Ndugu mhariri, mimi mahabusu Said Mbaraka, ninaomba kufikisha malalamiko yangu ya kubambikiwa kesi ya kukutwa na gramu 41 za dawa za kulevya aina ya Heroin kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sylvester Mwakitalu.

Kesi hiyo (EC. No 07/202) iliyopo Mahakama ya Shinyanga nilibambikiwa na aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Serikali wilayani Kahama (jina linahifadhiwa) baada ya kuingia kwenye mgogoro naye Novemba 30, 2015 kupitia mteja aliyekuwa ananiletea vipuri vya Land Rover kutoka DRC.

Nilifanya biashara na ofisa huyo kwa muda mrefu na alikuwa akija dukani kwangu kununua vipuri vya gari lake hadi tulipozoeana, kisha akaniomba nimuunganishe na yule mteja kutoka DRC kwa sababu alikuwa anakwenda Japan na Dubai kuleta magari mengi ili iwe rahisi kwake kupata vipuri vya gari lake kwa kuwa dukani kwangu havikupatikana.

Sikuwa mbishi, nilimpatia namba za simu za huyo mteja kutoka DRC na ofisa huyo akanisisitiza akija nimjulishe ili waonane kwa kuwa walishakuwa na mawasiliano siku za nyuma bila mimi kufahamu nini walichozungumza.

Nilifikiria labda alitaka kununua gari, ndipo Novemba 30, 2015 kama nilivyosema hapo juu yule mteja kutoka DRC alipita dukani kwangu kutoka Dar es Salaam na mimi nilimpigia simu ofisa yule, akanielekeza nimpeleke maeneo ya Hospitali ya Kahama iliyopo mkabala na wanakotengeneza majeneza.

Tukamkuta kwenye gari lake, Nissan Patrol, jeupe, akasema mteja wangu aingie mimi nimsubiri. Wakazungumza kwa dakika 30.

Baada ya kumaliza mazungumzo yao, ofisa huyo aliniita kisha akaniambia kuwa amefanya biashara na yule mteja kutoka DRC, nikashuhudia akikabidhiwa fedha katika boksi. Akabaki akimdai Sh milioni 30; akasema akimalizia malipo hayo, mimi nitapewa Sh milioni 10.

Mheshimiwa DPP, tulipotoka hapo nilimuuliza yule rafiki yangu wa DRC; ni biashara gani wamefanya? Hakunificha. Alifungua mfuko na kunionyesha dawa za kulevya zenye uzito wa karibu kilo moja hivi. Akadai kuwa ameuziwa na ofisa yule wa serikali, ila hana uhakika kama ni nzima. Akaahidi kunijulisha akifika kwao. Alipoondoka hakuonekana tena hadi leo!

Pamoja na mambo mengine, hilo deni la Sh milioni 30 za jamaa yetu wa DRC ndiyo zinaniletea shida hadi sasa licha ya kuahidi kuwa nitamlipa kwa namna yoyote ile.

Mheshimiwa DPP, kwa ufupi ninakumbuka usiku wa Februari 26, 2016 alikuja nyumbani kwangu ofisa huyo wa serikali akiwa na askari, wakafanya upekuzi wao waliokuwa wameshajipanga kuufanya. Wakanipa kesi ya kukutwa na gramu kadhaa za dawa za kulevya, wakidai wamezipata nyumbani kwangu! 

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani Machi 1, 2016 na ikasababisha nifungwe miaka mitatu gerezani kwa ushahidi wa kutengeneza. Nilikata rufaa kupitia kesi namba 125/2016 katika Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga na Februari 22, 2017 Jaji Victoria Makani akaniachiwa huru.

Mheshimiwa DPP, uhuru wangu nilioupata kisheria ulimuumiza sana ofisa huyo na baada ya kuniona mtaani, hakuamini. Alidhani labda nimetoroka gerezani. Akaanza kunifuatilia. Akaniweka chini ya ulinzi na kupiga simu sehemu mbalimbali. Alipopata ukweli kuhusu kushinda rufaa, alisema suala la pesa zake, Sh milioni 30, liko pale pale na usalama wangu ni kulipa fedha hizo, bila hivyo nitamtambua yeye ni nani.

Baada ya muda kidogo kupita ndipo tena Desemba 28, 2018 alikuja nyumbani kwangu akiongozana na askari polisi na mtendaji wa kata na watu wengine nisiowafahamu, kufanya upekuzi. 

Mheshimiwa DPP, baada ya kumalizika upekuzi na watu wote tulioshuhudia kuridhika kwamba hakuna kilichopatikana; ndipo ofisa huyo akiwa amebaki nyuma, nikamuona akiweka kitu katika gunia la mkaa. Nikapiga kelele, wana familia na askari polisi wakasogea pamoja na uongozi wa mtaa akiwamo mtendaji. Upekuzi ukasitishwa, tukaenda Kituo cha Polisi Kahama na jalada likafunguliwa mbele ya OCD Sofia Jongo. Alitaka kunibambikia gramu nne za heroin!

Sikuchoka kufuatilia kesi hiyo aliyotaka kunibambikia ofisa huyo. Ikabainika kuwa dawa zile ni zake, kesi imezungushwa na sasa ni miaka miwili hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa DPP, suala hilo likageuka kizungumkuti kwangu kwa kuwa dawa alizokamatwa nazo ofisa huyo zimeniletea shida kwa sababu nilifuatilia kujua kitakachoendelea dhidi yake kumbe nilichochea kuni katika moto kwa sababu nilionekana hatari kwake, akimaanisha nitamtolea siri yake.

Baada ya hapo, ndipo nikaanza kufuatwa na vitisho vikali nilipe Sh milioni 30 na kuambiwa nisipolipa nitapotezwa na hata nikihama mji, atanipata tu.

Hali hiyo ilinifanya kwenda kutoa taarifa kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya kwa wakati huo, Fadhili Mkulo, kwa kudhani kwamba pengine taarifa ile inaweza kuwa ni kinga kwangu huku nikiendelea na shughuli zangu za kawaida. Kumbe palikuwa na hatari kubwa mbele yangu ambayo alishaniandalia.

Nakumbuka alfajiri ya Mei 9, 2017 wakati ninafanya mazoezi na mbwa wangu wawili, nilivamiwa na watu walioongozwa na ofisa huyo na nikapigwa hadi nikavunjwa mikono na kupasuliwa kichwa kisha wale mbwa nao walipigwa hadi mmoja akafa.

Wakaniteka nikapelekwa sehemu nisiyoijua nikiwa nimezimia na nilipozinduka, nilijikuta ndani ya ngome nimefungwa kamba kwenye mti wa mwembe.

Nilipiga kelele na kutaka msaada, ndipo muda wa jioni alikuja mtu na kunihoji: “Wewe fala vipi? Shida ni nini dhidi yako na ofisa huyo?”

Nikampa historia yote. Yule mtu aligeuka na kutikisa kichwa, akaondoka na sikumuona tena.

Baadaye muda kama wa saa 3:30 usiku alikuja ofisa huyo na vijana wake. Wakanipiga tena na kunitonesha yale majeraha na hali ikazidi kuwa mbaya. Waliniinua na kunitumbukiza ndani ya buti ya gari wakaenda kunitelekeza karibu na Kanisa Katoliki, mkabala na shule ya uuguzi.

Wasamaria wema ndio waliniokota na kunipeleka Hospitali ya Wilaya. Baadhi yao pamoja na wauguzi, walinifahamu. Wakapiga simu kwa mke wangu, akaja kuendelea kunisaidia ili nipate matibabu. Alishauriwa na madaktari aende Kituo cha Polisi Kahama apate PF3.

Mheshimiwa DPP, pale kituoni tayari nguvu za ofisa yule zilishaenea kwa sababu mke wangu hakupewa PF3 na ilibidi arudi hospitalini. Tukaanza kumtafuta mkuu wa wilaya. Bahati nzuri tukampata, akamuamuru nitibiwe.

Baada ya matibabu zilipita wiki tatu ndipo Juni 26, 2017 ukaja ugeni wa Mkuu wa Mkoa kutembelea Kahama, nilipopata taarifa hizo nilifanya jitihada za kuonana naye nikiwa na majeraha yangu. Nilimsimulia matukio yote na akaniambia kwamba itakuwa bora zaidi nikimuelezea kwa maandishi. 

Mheshimiwa DPP, kwa msaada nilioupata katika tume aliyoituma mkuu wa mkoa kufuatilia jambo hili, ndipo ofisa huyo akatulia kidogo. Nikapata muda wa kupeleka kesi ya madai (namba 28/2018) mahakamani ya kujeruhiwa na kusababishiwa ulemavu wa kudumu na gharama za kunipotezea muda kwa kesi alizonibambikizia.

Hapo tena nikachokoza vita, kwani baada ya yeye kupokea wito kutakiwa afike mahakamani, ikawa shida kwangu, kwa kuwa kila wakati inapopangwa kesi lazima nikamatwe na kuwekwa kituoni na tarehe ikipita ninaachiwa, hali hiyo iliendelea huku kesi nayo ikiendelea na baada ya mvutano mkali alitumia nguvu kwa madaraka aliyonayo na mahakama ya chini ikampa ushindi.

Mheshimiwa DPP, nami sikuridhika nikakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga na kesi ikasajiliwa kwa namba 22/2019. Hapa tena baada ya kugundua alikuwa ananitafuta mara kwa mara na kunipa onyo kuwa kama sitaki kulipa Sh milioni 30 kwa kujifanya mjanja, atanionyesha na nitajua kuwa yeye ni nani.

Machi 28, 2020, Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga ilipanga kusikiliza kesi na yeye alipokea taarifa. Usiku wa Februari 27, 2020 kuamkia Februari 28, 2020, nilivamiwa na kundi kubwa la askari akiwamo Mtendaji wa Kata ya Malunga pamoja na kaimu ofisa mwingine mwandamizi wa serikali Wilaya ya Kahama wakitaka kufanya upekuzi nyumbani kwangu, lakini nikawagomea; nikawaambia wamuamshe Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa pamoja na majirani lakini waligoma na walivamia ndani na kuanza kupekua.

Kisha wakanikamata na kuiacha familia yangu wakaondoka na mimi hadi Kituo cha Polisi cha Kahama, nikalala siku moja; nikatolewa alfajiri ya Februari 28, 2020 na kusafirishwa hadi Dar es Salaam katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.

Nilikaa rumande siku zaidi ya 40 huku kitengo cha kufuatilia dawa za kulevya kikifuatilia kile walichodai ni mwenendo wangu na mtandao wa usafirishaji wa dawa hizo.

Mheshimiwa DPP, nikiwa kituoni hapo walinifuata na wakaniambia hakuna chochote, huenda tuna mambo yetu tu. Ndipo Aprili 7, 2020 tukarudi hadi Shinyanga na wala si Kahama tena nilikokamatwa.

Aprili 9, 2020 nikapelekwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya kukutwa na gramu 41 za dawa ya kulevya aina ya heroin.

Mheshimiwa DPP, kesi hii ina zaidi ya siku 205 huku upelelezi wake haujakamilika na wala dalili hazipo na njama za ofisa huyo zinaendelea hadi leo.

Kila tarehe ya kesi ya madai ikipangwa, sipelekwi mahakamani kwa mfano Septemba 15, 2020 sikupelekwa na kuna taarifa zinadai kuna njama zimepangwa mimi nisipelekwe.

Mheshimiwa DPP, kiukweli madai yangu katika kesi namba 22/2019 iliyopo mahakamani kwa sasa ndiyo yananiletea shida ya kuwa mahabusu gerezani na si vinginevyo na huo ndio ukweli. Naomba msaada wako wa kufuatilia kwa undani suala langu ili haki itendeke na ukweli ubainike.

501 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!