikitisha. Wakati Serikali ya Tanzania inatajwa kuwa na waajiriwa 450,000 hivi, nimejaribu kuangalia viwanda vya nchi za wenzetu vinaajiri watu wangapi.

Nimeangalia kiwanda cha ndege za Boeing. Hadi mwishoni mwa wiki kilikuwa kimeajiri wafanyakazi 141,322. Kampuni ya magari ya Toyota ya Japan inaajiri wafanyakazi 369,124. Idadi ya wafanyakazi katika kampuni hizi mbili jumla yake ni 510,446. Hizi ni kampuni binafsi mbili tu, zinaajiri watu wengi kuliko idadi ya waajiriwa wote wa Serikali ya Tanzania.

Sitanii, niliposikia Mwijage anasema ukiwa na cherehani tatu tayari una kiwanda, nilijua nchi haifiki popote. Nikajiuliza imekuwaje Rais Magufuli ukakubali kuwa na mawaziri ambao uwezo wao wa kufikiri uko chini kiasi hiki? Kwa nchi za wenzetu kampuni moja inakuwa na wafanyakazi hadi 400,000. Sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi duniani. Tunataka viwanda si vibanda vya SIDO.

Nahitimisha makala hii kwa kukupongeza Rais Magufuli kuwatengua wawili hawa. Ila bado unao mawaziri wawili wanaokuingiza chaka. Mmoja anakwambia wanaofunga biashara ni wapiga dili, baadaye anakwambia makusanyo ya kodi yameshindikana kutokana na biashara nyingi kufungwa. Mwingine alikuwa mwalimu mzuri wa chuo kikuu, lakini sasa akili yake ameiweka likizo. Anajifanya anakushauri, lakini ushauri anaokupa ni kinyume na aliyofundisha hadi alipostaafu akiwa na umri wa miaka 60. Fikiria, chukua hatua.

841 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!